Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Magari ya Serikali yanakuwa na mfumo wa nishati ya gesi?

Supplementary Question 1

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ninashukuru kwa majibu ya Serikali lakini kuna changamoto nyingi sana zilizopo. Ili kuvutia Watanzania walio wengi kuweka mfumo wa gesi kwenye magari ni lazima Serikali iwe imejipanga. Je, Serikali haioni haja ya kushirikiana na Sekta Binafsi kuhakikisha kwamba magari yanayotumia gesi yanaweza kuingizwa moja kwa moja hapa Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kufunga mfumo wa gesi kwenye magari ni gharama kubwa sana, ni takriban shilingi milioni mbili hadi tatu ambazo Watanzania wengi wanashindwa ku-afford. Je, Serikali haioni haja ya kupunguza kodi kwenye vipuri ambavyo vinatumika kufungia magari hayo kwa sababu hatuna kiwanda cha vipuri hapa Tanzania? (Makofi)

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumia nishati ya gesi asilia na katika kuhakikisha tunaweka mazingira rafiki kwa Sekta Binafsi kushiriki, Bunge litakumbuka, mwaka 2023/2024 Serikali ilifuta kodi ya ushuru wa bidhaa kwa magari yote yanayoingizwa nchini yakiwa na mfumo unaotumia gesi asilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tayari taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi zimeanza kunufaika. Mwanzoni mwa mwezi Januari, taasisi yetu ya magari yaendayo kasi pale Dar es Salaam imeidhinishiwa magari 755 yaweze kuagizwa kuingia nchini yakiwa na mfumo wa gesi asilia na tayari zabuni hiyo imekwishatangazwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuona uwezekano wa kupunguza bei kwenye vipuri, ninapenda kulifahamisha Bunge kwamba kwa sasa Serikali, kwa maana ya Wizara ya Fedha na taasisi yake ya TRA na TPDC na Wizara ya Nishati wapo katika mapitio ya maeneo ambayo yanaweza kupata msamaha kwa ajili ya vipuri hivi ili viweze kupatikana kwa urahisi. Vilevile, TPDC ipo katika mkakati wa kutafuta wawekezaji watakaoweza kuwekeza viwanda hivi hapa nchini ili vipuri hivi viweze kuzalishwa kwa bei rahisi. (Makofi)