Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Michael Constantino Mwakamo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Primary Question

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:- Je, lini Bandari ya Kwala itaanza kutumika kwa uhakika Kibaha Vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru na pia naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa umuhimu wa Mji wa Kwala ambao una bandari kavu, una kongani kubwa ya viwanda, una Mji wa Magindu unakua kwa kasi, Mji wa Chalinze unakua kwa kasi. Je, Serikali haioni sasa ni muda sahihi wa kujenga kituo cha treni ya SGR, mahali ambapo treni zinapishana ili wananchi wa maeneo hayo wanaotaka kuingia kwenye Mji la Kwala waingie kirahisi na kupata huduma zinazostahili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Bandari Kavu ya Kwala kazi yake ni kupokea mizigo inayotoka kwenye bandari zingine na inayoingia pale kwa njia ya treni. Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuiunganisha Bandari ya Kwala na Bandari ya Bagamoyo?

Name

David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mwakamo kwa maswali yake ya msingi ambayo ameendelea kuyafuatilia na jinsi ambavyo anatusaidia kama sekta kuona umuhimu mkubwa wa eneo la Kwala pamoja na Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimhakikishie kwamba, tayari Serikali imekwishaona umuhimu mkubwa wa kuunganisha Bandari ya Kwala pamoja na reli zote tatu, kwa maana ya Meter Gauge ya TAZARA pamoja na Meter Gauge ya TRC, Cape Gauge ya TAZARA na SGR. Tayari kituo kimeshawekwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kilometa 1.3 ya reli ya meter gauge imeshaunganishwa na katika eneo hilo husika. Hivyo, basi tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba eneo hili la Bagamoyo, eneo hili la Pwani ambalo ni kongani ya viwanda na linakwenda kuwa na uchumi mkubwa, linakuwa linaunganishwa moja kwa moja na reli hii ili kutoa mizigo sehemu moja kupeleka mizigo sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yake ya pili ni kuhusiana na bandari ya Bagamoyo namna gani inaweza kuunganishwa pamoja na Kwala. Moja, nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge, jinsi ambavyo Serikali imefanya kazi kubwa kuendelea kuboresha bandari nchini na hii inafanyika kwa sababu ya potential ya mizigo mingi iliyopo katika nchi jirani, ambapo ni muhimu tuboreshe bandari zetu ili tuweze kufikia masoko ya nchi zote zinazotuzunguka ikiwa ni pamoja na central corridor, nchi za kusini, kanda ya ziwa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hilo pamoja na maboresho ya bandari zetu mbalimbali ambayo tumefanya ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Mtwara, Tanga pamoja na bandari zilizopo katika Maziwa ya Tanganyika na Nyasa, Serikali imeona umuhimu wa Bandari ya Bagamoyo kwa sababu pamoja na kazi hiyo kubwa meli kubwa za maximum zinazoweza kutua katika bandari zetu ikiwemo Dar es Salaam ni za mita 320.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Bandari ya Bagamoyo ndiyo yenye uwezo mkubwa ya kuweza kupokea meli kubwa zaidi kwenda mpaka mita 400. Katika kutimiza hilo Serikali ina mpango wa kuunganisha Bandari ya Bagamoyo, Kwala na Bandari Kavu ya Kwala ili mizigo inayotoka sehemu mbalimbali duniani, ikitua pale Bagamoyo iweze kuunganisha moja kwa moja Kwala na kwenda sehemu mbalimbali inakohitajika ndani ya nchi yetu na nje ya nchi yetu.