Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. DOROTHY G. KILAVE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuyatambua maeneo yote yanayoathiriwa na maafa na kuweka mkakati wa ziada?

Supplementary Question 1

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali; je, Jimboni kwetu Temeke hivi ninavyoongea kuna maafa, kuna sehemu ambayo ipo ndani ya Kata ya Kilakala sehemu inaitwa Bongotonyo. Tumeshaisemea sana ndani ya Serikali; je, mpo tayari sasa kuangalia au ipo ni mojawapo kati ya haya majimbo ambayo mmesema yamewekwa 36? Mpo tayari kwenda kuiangalia na je, mnatusaidiaje kwa kipindi hiki? Maana yake ni janga kubwa kwetu ndani ya Temeke pamoja na Tandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali la pili; upi mkakati wa Serikali wa kuongeza au kuweka fedha za ziada ndani ya mifuko hii ya maafa kabla Serikali Kuu haijaja kufanya kazi hiyo? Kwa sababu ndani ya majimbo yetu kunakuwa na maafa yanatokea, lakini fedha zinakuwa ni kidogo sana.

Je, ni upi mkakati wa Serikali kuweka fedha kidogo ndani ya majimbo yetu au wilaya zetu, ili sasa inapotokea maafa majimboni kwetu, yaanze kufanyiwa kazi kabla ya Serikali Kuu? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge Dorothy Kilave kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika Jimbo lake na nieleze tu wazi na nikiri mbele ya Bunge lako siyo tu hayo maeneo anayoyataja, kuna maeneo mengine pia kwenye kata yake na ninakumbuka kwa mwaka wa fedha 2021/2022 alizungumza kwenye Kata za Kilakala, Miburani, Keko, Chamazi na maeneo mengine Mianzini na Kibondemaji, napo pia wakati wa mvua kumekuwa kukiwa na changamoto kama hizo za mafuriko ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada za Serikali kwa kweli zimekuwa zikichukuliwa ikiwa ni pamoja na yeye katika ushiriki wake. Utakumbuka kwenye baadhi ya maeneo Serikali ilianza kurejesha miundombinu ya barabara, lakini pia hatua nyingine ni urejeshaji wa mifereji pamoja na hata pale kwenye maeneo ambayo yalilazimu kutengeneza shule, ili wanafunzi wasipate changamoto kwenye yale maeneo, wewe Mheshimiwa Mbunge ulikuwa sehemu ya kuhakikisha wananchi hawa huduma zinarejea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata kwenye maeneo ambayo yalihitaji vivuko, Mheshimiwa Mbunge utakumbuka kwamba tuliweka, ni moja ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba tunakabiliana na maafa hasa ya mafuriko yanapotokea kwenye maeneo hayo ya wananchi, ili kurejesha huduma kuweza kuendelea kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hatua ya pili ameuliza swali la pili kuhusiana na mfuko kwamba uwepo mfuko. Sheria yetu hii ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 haikuanzia sera yenyewe lakini sheria ya mwaka 2022, Sera ya 2004, sheria ya mwaka 2022 inaeleza kinagaubaga kunakuwa na Kamati za Menejimenti ya Maafa kwenye maeneo yetu na zinaanzia ngazi ya kijiji inaenda ngazi ya kata, wilaya mpaka mkoa. Kwenye haya maeneo kutokana na mapato wanayoyapata na mipango ya halmashauri ambao ndio watekelezaji wa majukumu haya na Wakuu wa Wilaya wakiwa wasimamizi wa ngazi ya Mkoa na Wilaya, inapotokea kuna changamoto yoyote inaenda kwenye bajeti zao ndani ya halmashauri na hatua ya pili ni bajeti za kimikoa kwa ajili ya maafa, lakini inapotokea kwamba jambo hili limeenda kwenye ngazi ya kuwa na maafa makubwa ya juu zaidi kuna utaratibu pia wa kutoa taarifa kwenye Kamati ya Maafa ya Taifa. Huko pia tunao mfuko ambao upo kwa mujibu wa sheria wa kushughulika na masuala ya maafa.

Kwa hiyo, ikitokea hali kama hiyo ni taarifa tu na mara nyingi Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa iki-respond sana kwa haraka ikiwemo kwenye jimbo lako pia hata pale Manyara utakumbuka watu wamejengewa nyumba na wanaishi vizuri. Kwa hiyo, hali hii Mheshimiwa Mbunge inapotokea Serikali ipo pamoja na wewe katika ngazi zote, ahsante. (Makofi)