Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Amina Nassoro Makilagi
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:- Sheria ya Ndoa imekuwa kandamizi kwa wanawake na watoto:- Je, ni lini sheria hii italetwa Bungeni ili ifanyiwe marekebisho?
Supplementary Question 1
MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na kuipongeza Serikali kwa kuleta Muswada na Bunge lililopita Wabunge tukatunga sheria kali sana ambayo itawabana wale wote waliokuwa na tabia ya kuwaoa watoto. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania iliiagiza Serikali iifanyie marekebisho Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, kama kweli dhamira ni nzuri kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameeleza, ningependa kujua, ni kwa nini Serikali iliamua kukata rufaa badala ya kutekeleza maamuzi ya Mahakama? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa sheria nyingi sana ambazo zinawakandamiza wanawake na watoto, bado zipo katika nchi yetu ya Tanzania, zikiwepo hata sheria za kimila na nyingine na nyingine. Ningependa kujua sasa, Serikali ina mkakati gani na hasa Wizara ya Katiba na Sheria, kuhakikisha inaleta sheria zote kandamizi zinazowabana wanawake na watoto ili sheria hizi tuweze kuzifanyia marekebisho? (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Amina Makilagi kwa kupigania haki za akinamama bila kuchoka, matunda ya juhudi zenu, wewe mwenyewe Mheshimiwa pamoja na wanawake wenzako yanaonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuhusu kesi iliyokuwepo Mahakamani na kwa nini Mwanasheria Mkuu wa Serikali imebidi akate rufani, nimeeleza katika jibu langu la msingi kwamba Serikali inaona tatizo katika Sheria ya Ndoa, si kwamba haioni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotupeleka Mahakama ya Rufani ni vitu viwili. Kwanza, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, tayari iko katika mchakato chini ya Wizara yangu na utaratibu tunaoutumia tulidhani itakuwa vyema kwa mshikamano wa Taifa letu tukaendeleza majadiliano kama tulivyofanya wakati wa kuitunga hii sheria ya mwaka 1971. Sisi tunataka tu kupata busara za Mahakama ya Rufani kuhusu suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, haki ya kukata rufani si tu ya wananchi, lakini vilevile hata Serikali pale ambapo inaona kuna kitu ambacho kinahitaji kupewa msimamo madhubuti zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii anaweza akatokea Jaji mwingine wa Mahakama Kuu akatoa uamuzi tofauti kwa sababu wote wako katika maamuzi. Sasa tunachotafuta na anachotafuta Attorney General ni kupata sasa maamuzi kwenye Mahakama yetu ya juu katika nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ni kweli kabisa bado kuna baadhi ya sheria zinamkandamiza mwanamke lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Amina Makilagi na wanawake wenzake kwamba tumepiga hatua kubwa mno toka uhuru katika kuhakikisha kwamba mwanamke anapata haki sawa kama ambavyo Katiba yetu inavyosema chini ya Ibara ya 13.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke, tumefanya mabadiliko ya sheria nyingi, tukumbuke Sheria ya Ardhi namba Nne (4) na namba Tano (5) imeondoa kabisa ubaguzi uliokuwepo kwa mwanamke. Sasa hivi mwanamke ana haki sawa chini ya sheria hizo. Leo si kawaida tena kwa mume akatoka tu asubuhi akauza nyumba, akauza kiwanja bila kupata ridhaa ya mama na mama akienda Mahakamani hiyo sale ama mauzo hayo hayana maana kabisa. Leo hii akinamama talaka haitokei akaondoka hivi hivi lazima kugawana matrimonial property, hizo zote kwa kweli ni faida ambazo tumezipata katika mabadiliko mbalimbali ya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nenda Jela; wafungwa wengi wanaotumikia vifungo virefu katika nchi hii ni wale ambao wana makosa ya kunyanyasa akinamama. Namshukuru Mheshimiwa Makilagi ameelezea kuhusu sheria tuliyobadilisha juzi tu hapa Sheria ya Elimu ambapo leo hii mtoto wa kike aliye sekondari, aliye shule ya msingi, akipata mimba ole wako wewe uliyefanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yote hii ni kulinda na baada ya muda si mrefu tutaleta Muswada hapa wa Huduma ya Msaada wa Sheria ambayo nakuhakikishia utakuwa mkombozi mkubwa hasa kwa akinamama walioko vijijini ambao katika mfumo tulionao usiojali mtu kutokujua sheria; kwamba ignorance of the law is not defence, akinamama wengi watafaidika sana. (Makofi)
Name
Khatib Said Haji
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Konde
Primary Question
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:- Sheria ya Ndoa imekuwa kandamizi kwa wanawake na watoto:- Je, ni lini sheria hii italetwa Bungeni ili ifanyiwe marekebisho?
Supplementary Question 2
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Katika imani ya dini ya Kiislam, suala la ndoa na mirathi ni jambo ambalo halina mjadala wala mbadala. Je, mabadiliko yote ya sheria yanatuhakikishiaje kwamba hayataingilia uhuru na imani katika dini ya Kiislam? (Makofi)
Name
Dr. Harrison George Mwakyembe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Answer
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu kwa kifupi sana Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ndiyo sababu. Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anakwenda Mahakama ya Rufani akidai si moja kwa moja, lakini kama nilivyowaeleza hapa kwamba mchakato tuliouanza Serikali wa majadiliano sisi Watanzania, maridhiano utumike badala ya sisi kuja na Muswada, wanaosema ndiyo, ndiyo tukapitisha sheria hapa, nadhani nimeeleweka na Mheshimiwa Mbunge.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved