Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Primary Question

MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda?

Supplementary Question 1

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Mwaka wa fedha wa Serikali ulioisha Serikali ilileta shilingi milioni 800 kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali hiyo. Baada ya mwaka wa fedha kuisha halmashauri ikawa imetumia zaidi ya shilingi milioni 150 katika hizo shilingi milioni 800. Shilingi milioni 650 ikarudi Serikalini. Je, ni lini sasa Serikali itarudisha hizi fedha shilingi 650 ili ziende kutusaidia kukamilisha hospitali hii ya Halmashauri ya Mji wa Bunda?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Robert Maboto kwa swali lake lenye lengo la kuhakikisha kwamba sekta ya afya na hasa afya msingi katika Jimbo lake inaimarika. Ninaomba nimhakikishie kwamba kila mwaka wa bajeti Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kuendelea kuimarisha miundombinu ikiwemo miundombinu ikiwemo miundombinu ya Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie kiwango hicho cha fedha alichokitaja ni taratibu tu za Kiserikali, lakini ile fedha ilishatengwa na itafika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inaendeleza ujenzi. Kwa hiyo, nitazungumza na Mheshimiwa Mbunge kuona kwamba wamekwama wapi lakini ni taratibu tu za Kiserikali za kuhakikisha kwamba fedha hiyo baada ya kuwa imevuka mwaka kuna utaratibu wa kuiombea na inaweza ikatumwa katika halmashauri kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Primary Question

MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba, Kituo cha Afya cha Buswelu kina jengo moja tu la OPD na hakijakamilika mpaka leo. Sambamba na hilo, Kituo cha Afya Sangabuye ambacho ni cha mwaka 1974 mpaka leo miundombinu yake haijakamilika. Je, ni lini vituo hivi miundombinu yake itakamilishwa ili watu waweze kupata huduma kwa uhakika?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula kwa swali lake zuri linalolenga kuimarisha sekta ya afya msingi hususan kwenye Jimbo lake. Ninaomba nimtaarifu kwamba Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne imefanya uwekezaji wa zaidi ya shilingi trilioni 1.29 katika kuimarisha miundombinu katika sekta hii ya afya msingi. Pia, katika kipindi cha miaka hiyo minne ujenzi wa vituo vya afya 367 umefanyika ikiwemo pia na ukarabati wa hospitali na vituo ambavyo ni vya zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea na jitihada hizo na itafika katika vituo vya afya hivi viwili alivyovitaja, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inavikamilisha na vinaweza kutoa huduma ya afya iliyo bora kwa wananchi wake.

Name

Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda?

Supplementary Question 3

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali ilitupatia fedha kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Tarafa ya Nampungu na majengo yalikwishakamilika kwa muda mrefu sana na ujenzi ule haujaendelea. Je, ni lini Serikali itatupatia shilingi milioni 250 za awamu ya pili ili kukamilisha Kituo cha Afya kile na kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya afya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Tunduru?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Kungu kwa swali lake hili linalolenga kuimarisha huduma za afya msingi katika Jimbo lake. Serikali imekuwa ikiimarisha miundombinu katika sekta hii ya afya na imekuwa ikifanya hivyo kwa kutenga fedha kila mwaka wa bajeti kujenga miundombinu kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari katika kituo cha afya alichokitaja shilingi milioni 250 ililetwa kwa ajili ya majengo ya awali. Ninaomba nimhakikishie kwamba Serikali inaleta fedha iliyosalia kwa ajili ya kuendelea na awamu nyingine ya kukamilisha majengo yale ili kituo hiki cha afya kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi; na wananchi wasipate adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya.

Name

George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Primary Question

MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza:- Je, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda?

Supplementary Question 4

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Iwondo kilichoko Jimbo la Mpwapwa?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa George Malima kwa swali hili ambalo linalenga kuhakikisha na kupaza sauti na kuona kwamba huduma za afya msingi zinaimarika katika jimbo lake. Ninaomba nimhakikishie kwamba Serikali inafanya uwekezaji mkubwa sana wa kuendelea kuimarisha miundombinu katika sekta hii muhimu kabisa ya afya msingi. Katika jimbo lake fedha italetwa kwa ajili ya kukamilisha kituo hiki cha afya alichokitaja.