Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:- Je, Serikali inatambua biashara ya mtandao na Makampuni mangapi yamejisajili na mapato kiasi gani yamepatikana kwenye biashara hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, ninaomba sasa niulize maswali yangu mawili. Swali la kwanza; je, Serikali ina mkakati gani katika kuzuia udanganyifu na utapeli mkubwa unaofanywa katika biashara hizi za mitandaoni kwa sababu, kuna watu wengi sana wamelizwa, kwa ajili ya hii biashara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; je, Serikali inadhibiti vipi wanaouza bidhaa kwenye social media bila leseni kwa sababu, pia, kuna utapeli mkubwa sana unafanyika ili kuweza kukusanya mapato? (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kwa ufuatiliaji kwenye biashara na mahususi biashara mtandaoni. Ni kweli bado tuna changamoto nyingi na ndiyo maana nimesema Serikali imekuja na mkakati huo madhubuti na huu mkakati ni utekelezaji wa Sera ya Biashara ya Taifa ya Mwaka 2003, Toleo la Mwaka 2023, ambalo Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Dkt. Selemani Saidi Jafo, alipitisha. Katika kutekeleza hilo tumeweka mkakati huu mahususi ambao umelenga kuboresha biashara mtandaoni kwa sababu, tumeona changamoto hiyo iliyopo katika biashara mtandaoni kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, hiyo ni moja ya mkakati, lakini mikakati mingine ni Serikali kupitia Wizara mbalimbali, kwa mfano, Wizara ya Fedha tayari wana kitengo mahususi ambacho chenyewe kinasimamia biashara mtandaoni. Ndio maana utakuta rekodi zetu za mapato yameongezeka kwa sababu, tayari tuna-track kuhakikisha biashara zinazofanyika mtandaoni zinalipia kodi, lakini pia mapato ya Serikali hayapotei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, tayari kuna sheria mbalimbali ambazo zote hizi zinalenga kudhibiti au kuboresha biashara mtandao. Kwa mfano, wana Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, lakini pia, wana Sheria ya Miamala ya Kieletroniki ya mwaka 2015 na pia, kuna ile Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022. Yote haya yanalenga kuhakikisha tunapunguza au tunaboresha biashara mtandao ili iweze kuwa na manufaa kwa Watanzania, lakini pia kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili ni kweli kuna changamoto ya biashara ya kuuza bidhaa mtandaoni bila ya kuwa na kampuni. Kwa mfano, mtu anapiga picha bidhaa ya mtu kwenye duka halafu anarusha mtandaoni anatafuta wateja. Sasa mtu kama hujui, ameweka na namba ile ambayo bado ukituma hela mzigo hutapata, lakini pia na fedha yako itakuwa imetapeliwa. Sasa moja ya vitu ambavyo tumefanya, kama Serikali, tunawasaidia vijana, kwa mfano, sasa hivi tumewaambia kuna vijana wa Tanzania wamebuni mfumo mzuri ambao wenyewe unasaidia kuunganisha kati ya mteja kwa maana ya mnunuzi na mteja muuzaji kwamba, wameanzisha kampuni moja inaitwa fortune technology company na wana App moja inaitwa Swift PAC, ambayo yenyewe wanashirikiana na shirika la posta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba ukinunua fedha zako zitakaa pale kwanza na ukithibitisha kwamba, umepata mzigo ndio wale wana-release ile fedha kumpelekea yule ambaye anauza. Kwa hiyo, hizi ni hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na Serikali ili kuhakikisha tuna boresha biashara mtandao kwa sababu, hatuwezi kukwepa. Sasahivi biashara mtandao ndio kila kitu, lakini lazima tupunguze changamoto au athari hasi za biashara mtandao. Ninakushukuru sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved