Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia Wahitimu waliosoma katika Vyuo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata usajili ili kuajiriwa nchini?

Supplementary Question 1

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na utaratibu uliopo, lakini bado tuna vijana wengi ambao wamesoma katika vyuo vya nje katika nchi hizi za Afrika Mashariki ambao pamoja na kufuata utaratibu huu, lakini wakifika katika Bodi za Kitaaluma ambazo ni muhimu wao wasajiliwe ili kuanza kazi katika nchi hii wanakataliwa usajili. Sasa, ni nini kauli ya Serikali juu ya changamoto wanazopata vijana hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kumekuwa na mifano hai ya hawa vijana ambao, baadhi au wengi wao, nimewapeleka hata kwa Mheshimiwa Waziri, anafahamu changamoto zao, ambao wametumia gharama kubwa na muda mrefu kujielimisha katika vyuo vya nchi mbalimbali ndani ya Afrika Mashariki, lakini na wao wamekataliwa usajili. Sasa hivi wako mtaani wamekata tamaa na wanaishi kama watu ambao hawakusoma kabisa kwa sababu, wamekataliwa kutambuliwa elimu walizopata. Sasa, ni nini kauli ya Serikali juu ya kuwasaidia vijana hawa na changamoto wanazopitia sasa hivi? Ninashukuru sana. (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, amekuwa akifuatilia jambo hili kwa karibu sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia taasisi yetu ya Elimu ya Juu (TCU) hivi sasa imetengeneza utaratibu wa kutoa Hati ya Ruhusa au Certificate of No Objection. Huu ni mkakati maalum wa Serikali wa kuhakikisha kwamba, mwanafunzi kabla hajaondoka kwenda nje kwa ajili ya kusoma anapata cheti hiki au certificate hii, ambayo itamwezesha kutambua au Serikali itawezesha kutambua uhalali wa chuo anachokwenda kusoma na uhalali wa kozi anayokwenda kusoma, ili anaporudi sasa Serikali iweze kutambua na kusajili kwa haraka sana taaluma aliyokwenda kusomea.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni hili ambalo amezungumza Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli, wapo vijana wetu ambao wamekwenda nje na wamerudi na imekuwa changamoto kidogo. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge tutofautishe hizi mamlaka za ithibati pamoja na zile mamlaka za kitaaluma. Kwa sasahivi tumetengeneza utaratibu, tunakaa na Bodi zetu zile za Kitaaluma, ili kuhakikisha kwamba, tunakwenda ku-harmonize mazingira yote yatakayojitokeza huko mbele na hawa vijana wetu tutakaa nao ili kuhakikisha kwamba, tunakwenda kuliweka jambo hili sawasawa.

Mheshimiwa Spika, ninaomba nitoe rai, wito na ushauri kwa wanafunzi; watu wote ambao wanataka kwenda nje ya nchi, basi waweze kufuata utaratibu wa kupata kwanza hii Certificate ya No Objection, ili wanapokwenda kusoma tujue wanakwenda kusoma kwenye chuo gani na wanakwenda kusoma taaluma gani. Lengo ni kuwalinda wao, lakini vilevile kuwalinda Watanzania dhidi ya taaluma ambazo watakuja kuwatumikia Watanzania wote ili zisiweze kuleta athari ndani ya nchi. Ninakushukuru sana.