Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Christina Christopher Mnzava
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA K.n.y. MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Je, lini Serikali itaipatia ufumbuzi changamoto ya upungufu wa vifaa tiba na watumishi kwenye baadhi ya vituo vya afya nchini?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja na juhudi kubwa ambazo zinafanywa na Serikali ya kuhakikisha kwamba wanaboresha huduma za afya kwa maana ya kuwepo na vifaa tiba vya kutosha bado kumekuwa kuna changamoto ya vifaa. Baadhi ya dispensary na vituo vya afya akinamama wajawazito wananunua vifaa kwa ajili ya kujifungulia na Sera ya Afya inasema mama mjamzito anatibiwa bure. Swali la kwanza; je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na suala hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika Mkoa wa Shinyanga kuna changamoto kubwa ya watumishi: Msalala, Ushetu, Kahama, Shinyanga Vijijini, pamoja na Shinyanga Municipal. Kuna sehemu unakuta watumishi wengi, sehemu nyingine wachache. Je, ni nini kauli ya Serikali kwa vituo vya afya na zahanati kufanya reallocation ya watumishi ili sehemu zingine ambazo hazina watumishi, ziweze kupata watumishi? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tuna vituo vya afya ambavyo vinatoa huduma na Sera ya Afya inaelekeza kwamba, huduma kwa akinamama wajawazito, watoto wa umri chini ya miaka mitano na wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea ambao hawana uwezo wa kifedha, wanatakiwa kupata matibabu bure. Serikali imeendelea kutekeleza sera hii kwa ufanisi
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunafahamu kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Christina Mnzava bado kuna changamoto kwenye baadhi ya vituo kuwatoza akinamama wajawazito wanapokwenda kupata huduma hususani za kujifungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuelekeza halmashauri zote kote nchini kwamba ni maelekezo na kauli ya Serikali kwamba lazima wahakikishe vifaa vyote vya muhimu kwa ajili ya huduma za kujifungua zinapatikana vituoni. Akinamama wajawazito wakienda kupata huduma hizo wasitozwe fedha yoyote lakini gloves na vifaa vingine vyote lazima vipatikane. Kwa sababu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya dawa na vifaa tiba. Kwa hiyo, ni wajibu wao kuhakikisha kwamba vifaa hivyo vinapatikana katika vituo vyao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na upungufu wa watumishi kwenye Halmashauri ya Kahama, Msalala, Shinyanga Vijijini na Municipal, ni kweli lakini hii Serikali imeendelea kuajiri watumishi. Kwa kipindi cha miaka minne iliyopita zaidi ya watumishi 25,917 wameajiriwa na hivi karibuni watumishi wameajiriwa na kupelekwa kwenye halmashauri zote zikiwemo hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, zoezi hili ni endelevu, tutaendelea kuajiri watumishi na kuwapeleka maeneo yote ya upungufu ili kuboresha huduma. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved