Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Je, Serikali imechukua hatua gani kwa Vikundi hewa na udanganyifu kwenye mikopo ya asilimia 10 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu?
Supplementary Question 1
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, mikopo ya 10% ya wanawake inavyotolewa katika Halmashauri haina uwiano sawa, kwa sababu kuna Halmashauri zingine zina mapato madogo sana, kwa mfano chini ya shilingi bilioni tano lakini zingine zina mapato ya zaidi ya shilingi bilioni sitini kuendelea. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja sasa ya kutoa mikopo hii kwa msawazisho ili zile Halmashauri ambazo hazina mapato makubwa na zina uhitaji mkubwa wa mikopo hii waweze kuziongezea fedha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kumekuwepo na malalamiko sana kutoka kwenye kundi la wazee kwamba na wenyewe hawajafikiriwa kwenye mikopo hii, tunajua kwamba mikopo hii ni kwa ajili ya makundi maalum, sasa hivi inatolewa kwa vijana wanawake na watu wenye ulemavu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kuweza kuongeza kundi la wazee kwenye hii mikopo? Ahsante sana.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kutokana na sera ya ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa, kuna component muhimu sana ya D-by-D ambayo inaitwa ugatuzi wa fedha, fiscal decentralisation ambayo inataka Serikali zetu za Mitaa ziweze kukusanya mapato na kupanga matumizi.
Mheshimiwa Spika, ninaelewa hoja ya Mheshimiwa Mbunge, lakini kwa sababu, kila halmashauri inajitegemea kukusanya mapato kwa kalenda yake yenyewe na kuweza kupanga matumizi, kwa ajili ya watu wake. Basi hatuwezi, kama Serikali, kukusanya yale mapato na kuanza kuyagawa sawa kwenye halmashauri zote japokuwa inaweza ikaonekana kwamba, kuna baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zina mapato makubwa, lakini pia, tuzingatie maeneo hayo, nitatoa mfano.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, yenyewe jumla ya 10% ya Watanzania wote inatoka Jiji la Dar es Salaam. Kwa hiyo, unaweza ukaona pia, uhitaji unakuwa ni mkubwa.
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, mwaka jana kulikuwa na mapato ya ndani yametengwa, kwa ajili ya kutoa hii mikopo ya 10%, shilingi bilioni 13, lakini maombi yaliyojitokeza ni shilingi bilioni 19. Kwa hiyo, utaona kwamba, kuna uhitaji mkubwa pia, katika haya maeneo ambayo tunaona yana mapato makubwa. Kwa hiyo, Serikali inaelewa hoja yako na tutaendelea kuziwezesha Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa ili ziweze kujitengenezea mapato, kujitegemea na kupanga matumizi kusaidia haya makundi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na swali lako la pili, kuwajumuisha wazee katika hii 10% ya mapato ya ndani kwenye hii mikopo. Serikali ina vyanzo vingi vya kuwawezesha wananchi wake. Sasa 10% ya mapato ya ndani, hii mikopo inatoka mahususi, kwa ajili ya kundi la vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Bado kuna Mifuko na fursa nyingine ambazo zinawezesha makundi mengine, ikiwemo wazee. Mfano, kwenye Sheria yetu ya Manunuzi (PPRA) inataka kila Taasisi ya Serikali itenge 30% ya manunuzi yake, kwa ajili ya makundi maalum likiwemo kundi la wazee. Kwa nini?
Mheshimiwa Spika, sasa wazee wanaweza wakaunda kikundi, wakaajiri vijana, wakapata kazi. Wakaingia kwenye mfumo wa manunuzi, ule wa NeST, wakaomba kazi, wakapata na ikawa ni sehemu ya wao kuwa wamejipatia mtaji na fursa, kwa ajili ya kufanya shughuli za uzalishaji. Huku kwenye Mfuko huu wa 10% ya mapato ya ndani ya halmashauri tunataka tuwaone wahusika wao wenyewe na tunawakagua kwa shughuli zao wanazozifanya kwenye vikundi, tofauti na huu utaratibu mwingine ambao wazee wanaweza wakaajiri vijana wakawafanyia kazi, wakapata zabuni kupitia Mfumo wa NeST na wenyewe wakaweza kuwa wanajipatia kipato. (Makofi)
Name
Minza Simon Mjika
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:- Je, Serikali imechukua hatua gani kwa Vikundi hewa na udanganyifu kwenye mikopo ya asilimia 10 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu?
Supplementary Question 2
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Ninapenda kuuliza swali hili kwamba, kuna vikundi vingine ambavyo havirejeshi kabisa hizo fedha. Hizo fedha zipo katika mzunguko, ina maana zinapotemwa katika mzunguko vikundi vingine tena vinachukua. Je, Serikali inachukua hatua gani kwa watu wasiorejesha fedha hizo? (Makofi)
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha mfuko huu ambao unatokana na fedha za 10% za mapato ya ndani ya halmashauri ni kutengeneza mitaji, kwa ajili ya kuwezesha haya makundi. Mfuko huu ni mfuko ambao tunataka tuendelee kukopesha vikundi vingi zaidi (Mfuko wa Mzunguko). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kwamba, Mfuko huu unaendelea kudumu na kunufaisha makundi mengine mengi, basi tunachukua hatua mbalimbali ikiwemo hatua za kisheria. Tunafanya ufuatiliaji, kufuatilia wahusika wale ambao hawarudishi mikopo hii. Wale ambao wanajihusisha na udanganyifu tunawachukulia hatua za kisheria kwa kuazisha mashauri kupitia Mahakama. Watumishi wa umma ambao wanashiriki katika udanganyifu huo au wanakwepa kutimiza wajibu wao na kusababisha hasara hiyo ya upotevu wa fedha kupitia hizi zinazokopeshwa, basi na wenyewe taratibu za utumishi wa umma zinachukuliwa taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved