Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abdallah Dadi Chikota
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini utaanza?
Supplementary Question 1
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa zabuni ya awali imetangaza majengo mawili; jengo la kichomea taka na majengo ya watumishi nyumba nne; je, ni lini Serikali itatangaza zabuni ya jengo la mama na mtoto ambalo ni muhimu sana katika hospitali hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; hospitali hii ina upungufu mkubwa wa watumishi. Mahitaji ya watumishi ni zaidi ya 600, lakini waliopo sasa ni 277 tu. Serikali ina mpango gani wa kuleta watumishi katika Hospitali hii ya Kanda ya Kusini? Ninakushukuru.
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Chikota, kwa sababu amekuwa siyo mtu wa kupigania masuala ya jimbo lake tu, lakini amekuwa mtu anayepigania masuala ya Kanda ya Kusini na ndiyo maana hapa anaizungumzia Hospitali yao ya Kanda ya Kusini, Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kwamba ni lini tenda nyingine ya mama na mtoto itatangazwa? Ninataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutatangaza ndani ya wiki mbili na ninaomba tukitoka hapa mchana tukutane pale Wizarani, ataona process ambazo zinaendelea kwa ajili ya kutangaza hicho alichokisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili amesema suala la watumishi kwamba wako 270, lakini wanatakiwa zaidi ya 600. Ni kweli kwamba kwa ikama na ilivyo kwenye miongozo kwa kila hospitali ya kanda inatakiwa iwe na watumishi wangapi, kwa kweli hospitali ya Mtwara inaonesha kuwa na watumishi wachache. Hata hivyo, nimkumbushe kwamba hospitali hiyo ni mpya kama yeye mwenyewe anavyojua, wao ndiyo wameipigania mpaka ikaanza. Kwa sasa inatibu wagonjwa 102 kwa siku, wa ndani wanakuwa 40 na wengine kama 60 ndiyo wanatoka nje. Unaweza ukaona hata idadi ya watumishi ni wengi kuliko idadi ya wagonjwa wanaokuja kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tutaendelea kuongeza idadi ya watumishi jinsi ambavyo mahitaji yatakavyoendelea kujionyesha. Mpaka sasa ninataka kumhakikishia kweli kuna vitengo ambavyo vinahitaji kuwekewa watumishi, lakini idadi ya wagonjwa bado ni ndogo sana.
Name
Fatma Hassan Toufiq
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini utaanza?
Supplementary Question 2
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Ni nini mkakati wa Serikali wa kuongeza jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwani lililopo halitoshelezi? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa akipigania masuala ya Mkoa wa Dodoma. Ninamhakikishia kwamba kama mnavyojua tumekubaliana kuna ujenzi ambao unaanza karibuni kwa ajili ya hospitali zote za mikoa kujenga wodi za mama na watoto na wodi za watoto njiti ambao ni wale akinamama wanaojifungua watoto kabla ya muda wake na Dodoma siyo muda mrefu nayo itafikiwa.
Name
Zuena Athumani Bushiri
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini utaanza?
Supplementary Question 3
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza ninaishukuru Serikali ya Mama Samia kwa kazi nzuri iliyofanya ya kupeleka vitanda katika Vituo vya Afya vya Miamba pamoja na Ntii. Vitanda hivyo vimepelekwa lakini hakuna wodi za kulaza wagonjwa. Je, ni lini Serikali itajenga wodi hizo? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake makini. Nimemwona, siyo kwamba anazungumzia ambacho hajatembelea eneo husika, nimemwona akitembea kwenye kila kituo, kila wilaya kwenye Mkoa wa Kilimanjaro na hospitali yetu ya mkoa na KCMC akiangalia matatizo mbalimbali yanayosibu wanawake na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwambia Mheshimiwa Mbunge, kuna mkakati maalum ambao wenzetu wa TAMISEMI na sisi tunaendelea kuufanyia kazi ili kuhakikisha hayo matatizo yanakwenda kwisha moja kwa moja na kutakuwa na mambo makubwa sana yatatokea kwenye bajeti ya mwaka huu. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved