Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:- Je, lini TBS itaweka utaratibu wa kutoa elimu kwa Wajasiriamali wadogo wanaojihusisha na biashara ya kusindika vyakula?

Supplementary Question 1

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. TBS inawasaidiaje wajasiriamali wadogo wanaoishi nje ya Dar es Salaam kupata huduma kwa njia rahisi badala ya kusafiri umbali mrefu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni kwa namna gani TBS inashughulikia changamoto ya upatikanaji wa vyeti vya ubora kwa wajasiriamali wadogo?

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninampongeza dada yangu Mbunge, Mheshimiwa Janeth Mahawanga kwa ufuatiliaji katika kuhakikisha wajasiriamali hapa nchini wanafanikiwa. Hii siyo mara ya kwanza na amekuwa akifuatilia, ninamshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, sisi kama Wizara kupitia TBS tuna ofisi za kanda katika kanda saba ambazo hizo zinasaidia kuhakikisha wajasiriamali hawalazimiki kuja au kwenda Dar es Salaam ili kupata huduma ya kupata ubora. Pili, katika kanda hizo hata kwenye mikoa pia tunao wawakilishi. Kwa hiyo, hii inawasaidia wajasiriamali hao kuhakikisha hawalazimiki kusafiri kwenda mpaka Dar es Salaam. Watatumia kwenye kanda hizo; tuna Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam), Kanda ya Magharibi, Kaskazini, Kusini, Kati (Dodoma), Nyanda za Juu Kusini na Mwanza. Pia, katika mikoa tunao wawakilishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ni kweli kumekuwa na changamoto wakati mwingine kupata hati au vyeti vya ubora na ndiyo maana sasa tumeanza kutoa au kuhudumia wajasiriamali kupitia njia za kimtandao (kielektroniki). Kwa hiyo, mjasiriamali kwenye mtandao ana dirisha ambapo atatoa maelezo ya bidhaa; yale maelezo yatatusaidia sisi au afisa wa TBS kupitia na kuona nini kinahitajika. Kama kuna masuala ya kumweleza kwenye mtandao atamweleza lakini kama ni kwenda kumfundisha atamfuata yeye, siyo mteja aje ofisini. Hii inapunguza ule usumbufu au kuchelewesha kutoa vyeti kwa wajasiriamali ambao wanataka nembo ya ubora kwa kuwafuata pale walipo. Ninakushukuru sana.