Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Primary Question

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO K.n.y. MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza:- Je, nini mpango wa Serikali kuendeleza Bandari ya Kyamkwikwi na kujenga barabara ya kuunganisha Bandari na Barabara Kuu?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wilaya ya Muleba ina visiwa vingi na tumekuwa tukitegemea Meli ya Clarious kutoa huduma ambayo si salama kwa kipindi hiki. Swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kutupatia vyombo salama na imara kwa ajili ya kuhudumia watu wetu wa Muleba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Mheshimiwa Waziri Mkuu alipotembelea Wilaya ya Muleba mwaka juzi alitoa maelekezo TPA kujenga bandari ndogo ya Katembe Magarini. Je, lini TPA ina mpango wa kutekeleza hilo agizo? Ninashukuru sana.

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Kikoyo pamoja na Mheshimiwa Mwijage kwa sababu wamekuwa ni Waheshimiwa wanaofuatilia kwa ukaribu sana maboresho makubwa sana ya kibandari katika ziwa letu, Ziwa Victoria ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kumfahamisha Mheshimiwa Kikoyo kwamba Serikali imefanya mambo mengi katika Ziwa Victoria ili kuimarisha usalama na kuhakikisha kwamba usafiri unaokuwepo unakuwa ni wa uhakika. Kwa awali ninapenda kumhakikishia na kumweleza kwamba tayari Serikali imefanya maboresho ya kujenga bandari tatu ikiwemo Bandari ya North Mwanza, Bandari ya Kemondo na Bandari ya Bukoba. Bandari ya Kemondo imekamilika North Mwanza pamoja na Bukoba zinaendelea. Hiyo ni hatua ya kwanza ya kuhakikisha kwamba usafiri kwenye ziwa hilo unakuwa ni wa uhakika na wenye usalama.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali imechukua jukumu kubwa ya kujenga vituo mbalimbali vya uokoaji katika Ziwa Victoria. Vingine vimejengwa Sengerema, vingine Victoria pale, kwa maana ya Mwanza na Geita na maeneo mengine. Aidha, tayari Serikali imetenga fedha za kutosha na tupo kwenye hatua za mwisho wa kujenga meli kubwa MV Mwanza Hapa Kazi Tu ambayo tunategemea itakamilika siyo muda mrefu kuanzia sasa. Itakapokamilika hiyo itakuwa imaimarisha usafiri wa uhakika kati ya Mwanza, Bukoba kwa maana ya Mkoa wa Kagera, pamoja na maeneo kama Port Belly na maeneo mengine ambayo yanazunguka kwenye ziwa hilo.

Mheshimiwa Spika, ukija kwenye hoja yake ya visiwa vile vya kawaida alivyovisema ikiwa ni pamoja na vilivyopo katika eneo la Muleba, tayari Serikali inatambua umuhimu wa meli hiyo kuwepo, ambayo ni ya Serengeti. Tumekwishaanza utaratibu wa kuainisha mahitaji, kwa sababu meli hii ilisimama 2019 lengo letu tutazame mahitaji ni kiasi gani tuikarabati na ianze kufanya kazi ambayo itakwenda kwenye visiwa vidogovidogo ikiwa ni pamoja na ambavyo Mheshimiwa Kikoyo amevisema.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo tayari meli ya mizigo ya ML Wimbi ambayo ambayo yeye anaifahamu ambayo inabeba mizigo midogomidogo, ikiwemo bidhaa za dukani pamoja na dagaa na vitu vingine vingine iko mwishoni ikikamilika itakwenda pia kwenye eneo hilo la Muleba kwa ajili ya kuhakikisha tunawasaidia wananchi wetu hao.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili amezungumzia kuhusu agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wizara yetu inatekeleza maelekezo ya viongozi wakuu wote kwa msisitizo na uzito unaostahili, ikiwa ni pamoja na maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, na kwa kuanzia tayari tumeshaanza mchakato kwa ajili ya kuhakikisha tunatazama namna ya kuweka kwenye bajeti ijayo. Hata hivyo ikumbukwe kwamba nchi hii ina bandari 693, uwezo wa Serikali kuanza kuzijenga zote kwa wakati mmoja hauwezekani. Tunaanza kidogo na tumeshaanza kurasimisha mpaka mwaka 2021 tulikuwa tumerasimisha bandari 80 na Mheshimiwa Dkt. Samia suluhu Hassan amekwenda kwa kasi kubwa zaidi zimeongezeka zaidi ya bandari 50. Hivyo nimuombe awe na subira tutajitahidi hatua kwa hatua na kwake tutamfikia tena. Ahsante.

Name

Kavejuru Eliadory Felix

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Primary Question

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO K.n.y. MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza:- Je, nini mpango wa Serikali kuendeleza Bandari ya Kyamkwikwi na kujenga barabara ya kuunganisha Bandari na Barabara Kuu?

Supplementary Question 2

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, lini ujenzi wa Bandari ya nchi Kavu ya Gungu Mjini Kigoma utaanza kwa sababu Serikali imekuwa ikiahidi kwa muda mrefu sasa?

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu kwa kifupi.

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, samahani nilikuwa sijasikia bandari gani?

SPIKA: Bandari kavu.

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, bandari ya nchi kavu Gungu Mjini Kigoma.

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, Serikali kwa Kigoma inafanya mpango wa kujenga bandari kavu iliyopo Kigoma mjini ili kuunganisha kati ya nchi yetu na nchi jirani. Hii aliyoitaja ninaomba nichukue na tuanze kulifanyia kazi kulingana na mahitaji sambamba na uwepo wa fedha.

SPIKA: Mheshimiwa Kavejuru hiyo uliyoitaja iko jimbo gani?

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, iko Jimbo la Kigoma Mjini na tayari Serikali ilikwishaweka fensi kwa muda mrefu na ilipa fidia wananchi waliokuwa wanaishi pale wakaondoka kabisa kwa muda mrefu, zaidi ya miaka 10 sasa; na pana fensi. Sasa kwa muda mrefu wananchi wa Kigoma wamekuwa wakisubiri ujenzi wa bandari hiyo ya nchi kavu mpaka sasa hivi hakuna kitu kinachoendelea.

SPIKA: Haya ahsante sana. Sasa umepata ufafanuzi Mheshimiwa Naibu Waziri ni hiyohiyo ya mjini uliyoijibia, ndiyo hiyohiyo na yeye anayoiulizia ahsante sana.