Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. EDWIN E. SWALLE K.n.y. MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: - Je, Serikali haioni haja ya kuanzisha eneo mahsusi la viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya misitu?

Supplementary Question 1

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa wawekezaji wengi kwenye bidhaa za misitu hawana mpango wowote endelevu wa kuongeza thamani kwenye bidhaa za misitu na kwa kuwa Wizara hii ya Viwanda kazi yake ni uratibu wa viwanda hapa nchini, je, haioni haja sasa ya kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha eneo mahsusi au one stop centre mkoani Njombe kwa ajili ya viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya misitu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sisi kule mkoani Njombe ikiwemo kwenye Jimbo la Mheshimiwa Deo Mwanyika pale Njombe Mjini na Jimbo la Lupembe, wapo wawekezaji wanaovuna bidhaa za misitu, lakini wanawalipa wakulima bei kidogo sana kwenye magogo na kwenye mbao. Ni lini Serikali itaweka bei elekezi kwenye bidhaa za misitu nchini? (Makofi)

Name

Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu wa kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na misitu nikubaliane na ushauri wako, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine tumelibeba hili kwa ajili ya kwenda kulichakata na kuona uwezekano wa kukaa pamoja ili kuweka thamani ya mazao haya na wakulima wapate faida inayotakikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bei, ni kweli kabisa kwamba bei ya mbao inawezekana haijatolewa maelekezo rasmi juu ya bei elekezi na hii inatokana na biashara yenyewe ilivyo kwa maana ya viwango vya uzalishaji na ubora wa mazao yanayotokana na hili jambo.

Mheshimiwa Swalle, tumelichukua hili jambo na Wizara itakutana na ninyi Waheshimiwa Wabunge mnaotoka kwenye eneo hili ili muweze kuyaweka vizuri masuala ambayo yanahusiana na bei ambazo kwa kweli mngependa zipewe maelekezo kutoa faida kwa wazalishaji. (Makofi)