Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Medard Matogolo Kalemani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Primary Question
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI aliuliza:- Je, lini Serikali itakarabati shule kongwe za msingi katika Jimbo la Chato?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Pia ninatoa shukurani nyingi sana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi milioni 226 kwa ukarabati na kujenga madarasa manne kwenye Shule Kongwe ya Rudeba, Kata ya Iparamasa. Namshukuru Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri pia, kwa kututengea shilingi milioni 890, kwa ajili ya ukarabati wa madarasa mengine yaliyobaki. Kuna shule kongwe 169, nyingi zina uchakavu na kwa kweli fedha iliyotengwa nakubaliana nayo, lakini ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spuka, swali langu la kwanza; ninamwomba Mheshimiwa Waziri atembelee shule zote kongwe na ninamwomba atembelee ndani ya miezi hii miwili kabla Bunge halijakwisha akatoe tamko ili ukarabati uanze.
Mhshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; fedha hizi shilingi milioni 890 zitatoka lini ili ujenzi na ukarabati wa madarasa ya shule zote kongwe ikiwemo Ilyamchele, Nyambogo, Ichwankima, Kasenga, Nyamirembe, Buzirayombo nao ufanyike kwa haraka? Ahsante.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani kwa kutaka kuhakikisha kwamba, katika jimbo lake Sekta ya Elimu inawekewa kipaumbele na hasa katika shule hizi chakavu, shule kongwe za msingi. Kuhusu swali lake la kwanza, ninaomba mimi na Mheshimiwa Mbunge tukae, tujadili na tupange ratiba inayotekelezeka, ili tuweze kuona tunafanyaje kuhusiana na kuzitembelea shule hizi kongwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika Serikali hii ya Awamu ya Sita, uwekezaji wa zaidi ya shilingi trilioni 5.1 umefanyika katika Sekta ya Elimu katika shule kongwe. Shule kongwe 832 zimeweza kufanyiwa ukarabati katika kipindi cha miaka minne na katika Jimbo lake la Chato jumla ya shilingi bilioni 1.53 zimeletwa, kwa ajili ya kuhakikisha zinakarabati shule kongwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hata fedha hizi milioni 890 ambazo zimetengwa kwa mwaka huu wa fedha zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha zinakarabati shule hizo kongwe, lakini nitumie nafasi hii kuendelea kutoa msisitizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kwamba anaendelea kuzifanyia tathmini shule hizi Kongwe 169 katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na kuziweka katika mpango na bajeti kwa ajili ya kuendelea kuzikarabati ili shule hizi ziweze kuwa katika hali nzuri na kuwanufaisha wanafunzi wetu.
Name
Suma Ikenda Fyandomo
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI aliuliza:- Je, lini Serikali itakarabati shule kongwe za msingi katika Jimbo la Chato?
Supplementary Question 2
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ninaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo imejenga shule nzuri sana, ambapo hata sasa hivi kule vijijini maharusi walio wengi wanakwenda kupigia picha.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Mbeya wanapenda kujua, shule za primary (shule za msingi) kongwe ambazo hazijakarabatiwa ni nyingi sana. Ziko Halmashauri ya Busokelo, Rungwe, Kyela, Mbarali, Chunya, Mbeya DC na Mbeya Vijijini. Je, ni lini sasa Serikali itakwenda kukarabati shule hizo kongwe za msingi Mkoani Mbeya?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Suma Fyandomo ambaye amekuwa akifanya ufuatiliaji mkubwa sana katika sekta ya elimu ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Mbeya wanapata elimu bora, kupelekewa fedha kwa ajili ya miundombinu, lakini kuboresha Sekta ya Elimu kwa ubora wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kutoa msisitizo kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita inafanya uwekezaji mkubwa sana kuhakikisha hata katika eneo la shule zetu hizi kongwe za msingi zinaweza kukarabatiwa na zinakuwa kaika hadhi nzuri kwa ajili ya wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kusema, shule kongwe 932 katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita tayari zimefikiwa na kukarabatiwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kuwa katika Mkoa wa Mbeya tutaendelea kuhakikisha kwamba tunafanya kazi ya kuzifikia shule hizo ambazo ni kongwe, kuzifanyia tathmini na kuziweka katika mpango na bajeti kwa ajili ya kuzifikia na kuzikarabati ziwe katika hali nzuri.
Name
Stella Simon Fiyao
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI aliuliza:- Je, lini Serikali itakarabati shule kongwe za msingi katika Jimbo la Chato?
Supplementary Question 3
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Changamoto iliyopo Chato ndiyo changamoto kubwa iliyopo ndani ya Wilaya ya Ileje kwenye Shule ya Msingi Iyuli, Nchala na Ilanga zilizopo Kata ya Mlale. Je, Serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba wanakarabati shule hizi kwa sababu ziko katika hali mbaya ambayo inahatarisha afya za watoto na walimu?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Stella Fiyao, kwa swali lake zuri kwa maslahi ya wananchi wake wa Mkoa wa Songwe. Ninaomba pia nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri katika Mkoa wa Songwe kuhakikisha wanafanya tathmini ya shule hizi za msingi ambazo ni kongwe na chakavu na waweze kuweka katika mipango na bajeti, tena bajeti zao wenye za halmashauri (own source) ili waweze kuzifikia shule hizi na waanze kuzikarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu nasi tutakuwa tunaendelea kuweka mkono na kuongeza nguvu ili mwisho wa siku miundombinu hii ya shule hizi iweze kuwa mizuri na ziweze kuwanufaisha watoto wetu.
Name
Minza Simon Mjika
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. MEDARD M. KALEMANI aliuliza:- Je, lini Serikali itakarabati shule kongwe za msingi katika Jimbo la Chato?
Supplementary Question 4
MHE. MINZA MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ninapenda kuishukuru sana Serikali yetu kwa ujenzi wa shule nyingi mpya katika Mkoa wa Simiyu. Swali langu ni hili, je, ni lini Serikali itakarabati Shule za Msingi Inalo, Itubilo na Mwagindu ambazo zimekuwa ni za muda mrefu?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze Mheshimiwa Minza kwa swali lake zuri kabisa kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia nitumie nafasi hii kuendelea kutoa msisitizo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuendelea kufanya wajibu wao wa msingi wa kuhakikisha wanawekeza katika kuendeleza miundombinu muhimu kabisa ya kutoa huduma ikiwemo katika Sekta ya Elimu. Kwa hiyo, watumie nafasi hiyo na wajibu wao wa msingi kufanya tathmini katika shule zote kongwe na kuweka katika mipango na bajeti za halmashauri zao (mapato ya ndani) ili waanze kuzifanyia ukarabati kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu itaendelea kufika maeneo mbalimbali kwa awamu ili kuongeza nguvu kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu ya shule hizi chakavu inaweza kuimarika na inawanufaisha vijana wetu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Minza kwamba Serikali itafika kwa ajili ya kuhakikisha shule ulizoziainisha katika Mkoa wa Simiyu ambazo ni chakavu zinaendelezwa, zinaboreshwa, zinafanyiwa ukarabati na zinakuwa katika hali nzuri.