Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Condester Michael Sichalwe
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Momba
Primary Question
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, Mitambo mingapi ya kutengeneza Gongo imesambazwa kwa wananchi wanaojishughulisha na uzalishaji wa pombe ya gongo?
Supplementary Question 1
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa nafasi. Hivi karibuni ndani ya nchi yetu tumeshuhudia kuna pombe nyingi sana ambazo ni kali zinaingizwa na zimeendelea kuwaharibu vijana na nguvu kazi ya Taifa, vijana wengi wanaendelea kuharibikiwa kwa kunywa hizo pombe kali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ikiwa hizo pombe kali zinaweza zikaingizwa zikiwa zimetengenezwa kutoka nchi nyingine, zikaingia nchini kwetu na vijana wetu wakaendelea kuharibikiwa. Serikali imeshindwaje kuwafundisha wananchi wetu wa chini ambako huko gongo inatengenezwa na inapendwa na mpaka hivi tunavyoongea inaendelea kutumika, tumeshindwaje kuboresha gongo yetu ambayo inategenezwa na mazao ambayo yako ndani ya nchi yetu, dhidi ya kuingiza pombe kali ambazo zinawaharibu vijana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa ambacho kinazidi kwenye gongo ni zile kemikali kati ya ethanol na methanol. Ni kweli kwa kuwatumia wataalam wetu kuwafuata Maprofesa pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao wameshafanya utafiti, tumeshindwa kuendelea na zoezi hili ili kwenda kuwafundisha wananchi walioko kule chini ambao wanatengeneza kinywaji hiki, ili waweze kupata pombe bora ya gongo mfano wa Konyagi ambayo inazalishwa hapa nchini kwetu, ili kutokuendelea kuifanya gongo ni kinywaji haramu na kuendelea kukimbizana na wananchi, ilhali wananchi kinywaji hiki wanakipenda na hivi tunavyoongea wanaendelea kunywa? Ahsante. (Kicheko)
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kutetea jinsi ambavyo pombe za kienyeji zinaweza zikachakatwa kwa viwango vinavyofaa kwa matumizi ya binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba siyo binadamu wote hutumia pombe, lakini kwa wale wanaotumia ni dhamira njema ya Serikali kwamba watumie pombe ambayo inafikia viwango visivyoweza kudhuru afya zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kusema hayo kwa suala lake la vijana wetu kuharibiwa na pombe zinazotoka nje na pamoja na kwamba ni pombe zinazokidhi vigezo, hili suala la ulevi wa vijana linasababishwa na mambo mbalimbali ambayo ni wajibu wa jamii na malezi kufanyika kuhakikisha kwamba vijana wetu wanatambua madhara ya pombe, kwa sababu hata gongo leo ikihalalishwa haina maana kwamba vijana watakunywa na watabakia wakiwa wastaarabu wasipoweza kunywa kwa kiasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, la wajibu wa taasisi zetu za kitafiti kuweza kuchakata na kutengeneza formula ya kutengeneza pombe salama kutokana na pombe za kienyeji, zoezi hili linaendelea. Nimejibu katika majibu ya swali la msingi kwamba, kuna taasisi za Serikali TBS, SIDO na CAMARTEC wameendelea kufanya utafiti na kutengeneza mitambo ambayo inatengeneza pombe kali za kienyeji, ambazo zinakidhi vigezo vinavyoruhusiwa sokoni na wajibu wa kila mnywaji ni kunywa kwa kiasi asiharibu afya yake, maana hakuna pombe ambayo itakuacha salama hata kama inafikia viwango, kama utakunywa bila ustaarabu.
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, Mitambo mingapi ya kutengeneza Gongo imesambazwa kwa wananchi wanaojishughulisha na uzalishaji wa pombe ya gongo?
Supplementary Question 2
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba, mabaki ya korosho yanatengeneza pombe inaitwa nipa, lakini ndio gongo hiyo hiyo. Mabaki ya miwa, molasisi, yanatengeneza pombe inatumika sana kwao huko, kwa akina Mheshimiwa Saashisha na maeneo mengine inaitwa piwa. Tanga wanatumia miwa muhogo pamoja na mafenesi kutengeneza pombe hizo hizo. Sumbawanga wanatumia mahindi na maeneo mengine. Sasa wakulima wana nia ya kutaka kujiongezea kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa endapo Serikali inasema haijahalalisha pombe ya gongo kwa sasa kwa sababu ya madhara hayo yaliyotajwa na sisi tumetoa mifano pombe zinazoingizwa kutoka nje zenye madhara yanayofanana. Shirika la Viwango TBS, miaka mitatu, minne, iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Mtwara alipeleka aina, sample, ya gongo kutoka vijiji mbalimbali vya Jimbo la Ndanda kwenda kupima na kuona uhalali wake. Walisema kwamba, haina madhara makubwa ya kibinadamu, lakini pia, alcohol percentage yake ilikuwa ni moderate, haifanani hata na pombe zinazoingizwa kutoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo Serikali haioni haja ya kununua mazao haya ya ziada kutoka kwa wakulima ambayo yangefaa kutengeneza alcohol, methanol pamoja na spirit, ili waweze kuyaangamiza na kufanya wananchi wasipike hizo gongo ambazo sasa haziruhusiwi? (Makofi)
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Answer
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpongeza ndugu yangu, Mheshimiwa Mwambe, kwa swali lake la msingi sana na ambalo amelipangilia kwa namna ambayo sehemu ya pili, ametoa ushauri kwamba, kwa nini Serikali isiangalie bidhaa ambayo inaweza ikatengeneza pombe isiyo na madhara na kuitengenezea viwango, ili iweze kutengenezwa na kuuzwa kibiashara kunufaisha jamii kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tunalichukua, kama Serikali, lakini hili la bidhaa zingine ambazo zinatengeneza pombe; ili uweze kutengeneza kitu chenye kiwango na salama kwa mwili wa binadamu ni lazima tuangalie ingredients zinazowekwa mule. Nadhani shida ya gongo, maana ndio lilikuwa swali la msingi ni kwamba, vitu vinavyotumika kutengeneza gongo hauwezi kulinganisha na vitu vinavyotumika kutengeneza pombe inayotokana na korosho, miwa au hata asali. Kwa ile jamii ya watu wanaokaa misituni ambao pia, wanatengeneza pombe ya asali na kuchanganya na mitishamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wajibu wa Serikali. Serikali imesikia ushauri wa Mheshimiwa kufanya utafiti zaidi na kugundua aina mbalimbali ya pombe za kienyeji ambazo zinafikia viwango vya usalama viweze kutengenezwa bila pingamizi na wananchi waweze kutumia kwa manufaa yao.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved