Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mashimba Mashauri Ndaki

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Magharibi

Primary Question

MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:- Je, lini Serikali itaanzisha Mfuko wa kuimarisha bei za mazao, ili kusaidia wakulima wa pamba na mazao mengine bei inaposhuka?

Supplementary Question 1

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa bei ya mazao haya mwaka jana, hasa pamba, ilikuwa iko chini na mwaka huu 2025 wakulima hawana uhakika wa bei ya mazao hayo. Je, Mfuko huu wa Serikali ambao tayari umeanzishwa, unawasaidiaje wakulima kuwa na uhakika wa bei ya mazao yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa huko nyuma tulikuwa na bei elekezi ya pamba, ikitangazwa na Serikali mwezi wa Septemba ama wa Oktoba ili kuwahamasisha wakulima waweze kulima kwa wingi na kwa tija mwaka unaofuata. Je, Serikali inaonaje kurudisha utaratibu huo ili kuwahamasisha wakulima waweze kulima pamba kwa wingi? Ahsante.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mawili mazuri kabisa kwa wakulima wa pamba. Jambo moja ambalo namhakikishia ni kwamba, endapo bei ya pamba mwaka huu itashuka chini ya kile kiwango ambacho kinatarajiwa, maana yake ni moja ya kazi ya huu Mfuko ni kutoa ruzuku kwa wakulima wa pamba, ili kuhakikisha wanapata bei nzuri. Kwa hiyo, Mfuko utafanya kazi yake kama ambavyo umeundwa kwa kusudi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kurejesha ule mfumo wa awali wa kuweka bei elekezi kati ya Mwezi Septemba na Oktoba, sisi huwa tunapokea maoni ya wadau na tukishayapokea tunayafanyia kazi. Kwa hiyo, kama watakuwa wameachana na soko huru, maana yake ni sasa sisi tutarudi tuzungumze nao. Kama wao watakubali, maana yake ni Serikali tutarudi katika mfumo wa awali. Kwa hiyo, kwa sasa tunapokea kama maoni ambayo tunaweza kwenda kuyafanyia kazi. Ahsante.