Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha Watu wenye Ulemavu wanajikwamua kimaisha?

Supplementary Question 1

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu hayo mazuri ambayo amenipa, moja ya sababu ya baadhi ya watu wenye ulemavu kutokuwa na uchumi imara ni upatikanaji wa elimu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi tunajua hali zao zilivyo na wanapata adha sana kwenye ada wakiwa vyuoni, shuleni na halikadhalika wakiwa kwenye elimu ya juu; kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa ruzuku. Swali la kwanza; je, kwa nini Serikali isiwapatie ruzuku hawa watu wenye ulemavu wakiwa masomoni ili waweze kupata elimu vizuri na baadaye wajikwamue kimaisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano kwa kutumia lugha za alama kwa hawa watu wenye ulemavu wakienda kupata mahitaji katika jamii, kwamba wengi wanashindwa kuwaelewa hawa watu wenye ulemavu na baadaye hatimaye wanaweza kuajiri watu ili waweze kuwasaidia; ambapo inakuwa ni adha kubwa kwao. Je, Serikali haioni haja Wizara yao pamoja na Wizara ya Elimu wakashirikiana pamoja ili waweze kufundisha lugha ya alama kwa walimu wote na wanafunzi wote ili waweze kupata hiyo elimu ya lugha ya alama ili wale watu wenye ulemavu wanapochanganyika na jamii waweze kupata mambo ambayo yatakayowasaidia kiuchumi?

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimia Mwenyekiti, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tendega, kama alivyoeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakubaliana na Mheshimiwa Tendega kwamba, watu wenye ulemavu, ambao mimi ni wajomba zangu, wanapata changamoto kubwa sana hasa kwenye masuala ya elimu. Hata hivyo, zingatio hilo lilionwa na Mheshimiwa Rais alipokutana nao Chamwino – Dodoma, mwezi Machi, 2022 na walieleza moja ya changamoto ilikuwa ni hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maagizo ya utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais yalitolewa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu. Mojawapo ilikuwa ni kuhakikisha miundombinu rafiki inakuwepo kwenye maeneo yote ya utoaji elimu ikiwemo shule, utoaji wa vifaa saidizi na vifaa mwendo. Vilevile, Mheshimiwa Rais aliongeza bajeti ya kusaidia watu wenye ulemavu kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. Katika hatua nyingine tuliamua kuunda Mfuko Maalum wa Watu Wenye Ulemavu na kufungua akaunti maalum kupitia BOT ambayo tayari kwa mwaka huu fedha imeshawekwa shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kuwasaidia kwenye mambo ya elimu na uwezeshaji kwa ujumla, ikiwa ni sambamba na na kuwatengenezea mazingira mengine ya uwezeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, Mfuko wa TASAF unazingatia watu wenye ulemavu, Mfuko wa 10% zile zinazotoewa na halmashauri unazingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu. Vilevile, kipengele cha ajira kuna mwongozo wa asilimia tatu ya ajira zote zinazotolewa nchini. Pia, hata wanapokwenda kwenye ushindani wa kielimu au wa ajira kuna upendeleo maalum ambao unatolewa kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ikiwa ni sambamba na kufungua shule zilizokuwa zimefungwa zaidi ya miaka 10.

Mheshimia Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa ya kutengeneza shule ambazo zitasaidia. Ukiacha elimu ya juu pia zipo za elimu ya kati, ufundi na za marekebisho. Pale Sabasaba – Singida tayari imekwishakufunguliwa; Lwanzali – Tabora (Mtapika) linaendelea kujengwa; Milongo – Mwanza na Yombo – Dar es Salaam. Zote hizi ni za elimu jumuishi kwa ajili ya kuweza kuwasaidia watu wenye ulemavu ili kujipatia elimu na kuweza kusaidiwa. Thamani yake ni zaidi ya shilingi bilioni tatu ambayo Mheshimiwa Rais aliitoa. Pia bilioni 3.6 nyingine Mheshimiwa Rais ameitoa kwa ajili ya kufungua shule na vyuo vingine kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la pili la swali la Mheshimiwa Mbunge Mama Tendega ni kuhusu lugha za alama. Kupitia Bunge lako Tukufu na niwambie Watanzania, Mheshimiwa Mbunge ambaye ameuliza swali na wajomba zangu; habari njema ni kwamba, tayari tumekwishaanza kufanya mabadiliko ya mitaala, ukiacha hata mtaala rasmi kupitia Wizara ya Elimu. Tunataka sasa lugha ya alama iwe ya watu wote kwa sababu wanahitaji msaada na wanajumuika na jamii kwa watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tumeanza kwenye televisheni yetu ya Taifa unaona kuna mtu anatafsiri habari kwa lugha ya alama kwenye Bunge lako Tukufu na kwenye shughuli za kitaifa ambazo zimekuwa zikifanyika tumeweka zingatio hilo. Kwa hiyo, nikijbu swali la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tuko tayari kuweza kuhakikisha mazingatio haya yanakuwepo na wajomba zangu hawa watu wenye ulemavu tunazingatia haki zao kwa sababu hujafa hujaumbika na sisi wote ni waja wa Mwenyezi Mungu. Ahsante.