Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Primary Question

MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza:- Je, ni hatua ipi imefikiwa na Serikali kuanza ujenzi wa Daraja la Kisorya – Lugezi linalounganisha Wilaya ya Ukerewe na Bunda?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa hatua iliyokwishachukua ya ukamilishaji wa kivuko, pamoja na hatua hiyo ya upembuzi na upembuzi yakinifu kwenye daraja hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kutokana na umuhimu wa daraja hili wa kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Ukerewe, Serikali iko tayari sasa kuweka kwenye bajeti ya mwaka ujao 2025/2026 ili ujenzi wa daraja hili uweze kuanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mkataba wa Barabara Unganishi kati ya Rugezi – Nansio ulitakiwa kukamilika tarehe 4 mwezi wa Pili na mkandarasi huyo alishafika site akaanza kazi, akaharibu madaraja na barabara ile, hali ambayo imesababisha usumbufu mkubwa sana kwa wananchi wa Ukerewe. Sasa, napenda Serikali iwaambie wananchi wa Ukerewe, nini hatma ya Barabara hii ya Kisorya – Rugezi? Nashukuru.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe kwa pongezi kwa Serikali, lakini pia, namhakikishia kwamba, daraja hili, kama nilivyosema, tulishalisanifu. Ni daraja refu ambalo linavuka Ziwa Victoria, lenye zaidi ya kilometa 100. Serikali kwa kuona kwamba, itachukua muda ndiyo maana iliamua kujenga kivuko kipya, kikubwa ambacho kiko kwenye hatua za mwisho kabisa, kwa ajili ya kuunganisha Ukerewe na Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tumekuwa tunatenga. Hata mwaka unaokuja tutatenga kwenye bajeti fedha ya kuanza ujenzi wa daraja hili la Kisorya – Rugezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ni kwamba, ni kweli mkandarasi na bahati nzuri ni mkandarasi mzawa ambaye amefanya kazi nzuri, ameshaleta maombi ya malipo yake ya fedha, hati za malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunafahamu na tunafanya jitihada tumlipe ili aweze kuendelea na kuikamilisha hiyo kazi ambayo ameshaianza. Ahsante.