Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza:- Je, upi mkakati wa kuendelea kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa Makundi ya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu?

Supplementary Question 1

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nianze kwa kuishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa mapitio makubwa yaliyofanywa katika mfumo wa kutoa mikopo hii ya 10% iliyolenga kuleta ufanisi, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; pamoja na marekebisho ya kikanuni ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyazungumza mbele yetu hapa, ambayo yanalenga kuonesha kwamba pamoja na maombi kufanywa kwa njia ya vikundi, lakini bado kijana au mwanamke mmoja mmoja wana uwezo wa kutumia fedha hizo binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado vijana na wanawake wameendelea kupata changamoto ya kupata watu ambao wanaendana kimalengo, wakaunda kikundi na kwenda kuomba mikopo hii. Je, Serikali haioni haja ya kurekebisha tena kanuni hizi ili kuruhusu uombaji wa mikopo hii kwa vijana na wanawake kwa mtu mmoja mmoja? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; pamoja na hizi fedha za 10% zinazotolewa kama uwezeshaji wa mitaji kwa makundi maalum, tunayo Mifuko ya Uwezeshaji wa Vijana ambayo imekuwa ikikumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha kwa ajili ya changamoto za vijana hawa. Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inaongeza fedha katika Mifuko hii ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika na fedha hizi? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba nianze kumpongeza Wakili Msomi, Mheshimiwa Ng’wasi Damasi Kamani kwa maswali yake haya ambayo yana maslahi mapana kwa ajili ya vijana wa Tanzania, lakini pia wanawake na watu wenye ulemavu ambao na wenyewe ni wanufaika wa mikopo hii ya 10% ya mapato ya ndani katika halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza, ninaomba niendelee kutoa ufafanuzi kwamba kwa maboresho ya kanuni ambazo zinasimamia utoaji wa mikopo hii, kikundi kitaomba mkopo kama dhamana, lakini ndani ya kikundi kile wanakikundi wanaruhusiwa kukaa na kukubaliana wao wenyewe kila mmoja kuwa na mradi wake, lakini kwa maana ya uombaji wa mkopo, mkopo utaombwa na kikundi kama dhamana lakini haizuii mwanakikundi kuwa na mradi wake yeye mwenyewe ndani ya hicho kikundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni hizi hizi pia zinaruhusu mtu mwenye ulemavu aweze kukopa yeye mwenyewe, tofauti na utaratibu uliokuwepo awali ambao ulilazimu hadi kundi hili la watu wenye ulemavu waunde makundi. Kwa hiyo, Serikali inatambua mahitaji ya wanufaika wa mikopo hii na kila siku inaendelea kuboresha taratibu ili kuweza kufikia ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Mbunge; Serikali inatambua na ndio maana kuna jitihada hizi, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya uwekezaji mkubwa kuhakikisha anatengeneza mazingira ya kuwawezesha vijana pia na makundi haya mengine maalum kimtaji ili waweze kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuimarisha, siyo tu kwenye upande huu wa mikopo ya 10% ya halmashauri, bali pia Mifuko mingine ambayo ipo na ambayo inawezesha haya makundi maalum kupata mitaji. Mathalani kuna Mfuko huu wa Maendeleo ya Vijana ambao mwaka huu umeweza kuwekewa mtaji wa bilioni moja; hizi ni jitihada za makusudi kabisa. Pia kuna Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao umeweza kutoa mikopo ya zaidi ya bilioni 2.7. Vivyo hivyo kuna Mfuko Maalum wa Watu Wenye Ulemavu ambao unatoa mikopo ya kufikia bilioni 1.14. Zote hizo ni jitihada kwa ajili ya kuhakikisha mitaji inapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna fursa nyingine ambazo zinatengenezwa kwa ajili ya makundi mengine ya…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri ahsante ameshakuelewa…

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mining for better tomorrow upo kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo waweze kupata mitaji. Building for better tomorrow kwa ajili ya kuwawezesha vijana kuingia katika kilimo. Serikali itaendelea na jitihada hizi kwa sababu ni dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwawezesha vjana, wanawake, watu wenye ulemavu na Watanzania wote kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali. Ahsante.

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza:- Je, upi mkakati wa kuendelea kuwezesha upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa Makundi ya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu?

Supplementary Question 2

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali. Kwa kuwa mikopo hii 10% inatokana na mapato ya ndani ya halmashauri na kuna baadhi ya halmashauri ambazo mapato yake ni kidogo mfano Halmashauri ya Momba. Ni upi mbadala wa mikopo ya 10% ambao utafanana kwa sura hiyo hiyo ili kuzisaidia halmashauri ambazo hazina kipato kwa sababu baadhi ya wananchi wamekosa mikopo hiyo?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, ukiacha fursa tu hii ambayo inapatikana kwenye 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri bado kuna fursa nyingine nyingi. Nimetoka kutolea mfano hapa, kwamba kuna Mifuko mingine ya kuwawezesha wananchi kimitaji. Kwa mfano, mitaji ya huu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wenye mtaji wa bilioni moja, nimetaja pia Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao mpaka sasa umeweza kutoa zaidi ya bilioni 2.7 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna makundi mengine pia ambayo nimeyataja. Kwa mfano, kuna Mfuko Maalum wa Watu Wenye Ulemavu ambao ni bilioni 1.14 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi ambayo yote hii inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa hiyo, niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa fursa mbalimbali zitakazowawezesha kupata mitaji na kufanya shughuli za uzalishaji mali.