Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI K.n.y. MHE. SALIM MUSSA OMAR Aliuliza: - Je, ni upi mpango wa Serikali kuifanya NFRA kujitegemea hususan Idara ya Vyakula ili kuepuka uhaba wa chakula pindi nchi tegemezi zinapokumbwa na majanga?

Supplementary Question 1

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pamoja na majibu mazuri ninaomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, NFRA wamekuwa wakikopa pesa kwenye taasisi za kibenki na kimsingi tunapokopa pesa kwenye taasisi za kibenki kumekuwa na riba jambo ambalo limekuwa likiirudisha nyuma NFRA katika utekelezaji wake mahsusi.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia pesa NFRA ili iweze kujitegemea na kuachana na suala la ukopaji kwa sababu linawarudisha nyuma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali (b), kukodi maghala imekuwa ni jambo ambalo kwanza maghala yanakodiwa mengi, lakini pia ni pesa nyingi sana ambayo NFRA imekuwa ikitumia na mpango huu ni wa muda mrefu sasa, NFRA bado haijaanza kujenga.

Je, ni lini Serikali itaenda kujenga maghala kwa haraka katika maeneo ya Kigonsera, Liganga, Namtumbo pamoja na Mgazini? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi nimpongeze sana muuliza maswali ya nyongeza dada yangu Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma na hii imekuwa ni moja ya ajenda yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja awe na uhakika nalo kwamba moja NFRA Serikali kupitia bajeti tumekuwa tukitenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kununua chakula, hilo ni moja na la uhakika na la kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kukopa ni sehemu ya NFRA kujijengea uwezo wa kujiendesha kibiashara kwa sababu wakikopa bahati nzuri huwa wanarudisha zile fedha kwa sababu tumekuwa tukifanya biashara na nchi jirani za yale mazao ambayo tumekuwa tukiyanunua hapa nchini. Lakini Serikali haitaacha jitihada zake za kuongeza fedha ili kuhakikisha kwamba NFRA inapata uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba sasa tunakwenda kuwa na hati fungani ya usalama wa chakula ambayo sasa itaongeza mtaji mkubwa na kupunguza NFRA kwenda kukopa katika taasisi za kifedha. Kwa hiyo, hilo nimthibitishie tu tupo katika mpango kabambe kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kujenga maghala, huo ni mpango wa Serikali na mpango tulionao ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na maghala ya chakula katika halmashauri zote nchini na ndiyo maana unasema tunataka kutoka tani 700,000 za sasa kwenda tani milioni tatu. Sasa ili uweze kufikia ni lazima tupeleke maeneo yote ili hata kwenye yale maeneo wakati mwingine yakifikiwa na njaa iwe rahisi wale wananchi kukipata chakula katika maeneo ya karibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo ndiyo mipango ya Serikali ambayo tupo nayo sasa hivi, ahsante. (Makofi)