Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Joseph Michael Mkundi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ukerewe
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: - Je, zipi athari za kisayansi zinazosababishwa na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba?
Supplementary Question 1
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nishukuru kwa majibu ya Serikali, lakini katika majibu ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza wazi kwamba ufugaji huu usipofanyika kwa kufuata kanuni unaweza kuwa na athari kwenye mazingira, lakini na upotevu wa bioanuai za asili na hili linaweza kupelekea athari na upotevu wa samaki wa asili.
Nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba kunakuwa na ufuatiliaji na usimamizi wa karibu ili kuepusha athari hizi zinazoweza kusababisha kupoteza samaki wa asili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili; kufuatia uwekezaji wa ufugaji wa vizimba kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wafugaji kukosa soko la samaki kwa sababu uzalishaji umekuwa mkubwa na mojawapo ni moja ya kikundi kwenye jimbo langu, Jimbo la Ukerewe, Kikundi cha Bagayo, wamevuna karibu tani 12 lakini wamekosa soko. Nini sasa mkakati wa Serikali kuwasaidia vikundi kama hivi ili iweze kuwaongezea tija? Nashukuru.
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba tunalinda mazalia ya samaki asili ni pamoja na kutoruhusu vizimba kuwekwa mahala popote na ndio maana tumesema kwamba kabla ya kuweka vizimba ni lazima Serikali kupitia TAFIRI ijiridhishe ni eneo gani linaweza kuwekewa vizimba na eneo gani haliwezi kuwekewa vizimba, sio tu kiholela kwamba mtu anachukua vizimba anapeleka popote kwenda kuweka vizimba, hiyo hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana watu wetu, wataalamu wetu wanajua maeneo yote katika Ziwa Tanganyika, katika Ziwa Nyasa tumeshakamilisha ufuatiliaji wa kujua wapi tunaweza kuweka vizimba, Ziwa Victoria pia tunafahamu. Kwa hiyo tunapokwenda kuweka vile vizimba ni maeneo kwanza ambayo sio ya mazalia ya samaki asilia, tunakwepa mazalia asilia yaendelee kujizalia kadri inavyowezekana. Kwa hiyo, vizimba hivi vevyewe vinakwenda kuwekwa katika maeneo ambayo hakuna mazalia kabisa ya samaki asilia na ndio maana uzalishaji unaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la pili la kukosa soko la Samaki, nimuombe Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki tukutane tuwaunganishe wafanyabiashara wake, wafugaji wake wa Samaki na wafanyabiashara wakubwa wa samaki, kwa sababu taarifa tulizonazo ni kwamba tuna mahitaji makubwa ya Samaki kuliko uzalishaji wa samaki tulionao. Sasa nitashangaa sana samaki hawa kukosa soko wakati bado nchi inahitaji samaki pengine labda wafugaji wetu wamekosa network ya kujua wapi wanaweza wakauza hawa samaki. Serikali ipo tayari kumuunganisha Mheshimiwa Mbunge na wafanyabiashara wakubwa wa samaki ili tuone namna ya kuwasaidia wavuvi wetu, ahsante.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: - Je, zipi athari za kisayansi zinazosababishwa na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba?
Supplementary Question 2
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Waziri, mbali na kwamba Serikali mnahamasisha ufugaji wa samaki kupitia vizimba, lakini vilevile mliwahamasisha wafugaji kujiunga kwenye vikundi ili muweze kuwapatia vifaa vya kisasa waweze kuvua kisasa. Sasa unajua wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini ni wavuvi kweli kweli na wamejiunga kwenye vikundi, ni lini sasa Serikali mtawawezesha vifaa vya kisasa ikiwepo na maboti waweze kuvua kisasa?
Name
Alexander Pastory Mnyeti
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Answer
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwanza nimpongeze sana dada yangu Ester Bulaya, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kufuatilia maendeleo ya watu wake na tumeshapokea orodha ya vikundi kutoka katika Jimbo la Bunda Mjini, Bunda Vijijini lakini pia Mwibara ambapo Mheshimiwa Mbunge ameleta orodha ya majina ya vikundi vyake. Tumeshatoa vizimba na boti na nyenzo za kuvulia samaki kwa vikundi mbalimbali katika eneo la Ziwa Victoria; awamu ya kwanza tulitoa vizimba vya kutosha, sasa tupo kwenye hatua ya pili ya kutoa vizimba na tumeshaanzia Geita, tupo Mwanza sasa tunakuja Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mbunge kwamba baada ya wiki moja au mbili tunakwenda kugawa vizimba vingi sana katika eneo la Bunda, Tarime kwa Esther Matiko, tutakwenda kugawa vizimba na nyenzo za kuvulia ili kuhakikisha kwamba wavuvi wetu wa samaki wanakwenda kupata uzalishaji mkubwa wa samaki katika eneo hilo, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved