Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jafari Chege Wambura
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rorya
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Serikali itahimiza kuwa na zao la kimkakati Mkoa wa Mara?
Supplementary Question 1
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, mazao makuu matatu yanayolimwa Mkoa wa Mara kwa ajili ya chakula na sehemu ndogo kibiashara, ni pamoja na mahindi, mtama na muhogo; na kwa kuwa, mpaka sasa Mkoa wa Mara haujawa na mazao ya kimkakati na kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kuchukua mazao haya matatu, kuyaingiza kwenye Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ili kuendelea kuongeza thamani, kuimarisha soko na tija kwa mazao haya kwa wakulima wa Mkoa wa Mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; ni kuhusiana na vipimo vya afya ya udongo vinavyoendeshwa nchi nzima ikiwemo Mkoa wa Mara na Wilaya ya Rorya. Nataka kujua, je, ni lini Serikali itakamilisha mfumo huu ili kutengeneza road map na kutengeneza mfumo mzuri kwa wakulima? Kujua aina ya mazao wanayopaswa kulima kwenye maeneo yao ili kuendelea kuongeza tija kwa mazao ya kibiashara kwenye maeneo wanayolima hasa Mkoa wa Mara na Wilaya ya Rorya kwa ujumla wake?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri ambayo pia ni kuonesha namna ambavyo anawasimamia wananchi wake. Kwenye suala la kwanza kuhusu stakabadhi ghalani kwa mazao ambayo ameyatamka, tumepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge. Kinachofanyika hivi sasa tunaangalia uwepo wa miundombinu muhimu ikiwepo maghala na upatikanaji wa masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge hili, natoa maelekezo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mazao Mchanganyiko na Mazao ya Bustani (COPRA) iweze kufanya tathmini endapo muhogo na mtama yanaweza kuingizwa katika masuala ya stakabadhi ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili la kuhusiana na ikolojia, ni kweli Serikali imejipanga kuhakikisha inapima afya ya udongo nchi nzima na mpaka hivi sasa tumeshafikia mikoa karibu yote nchi nzima, imebaki mikoa nane ukiwemo Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumuhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, hatua ya kwanza iliyofanyika ni ugawaji wa vifaa vya upimaji wa afya ya udongo ikiwemo Halmashauri ya Rorya na yenyewe wamepata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri hivi sasa Wilaya ya Rorya wanafahamu mazao ya kuanzia kwa sababu ardhi ya Wilaya ya Rorya ni ya kitifutifu, yenye mchanga na mfinyanzi mweusi ambayo ina uwezo ku-support mazao kama pamba, muhogo na mtama. Nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ifikapo mwaka 2026, tutakamilisha ramani ya nchi nzima ya afya ya udongo ili tuwaongoze vizuri wananchi kujua mazao gani ya kulima katika eneo husika.
Name
Robert Chacha Maboto
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Primary Question
MHE. JAFARI W. CHEGE aliuliza:- Je, lini Serikali itahimiza kuwa na zao la kimkakati Mkoa wa Mara?
Supplementary Question 2
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Je, Serikali sasa haioni ni muda muafaka wa kurasimisha zao la mahindi kuwa zao la kibiashara katika Mkoa wa Mara?
Name
Anthony Peter Mavunde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Dodoma mjini
Answer
WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika kitabu cha bajeti cha zao la kilimo, tumeainisha mazao kulingana na mahitaji yake na vilevile umuhimu wake. Kutokana na mahitaji makubwa hivi sasa ya zao la mahindi kama alivyosema, Serikali iko mbioni kuona namna ambavyo pia tutalifanya zao hili kuwa kama sehemu ya zao kubwa la kibiashara kwa sababu ya mahitaji yake makubwa nje ya Tanzania na mahitaji makubwa yaliyopo katika Bara letu la Afrika.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved