Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Michael Constantino Mwakamo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Primary Question
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga Shule chache za Kata kuwa za bweni kwa kuwa, matokeo ya wanafunzi si mazuri?
Supplementary Question 1
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kupeleka fedha za ujenzi wa mabweni ya kuongeza shule za kata kuwa kidato cha tano na cha sita. Swali langu la kwanza; kutokana na ufaulu ambao kwa kweli, siyo mzuri kwa kidato cha nne na hii inatokana na jiografia za kata, shule hizo kuwa mbali na maeneo ambayo watoto wanatoka. Je, Serikali haioni ni muda sahihi sasa kutoa ruhusa kwa wadau mbalimbali kujenga angalau hostel kwenye maeneo ya shule, ili watoto wa kidato cha kwanza mpaka cha nne waweze kukaa jirani?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa, lengo mama la ujenzi wa shule hizi ni kuongeza pia, idadi ya watoto wengi watakaofika elimu ya sekondari, lakini kutokana na matokeo ya kidato cha nne kutokuwa mazuri sana. Je, Serikali imeshafanya tafiti au haioni haja ya kufanya tafiti kubaini tatizo la watoto wa kidato cha nne kutokuwa na ufaulu mzuri, ili tuweze kuondoa tatizo hilo?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ujenzi wa hostel kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wanaosoma katika shule zetu za sekondari waweze kuwa karibu zaidi na shule na iweze kuwasaidia katika kupata utulivu wa masomo yao; ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, huo ndio utaratibu. Serikali tunatoa nafasi na tunashirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo wazazi pia, kujenga hostel katika shule kuanzia kidato cha kwanza na cha nne, kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi waweze kupata sehemu ambayo wataweza kufanya masomo yao kwa utulivu.
Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto ya umbali kwa wanafunzi wetu kufika shule; ndiyo maana kuna mradi mahususi kabisa wa kuendelea kuongeza miundombinu ya shule zetu hizi, Mradi unaofahamika kama SEQUIP, ambao unaboresha miundombinu ya shule zetu kwenye upande wa elimu ya sekondari. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kujenga Shule hizi za Kata ambazo ni za kutwa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kupunguza msongamano na kupunguza wanafunzi wetu kutembea umbali mrefu kufika katika shule ili waweze kupata utulivu na muda mzuri wa kuweza kujisomea masomo yao.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ufaulu; vilevile, Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kabisa za kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu nchini. Ndiyo maana utaona katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, uwekezaji zaidi ya shilingi trilioni 5.1 umefanyika katika Sekta ya Elimu. Yote hiyo, kwanza ni kuendelea kuboresha miundombinu ya shule pia, kuendelea kuajiri na kuwawezesha kimafunzo walimu wetu.
Mheshimiwa Spika, pia, kuboresha namna gani ya kutoa elimu, kwa maana ya kuongeza vifaa na vitendea kazi, kwa ajili ya walimu wetu, matumizi ya teknolojia za TEHAMA, kujenga maabara, ili kuendelea kuboresha elimu inayotolewa. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendela kufanya uwekezaji huo mkubwa ili kuendelea kuimarisha elimu inayotolewa kwa vijana wetu.
Name
Maimuna Salum Mtanda
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Primary Question
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga Shule chache za Kata kuwa za bweni kwa kuwa, matokeo ya wanafunzi si mazuri?
Supplementary Question 2
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, Shule ya Kata ya Mikumbi iliyopo Jimbo la Newala Vijijini tumeanzisha ujenzi wa bweni la wasichana ili kuwakinga na madhara kwa sababu, wanatoka maeneo ya mbali sana na shule ilipo. Je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi wa Jimbo la Newala Vijijini kuipatia fedha, ili bweni lile liweze kukamilika? Ahsante.
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu katika Sekta ya Elimu na hasa Elimu Msingi. Ninaomba nitumie nafasi hii kumtaarifu Mheshimiwa Maimuna Mtanda kwamba, Serikali itaunga mkono jitihada hizo za wananchi ambao wameanza kujenga miundombinu hiyo muhimu kabisa katika Sekta ya Elimu, ili iweze kukamilika na iweze kuwasaidia wananchi wetu, kwa maana ya watoto wao, kupata sehemu nzuri ya kupatia ellimu. (Makofi)
Name
Issa Ally Mchungahela
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Primary Question
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga Shule chache za Kata kuwa za bweni kwa kuwa, matokeo ya wanafunzi si mazuri?
Supplementary Question 3
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuuliza swali. Shule nyingi za vijijini zipo mbali sana na wananchi walipo, kwa maana ya wanafunzi wanakopatikana. Kwa nini Serikali isiamue kwamba, shule za kata zote za vijijini zijenge mabweni, kwa ajili ya shule hizo?
Name
Zainab Athuman Katimba
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa sasa shule zetu zinazotoa elimu ya kidato cha kwanza mpaka kidato cha nne ni shule za kutwa. Serikali kwa wakati huu inaweka kipaumbele zaidi katika kuhakikisha inajenga hizi shule za kata nyingi zaidi katika maeneo yenye uhitaji, ili kupunguza umbali wa wanafunzi kutembea kufika kwenye shule, pia, kupunguza msongamano na kuwapatia fursa vijana wetu kupata elimu.
Mheshimiwa Spika, shule ambazo zinajengewa mabweni ni shule za kidato cha tano na sita, ambazo ni shule za kitaifa, kwa maana zinachukua wanafunzi kutoka maeneo yote ya Tanzania. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kuna njia nyingine ambazo zinatumika, kwa mfano Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali, kwa ajili ya ujenzi wa hostel kwa kushirikiana na wazazi ili wanafunzi waweze kupata sehemu ya kuendelea kupata utulivu wanapokuwa wanapata masomo yao. Kipaumbele cha Serikali kwa wakati huu ni kujenga shule za kata maeneo ambayo bado yana uhitaji na hizi shule za kata ni shule za kutwa.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved