Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Neema Gerald Mwandabila
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuhakikisha fursa zote za mikopo zinatolewa kwa uwiano unaozingatia usawa katika halmashauri zote?
Supplementary Question 1
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kufahamu wamechukua hatua gani kuhakikisha halmashauri zote zinakuwa na Maafisa Mikopo kwa kuwa wanatoa mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, nataka kufahamu kwa kuwa Wizara mbalimbali zimekuwa zinatoa mikopo kupitia halmashauri zetu na kumekuwa na halmashauri ambazo mpaka leo zinadaiwa kwa muda wa miaka mingi. Je, wao kama Wizara wamefanya hatua gani kuhakikisha halmashauri zinazodaiwa na Wizara zinalipa mikopo yao? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunafahamu katika halmashauri zetu tunatoa mikopo ya 10% kwa makundi maalum. Maafisa Maendeleo wa Halmashauri na maafisa wengine wa halmashauri ni viongozi ambao wanasimamia mikopo hii ya 10% na wanafanya kazi kama Maafisa Mikopo katika halmashauri hizi. Kazi inayofanyika ni kuendelea kuwajengea uwezo wa kifedha wa kusimamia na kuratibu vizuri shughuli za mikopo ya 10%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mpaka sasa tangu tumeanza mikopo hiyo tunakwenda vizuri na Serikali inaendelea kufanya uratibu na usimamizi wa karibu ili Maafisa Maendeleo ya Jamii na maafisa wengine wa halmashauri waweze kusimamia vizuri mikopo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kwamba, kweli kuna halmashauri zinakopeshwa na Wizara mbalimbali (Wizara ya Ardhi na Wizara nyingine). Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeendelea kusisitiza na kusimamia marejesho ya fedha hizo kwenye Wizara husika kutoka kwenye halmashauri na tutaendelea kufanya hivyo. Pia, marejesho yanatia moyo kwa sababu kwa kiasi kikubwa halmashauri zimeendelea kurejesha mikopo yao. Ahsante sana.
Name
Shally Josepha Raymond
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuhakikisha fursa zote za mikopo zinatolewa kwa uwiano unaozingatia usawa katika halmashauri zote?
Supplementary Question 2
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wengi katika kata zetu hawajanufaika na mikopo hii. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kufikisha hiyo huduma ya elimu kwa wanawake pamoja na hao Maafisa Mikopo? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maboresho ya mfumo wa mikopo ya 10%, tofauti na huko nyuma sasa tuna Kamati za Mikopo kuanzia ngazi za vijiji na mitaa. Moja ya kazi za Kamati zile za mikopo ni kuwatambua akinamama, vijana na watu wenye ulemavu wenye sifa za kupata mikopo hiyo ili kuwapa elimu na mbinu za ujazaji wa maombi yao kupitia mfumo wa kielektroniki ili waweze kupata mikopo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ngazi ya mikoa pia kuna kamati ambazo zinahusika na elimu, uhamasishaji na usimamizi kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka ngazi ya wilaya. Kwa hiyo, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, bado tunahitaji kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia, nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuwaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri kote nchini, Maafisa Mikopo (Maafisa Maendeleo) na Kamati zote zinazoratibu mikopo kwa ngazi ya vijiji, kata na halmashauri zihakikishe zinaendelea kuwaelimisha wananchi na kuwawezesha kujaza maombi ya mikopo hii ili wengi waweze kunufaika kama ilivyo dhamira ya Serikali.
Name
Grace Victor Tendega
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza:- Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuhakikisha fursa zote za mikopo zinatolewa kwa uwiano unaozingatia usawa katika halmashauri zote?
Supplementary Question 3
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kumekuwa na changamoto nyingi sana kwa akinamama, vijana na watu wenye ulemavu kupata hizo fedha. Kabla hawajapata hizo fedha kumekuwa na mtiririko mkubwa wa utoaji fedha kwa maana ya kwamba, kuandikiwa maandiko na hayo mambo mengine ambayo ni changamoto. Kwa nini Serikali isiweke utaratibu mzuri wa hawa akinamama, vijana na watu wenye ulemavu kupata fedha hizo kabla hawajatumia fedha nyingi?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tuna mikopo hii ya 10% na mahitaji ni makubwa zaidi kuliko upatikanaji wa fedha zenyewe. Pia, uzoefu unaonesha kwamba, vikundi vingi vinaomba mikopo hiyo kwa pamoja na halmashauri inatoa kwa awamu kutokana na upatikanaji wa fedha. Ndiyo maana kuna baadhi ya vikundi vinakuwa vimeomba mikopo hiyo vinasubiri kwa muda mrefu kidogo, kwa sababu baada ya kutoa ile mikopo kunakuwa kunahitajika muda wa kukusanya yale mapato mengine ili kuweza kuwakopesha. Kwa hiyo, ni moja ya sababu ambayo inachelewesha baadhi ya vikundi kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, sababu nyingine ni kweli kwamba kuna baadhi ya maafisa wetu hawasimamii kwa uthabiti na kuwawezesha vikundi kupata mikopo kwa wakati. Pia, Serikali ilishatoa maelekezo kwamba Maafisa Mikopo (Maafisa Maendeleo ya Jamii) kote nchini na Wakurugenzi wa Halmashauri zetu wahakikishe vikundi vyenye sifa vilivyokidhi vigezo na ambavyo tayari fedha ipo wapate mikopo mapema iwezekanavyo ili waendelee na shughuli zao badala ya kwenda na kurudi mara kwa mara. Ninakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved