Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Primary Question

MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kutoa mafunzo ya utaalam, mitaji, kuwaunganisha na masoko wajasiriamali wanaoongeza thamani ya mazao?

Supplementary Question 1

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amejibu, Jimbo la Bukene lina fursa za kiuchumi nyingi sana kupitia uchakataji na uongezaji thamani ya mazao kama kusindika mafuta ya alizeti, kuchakata mchele, kuchakata unga wa sembe.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inaweza kuwaleta wataalam wake Jimboni Bukene ili wakae na hao wajasiriamali wawafundishe namna ya kupata mitaji? Namna ya kuboresha bidhaa zao na kuwaunganisha kwenye masoko makubwa ili bidhaa zao ziweze kupata masoko?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Selemani Zedi kwa jitihada kubwa anazozifanya kuwasaidia wananchi wa Bukene ambao ni wajasiriamali kwenye sekta ya uongezaji thamani mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu ameweka nguvu kubwa katika Sekta ya Kilimo na sasa hatua inayofuata ni kuona namna gani haya anayosema Mheshimiwa Mbunge, moja, kuwasaidia wajasiriamali kusindika, kuongeza thamani mazao ya kilimo ikiwemo mahindi mchele na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, sisi kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, kupitia shirika letu la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) lakini pia kupitia TBS, tumeshaweka mpango na kuna bajeti mahususi ambayo moja inasaidia kutoa mafunzo, lakini pili kuwasaidia hata kujenga mabanda kwa maana sehemu nzuri za kutayarishia bidhaa zao za kilimo, lakini kuwasaidia teknolojia rahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba wataalam hawa kutoka SIDO na TBS ambako tayari tuna mpango huu wa kuwasaidia wajasiriamali wadogo, watakuja ili washirikiane na Mheshimiwa Mbunge kukaa na wananchi na wajasiriamali hawa ambao Mheshimiwa Mbunge anawasemea ili wapate mafunzo na teknolojia rahisi na mikopo, lakini zaidi kutafuta masoko kupitia maonesho na mipango mingine. Ninakushukuru.