Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete Tabora?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, Mkoa wa Tabora ni mkoa wa tatu kwa wingi wa watu kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022. Kipaumbele cha Mheshimiwa Rais katika masuala ya afya ni afya ya mama na kupunguza vifo vya mama mjamzito na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; mpaka leo Tabora Hospitali ya Mkoa tunaambiwa inajengwa kwa awamu kuanzia mwaka 2020 mpaka sasa jengo lile bado halijakamilika. Serikali ituambie ile ni Hospitali ya Mkoa ama ni kitu gani? Kwa sababu mpaka leo hakuna uwezekano wa kumalizika kwa jengo lile, bado bilioni mbili zinahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; pamoja na changamoto ya majengo likiwemo na jengo hilo la mama na mtoto na ndiyo maana nikashauri hospitali ile iwekwe iwe ya Wilaya na Hospitali ya Mkoa ijengwe nyingine. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaboresha huduma za afya za Mkoa wa Tabora, kwa sababu ni mkoa ambao una watu wengi na wanahitaji huduma za afya badala ya kuwapa rufaa kila siku kwenda Bugando na kuja Hospitali ya Benjamini wakati pale tunaambiwa tuna Hospitali ya Mkoa? Ninakushukuru. (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa hamasa aliyokuwa nayo nzuri ya kuhakikisha Hospitali yao ya Mkoa ya Tabora inafanyiwa kazi vizuri. Niseme tu kwa kweli anafanya kazi vizuri sana Mheshimiwa Mbunge akishirikiana na Mheshimiwa Mwakasaka kwa ajili ya kutetea hospitali hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe Mheshimiwa Mbunge wasiwasi, kwanza alimwona jana Waziri wa Afya, alikwenda kwenye hospitali hiyo na alikwenda kwa msisitizo wa kuhakikisha kwamba hospitali hiyo sasa haya anayoyasema yanaenda kutatuliwa mara moja kabla ya kufika Februari, 2026. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe tu wasiwasi, leo fedha ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiingiza kwenye Sekta ya Afya ni nyingi sana kiasi kwamba sio tu zimetatua matatizo ya afya kwa Tanzania yetu, imebubujika imekwenda mpaka kwenye mataifa yanayotuzunguka, ndiyo maana unasikia leo watu wanatoka nchi mbalimbali wanakuja kutibiwa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi, tunaanza moja moja, bora wao waliokuwa na hospitali hiyo ya mkoa ya zamani, wenzao walikuwa hawana hospitali ya mkoa kabisa na leo wanayo. Sasa usiogope, kila kitu ambacho mnataka kwenye Mkoa wa Tabora, kwenye eneo la afya Mheshimiwa Rais wetu ameshajipanga kwa ajili ya kuhakikisha hayo mambo yanatekelezeka. (Makofi)

Name

Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Primary Question

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete Tabora?

Supplementary Question 2

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Bado kuna upungufu mkubwa wa madaktari katika Hospitali yetu ya Kitete na Serikali ilikuwa imetuahidi itatuongezea Madaktari, mpaka sasa hivi imeshatuongezea madaktari wangapi bigwa ambao tulikuwa na upungufu nao? (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ushahidi unaoonesha jinsi ambavyo Mheshimiwa Hawa Mwaifunga na Mwakasaka wanashirikiana kwa pamoja kuhakikisha Hospitali ya Kitete inakuwa imekaa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niseme tu, Mheshimiwa Mwakasaka jana alimwona Mheshimiwa Waziri amekwenda pale na anakumbuka siyo muda mrefu mimi na yeye tulishirikiana tukaenda kwenye hospitali yenu na hili ni kwa sababu kumekuwa kunapelekwa wataalam mbalimbali kwenye hospitali yetu. Toka niende pale mpaka sasa sina namba kamili, lakini baada ya hapa tuje tukae na yeye ili tuweze kuangalia namba kamili nimwambie, nisije nikamwambia namba isiyo sahihi. (Makofi)