Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara za lami katika Mji Mdogo wa Karatu?

Supplementary Question 1

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ya ujenzi wa barabara ambayo inaendelea katika Mji wa Karatu. Kwa kuwa Mji wa Karatu ni mji unaokua kwa kasi na ni mji muhimu kwa maana ya eneo la kiutalii.

Swali la kwanza; je, Serikali haioni haja sasa ya kupanua wigo wa ujenzi wa barabara katika maeneo mengine ya pembezoni katika Mji wa Karatu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna baadhi ya kata ambazo zinakuwa kwa kasi zikiwemo Kata ya Mang’ola, Barai, Endambashi, Mbulumbulu na Rotia. Je, Serikali haioni ni muhimu angalau baadhi ya barabara katika maeneo hayo na yenyewe ikajengwa kwa kiwango cha lami?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kumpa taarifa Mheshimiwa Cecilia Paresso kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati ya kuendelea kuongeza mtandao, lakini kuboresha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya ambazo zinasimamiwa na TARURA ili ziweze kuwa katika hali nzuri ifikie mtandao mrefu zaidi na wananchi waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi vizuri zaidi, lakini wananchi pia waweze kufikia huduma za msingi kabisa za kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niendelee kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira hiyo ya Serikali ya Awamu ya Sita utaiona hata kwenye kuongeza bajeti ya TARURA kwa maana ya kuhudumia barabara hizi muhimu za wilaya. Utaona wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani bajeti ya TARURA ilikuwa ni bilioni 275 kwa mwaka, lakini tunavyozungumza wakati huu tunatarajia katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 bajeti ya TARURA itakuwa ni trilioni 1.18, kwa hiyo, dhamira unaiona. Katika Wilaya ya Karatu DC, kipindi cha miaka hii minne utaona kwamba jumla ya shilingi bilioni 7.8 zimetumika kwa ajili ya kuboresha barabara zetu hizi za wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, tunatajaria kuwa na bajeti ya bilioni 2.25 katika Wilaya hii ya Karatu DC. Kwa hiyo, ninaomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwenye maswali yako yote mawili kwamba, Serikali itaendelea kuhakikisha kila mwaka wa bajeti inatenga fedha kwa ajili ya kuja kuhudumia na kuboresha miundombinu ya barabara hizi muhimu kabisa katika Wilaya hii ya Karatu DC ili ziweze kuwanufaisha wananchi kiuchumi, lakini kuwawezesha kufikia huduma za muhimu kabisa za kijamii.

Name

Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara za lami katika Mji Mdogo wa Karatu?

Supplementary Question 2

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Mtwango ni mji mdogo katika Jimbo la Lupembe na kuna barabara za TARURA pale, palikuwa na barabara ndogo ambayo ujenzi ulianza, lakini hauendelei. Ni lini ujenzi wa lami Mtwango utakamilika Mheshimiwa Naibu Waziri?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kusisitiza kwamba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha barabara hizi muhimu kabisa za wilaya ambazo zinasimamiwa na TARURA zinaendelea kuimarika na zinaweza kupitika katika kipindi cha mwaka mzima. Dhamira hii ya Serikali utaiona jinsi gani kila mwaka wa bajeti fedha zinatengwa kwa ajili ya kuhakikisha mtandao mrefu zaidi wa barabara hizi za TARURA unaweza kufikiwa na barabara hizi zinakuwa katika hali nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Edwin Swalle kwamba hata katika eneo hili alilolitaja eneo la Mtwango Serikali itafika italeta fedha kwa ajili ya kuhakikisha inajenga barabara hiyo, inaweka miundombinu yote muhimu kwa ajili ya kuwezesha barabara hizi muhimu kabisa kiuchumi, lakini kijamii ziweze kuwa katika hadhi nzuri na ziweze kuwanufaisha wananchi.