Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FATMA HASSAN TAUFIQ K.n.y. MHE. MARYAM AZAN MWINYI aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa Wafanyakazi wa Majumbani unaozidi kukithiri kwenye Jamii?

Supplementary Question 1

MHE. FATMA H. TAUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; pamoja na kuwa Serikali imesema italeta mkataba huo, imekuwa ni muda mrefu sana. Je, Serikali inaji-commit vipi kuleta mkataba huu C189 ili kuweza kuwalinda wafanyakazi hao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; baadhi ya wafanyakazi wa ndani ni watoto ambao wako chini ya miaka 18. Hawa wako katika hatari kubwa sana ya kufanyiwa ukatili. Je, Serikali haioni kwamba imefikiwa wakati sasa wa kupata data kamili ili kuweza kuwanusuru watoto hawa? Ahsante.

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze tu hapa kama Mheshimiwa Taufiq alivyouliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Maryam. Ni kweli kama Serikali tunatambua kwamba kuna manyanyaso makubwa sana wafanyakazi wa ndani wanayapata na hasa ni kwa sababu makubaliano ya kikazi yanakuwa hayajajengewa msingi wa kisheria. Hata wakati mwingine imesababisha kufanya kazi kwa wafanyakazi ambao wako chini ya umri unaotakiwa kwa mujibu wa sheria hata ile Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo pia, wapo wapo wafanyakazi ambao wamekuwa wakinyanyaswa, wakipewa ujauzito na wakati mwingine wakinyimwa chakula na kunyanyaswa kwa sababu hii ni kazi pekee ambayo unakula kazini na unalala kazini; lakini pia ni kazi ambayo ni kubwa sana kwa sababu malezi yote ya watoto kwa Taifa kwa sehemu kubwa yamekuwa yakichangiwa na wafanyakazi wa ndani. Siku hizi familia watu wamekuwa busy, wazazi wanawaachia majukumu wafanyakazi wa ndani wa kike au wa kiume na matokeo yake hata ule mmomonyoko wa maadili unaanzia hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo, kwamba kumekuwa na hizi changamoto, tumeamua na tumedhamiria kuhakikisha kuwa mkataba huo Serikali inausaini; na tumekwishafika kwenye hatua kubwa. Hatua ya kwanza ya ngazi ya Wizara, hatua ya pili kupitia kwenye ngazi ya Baraza la Mawaziri kupitia committee ya watendaji (wataalam) na tunasubiri hatua nyingine ambazo ni za kumalizia. Kwa sababu tunatambua kwamba kwenye eneo hili wapo wafanyakazi ambao si tu wa kike peke yake, hata wa kiume wamekuwa wakinyanyasika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia hata kabla hatujasaini sheria hii kuomba sisi wazazi wa kike na wa kiume kutokukaimisha majukumu yote pia hata kwa wafanyakazi hawa wa ndani. Kwa sababu kuna wakati wanakaimisha majukumu ya kufua nguo za baba, kufanya kila kitu na chakula. Matokeo yake hatimaye kuna kazi ambazo hazikaimishwi watoto hawa wamekuwa wakijikaimisha au wazazi kulazimisha na inaleta migogoro ya kindoa wakati mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia haya tunataka tuone kwamba, hata mafunzo ya wafanyakazi wa ndani yazingatiwe. Tuwe na mafunzo maalum na wakiajiriwa tujue umri, anakotoka na stahiki zake nyingine za afya na usalama mahali pa kazi, muda wa kazi; kwa sababu wengine wanafanya kazi muda wote, hata usiku wa manane anaamshwa afanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuliangalia hili kwa uchungu mkubwa alionao Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekwishakutoa maagizo mahususi; na maelekeo ya utekelezaji Mheshimiwa Waziri Mkuu amekwishatupatia na hivi karibuni mkataba huu tutamalizana nao. Mheshimiwa Waziri wangu Ridhiwani Kikwete anafahamu kwamba mkataba huu umeshafikia hatua nzuri na yeye ananiona anatikisa kichwa hapo. Kwa hiyo, jambo hili tumelipokea kama Serikali na tutalifanyia kazi haraka sana.

MWENYEKITI: Ninakushukuru sana Mheshimiwa. Ninaona Mheshimiwa Waziri anataka kusimama, Mheshimiwa Ridhiwani.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ninataka niyaunge mkono na ni maelezo ya kweli, ninataka kuongeza katika lile eneo la ahadi ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ametuelekeza sisi kama Wizara na katika utaratibu ambao unaweza kuwa ni mpya kabisa katika maelekezo ya Mheshimiwa Rais, ameelekeza Wizara na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri ikutane pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza leo hii kazi hiyo ya kukutana kwa Wizara na Cabinet ya Secretariat inakamilika leo. Kwa hiyo, ninataka nilihakikishie Bunge lako kwamba tuko katika hatua nzuri; na sasa hivi ni kupeleka kwenye Cabinet ili baada ya hapo tuweze kuleta mbele ya Bunge lako kwa ajili ya kupitia mkataba huo. Ninashukuru.