Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka magari kwenye vituo vya Polisi Mkoani Mbeya?

Supplementary Question 1

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niishukuru Serikali kwa namna ambavyo imetupatia hizo gari 12. Hata hivyo, Mkoa wa Mbeya ni mkoa ambao ni mkubwa sana. Pamoja na gari hizo 12 Wilaya ya Rungwe kuna gari ya double cabin ambayo Serikali wametupatia. Gari hiyo haiwezi kutosheleza mahitaji kwa sababu kama kumetokea uhalifu, mauaji, gari haiwezi hiyo ya double cabin kupakia mwili wa marehemu. Vilevile, Busokelo hakuna gari. Ukienda Mbarali kuna shida kwa sababu gari ipo moja ambayo ni nzima na inatakiwa ifike mpaka kule Madibila, Chimala, Lwiwa na Luhanga, lakini gari hakuna. Pamoja na hayo, Mbeya Mjini kuna gari lakini gari hizo hazitoshelezi. Mbeya DC hakuna gari kabisa. Mbalizi nako ni Mji mkubwa sana na hivyo kunakuwa na uhalifu wa mara kwa mara; bado Uyole hakuna gari yoyote, mpakani mwa Inyala hakuna gari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakwenda kuuliza swali langu la kwanza; Chunya ni kubwa mno ipo mpaka mpakani mwa Tabora hakuna gereza, gari hiyo hiyo itumike kutafuta waharifu lakini ipeleke watuhumiwa Mbeya Mjini. Je, ni lini Serikali itapeleka magari ya kutosheleza mahitaji ya Mkoa wa Mbeya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Mkoa wa Mbeya pale kwa masikitiko makubwa, pamoja na gari hizo ambazo zipo service inapelekwa fedha kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano kwa mkoa mzima, ndizo zinapelekwa pale, ilhali magari 10 ni mabovu na yanatakiwa kutengenezwa pesa hakuna lakini pamoja na hilo magari ambayo ni mabovu kabisa hayatengenezeki yapo 11…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Suma, Waziri ameshakuelewa.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, lakini Ziwa Nyasa kule kuna boat ambalo linatakiwa kukamata wahalifu, boat lile limeharibika muda mrefu, ninaomba Serikali iseme hapa itatengeneza lini magari? (Makofi/Kicheko)

Name

Daniel Baran Sillo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mbeya. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kwa ufatiliaji wake mkubwa kuhusiana na vitendea kazi katika Mkoa wa Mbeya yakiwemo magari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kweli tunajua kwamba Mkoa wa Mbeya ni mkubwa, na ndiyo maana ndani ya miaka miwili, mwaka wa fedha 2022/2023 na 2024/2025 tumepeleka gari 12. Hata hivyo, bado mahitaji ni makubwa. Nimhakikishie Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha sana vitendea kazi katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Polisi. Kwa hiyo bado Mkoa wa Mbeya utaendelea kuangaliwa kwa jicho la tofauti kwa ukubwa wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu service ya magari; ni kweli fedha hutengwa kila mwaka kwa ajili ya service ya magari. Nimhakikishie kwamba Jeshi la Polisi lipo makini litaendelea kufanya service ya magari hayo ili yaweze kuhudumia wananchi wa Mbeya na Wilaya zote ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja. Ahsante sana. (Makofi)