Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Primary Question

MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: - Je, lini Serikali itasikiliza malalamiko ya watumishi dhidi ya Kikokotoo?

Supplementary Question 1

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, kwanza ninaishukuru Serikali kwa kuwa sikivu kupandisha hizi asilimia za malipo ya mkupuo kutoka 33% hadi kufika 40%. Swali la kwanza; kwa nini sasa, Serikali isikubali kurudi kwenye kiwango au gawio la zamani kutoka hizi 40% kwenda 50% ambapo kwa hali hii wafanyakazi wakistaafu wanaweza kupata mafao bora?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa kiwango cha sasa ni 40%. Je, huoni sasa ni wakati mzuri wa kuwapandishia hawa watumishi wanaostaafu kwenda 50% ya kiwango cha zamani, maana zamani walikuwa wanagawanya ile 500 kwa 80 kuliko ilivyo sasa?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, tunazidi kukubaliana na hoja ya Mheshimiwa Mbunge na ikumbukwe vizuri katika Bunge lako hili Tukufu kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 kulikuwa na hoja za Waheshimiwa Wabunge zilizoomba kufanya mabadiliko katika viwango vya pensheni. Kwa usikivu wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alimwelekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri Mkuu alituelekeza namna ya kuweza kufanyia kazi jambo hilo. Tulifanya marekebisho hayo kutoka kwa wale waliyokuwa wanalipwa 50% ya mkupuo kwa kipindi kile, kutoka 30% kwenda 40% lakini kwa wale waliokuwa wakilipwa 33% wamepandishiwa mpaka kufikia 35% kwa wale waliyokuwa wanalipwa 25% kabla ya mabadiliko ya Mfuko.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mabadiliko ya pensheni ni endelevu na tunazingatia sana kufanya tafiti, lakini pia kufanya actuarial evaluation ambazo zinaendelea na kwa mujibu wa sheria kila baada ya miaka mitatu tunafanya actuarial evaluation na kuangalia hali ya uchumi na ustahimilivu wa Mifuko na tunafanya mabadiliko hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba zingatio hilo limeendelea kuwepo na ndiyo maana hata mwaka huu mwezi Januari tumeongeza kiwango cha pensheni kutoka ile iliyokuwa inalipwa shilingi laki moja kama kiwango cha pensheni kwenda shilingi laki moja na nusu. Kwa hiyo, hayo ni mazingatio ambayo tumeendelea kuboresha na Mifuko yetu kwa kweli imeboreka na sasa changamoto za masuala ya pensheni ni chache sana na ni kwa specific cases. Ahsante. (Makofi)