Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi ya Kisasa – Makete kupitia miradi ya kimkakati ya Serikali?
Supplementary Question 1
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninashukuru kwa majibu ya Serikali, yanaleta matumaini na ni majibu ambayo wananchi wa Makete wanayo matumaini nayo, lakini nina swali moja kubwa la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninampongeza Mkuu wangu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi, Mkuu wangu Mheshimiwa Kissa Gwakisa Kasongwa na Mkurugenzi Jerry Mwaga kwa sababu wameanza kulifanyia kazi suala hili ambalo unalisema na kutenga shilingi milioni 100. Pili, ujenzi wa barabara kutoka Njombe kuelekea Makete na kutoka Makete kuelekea Mbeya ndiyo unaotufanya tuwe na uhitaji wa stendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni moja tu, ni upi mkakati wa Serikali kwamba, Halmashauri ya Makete mapato yake bado ni madogo yako chini na imetenga eneo la ekari 24.5 kwa ajili ya kujenga stendi ili barabara ikikamilika ikutane na stendi imekamilika? Je, Serikali haiko tayari kutupatia fedha kwa mkopo au kwa namna nyingine ili halmashauri yetu iweze kujenga stendi hiyo? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli kwamba kuna ujenzi wa barabara ya lami ambayo tayari imekamilika, kutoka Njombe mpaka Makete, lakini kuna mpango wa Serikali kuendelea na ujenzi wa barabara kutoka Makete kwenda Mbeya, barabara hizi zitaongeza sana idadi ya magari yanayoingia katika Halmashauri ya Makete hivyo kulazimika kuwa na stendi kubwa na ya kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Sanga kwamba, Serikali hii inatambua uhitaji wa stendi katika Halmashauri ya Makete na ndiyo maana ilimwelekeza Mkurugenzi kutenga eneo na ameshatenga eneo la ekari 24.5. Ninakuhakikishia tu kwamba tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo kwa awamu, kwa kushirikiana na mapato ya ndani pia Serikali Kuu ili tuhakikishe kwamba huduma za usafiri zinaimarishwa zaidi katika Wilaya ya Makete. Ahsante. (Makofi)
Name
Yustina Arcadius Rahhi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi ya Kisasa – Makete kupitia miradi ya kimkakati ya Serikali?
Supplementary Question 2
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa stendi katika Mji wa Mbulu kupitia Mradi wa TACTIC?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa TACTIC unaendelea kutekelezwa katika miji 45 ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Tayari tuko awamu ya kwanza na ya pili na tunatarajia kuanza awamu ya tatu wakati wowote. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa sababu stendi hiyo iko kwenye mpango wa TACTIC, tutahakikisha tunapoanza utekelezaji wa tier hiyo, tunaanza na ujenzi pia wa barabara pamoja na stendi ili Mji huo uwe na huduma nzuri zaidi za usafiri. Ahsante. (Makofi)
Name
Eng. Ezra John Chiwelesa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi ya Kisasa – Makete kupitia miradi ya kimkakati ya Serikali?
Supplementary Question 3
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwaka jana tarehe 6 Agosti, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi alifanya ziara katika Mkoa wa Kagera, Tarehe 07 akawa Biharamulo na ziara hiyo aliambatana na Waziri wa TAMISEMI ambaye aliwakilishwa na Naibu Waziri. Moja ya maombi ya watu wa Biharamulo ilikuwa ni ujenzi wa stendi ya kisasa na alitoa maelekezo ambapo majibu tuliyoyapata ni kwamba ilibidi andiko lirekebishwe liweze kurudishwa upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, andiko limerekebishwa na tayari liko Wizarani, TAMISEMI. Sasa, ni lini ujenzi wa stendi ya kisasa Wilayani Biharamulo utaanza? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumepokea andiko la kimkakati la Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo kwa ajili ya ujenzi wa stendi, na tunafahamu kuna uhitaji mkubwa wa stendi. Kama yalivyo maelekezo ya Katibu Mkuu wa Chama lakini ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunajenga stendi ya kisasa pale Biharamulo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge Engineer Chiwelesa kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari tumepokea andiko hilo, tunafanya mawasiliano na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupata fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo, angalau kwa awamu, lakini tunahakikisha kwamba tutaanza utekelezaji mapema iwezekanavyo. Ahsante. (Makofi)
Name
Minza Simon Mjika
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza:- Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi ya Kisasa – Makete kupitia miradi ya kimkakati ya Serikali?
Supplementary Question 4
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wilaya ya Meatu imeshaandaa eneo kwa ajili ya stendi mpya. Je, ni lini sasa Serikali itajenga stendi mpya katika Wilaya hiyo ya Meatu? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu uhitaji wa stendi ya mabasi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, lakini kama ambavyo uko uhitaji katika halmashauri mbalimbali, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza kwa Waheshimiwa Wabunge wote na ninatoa msisitizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote kote nchini ambao wana maeneo na uhitaji wa ujenzi wa stendi kwa ajili ya huduma za usafiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza waainishe maeneo ya ujenzi wa stendi hizo, lakini pili waanze kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hizo na wale ambao watakuwa hawana uwezo wa ujenzi wa stendi hizo walete maombi hayo kwa ajili ya ujenzi kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutafuatilia hilo ombi na tuone namna ambavyo tutaanza ujenzi katika Halmashauri ya Meatu. Ahsante.