Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abdallah Dadi Chikota

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyamba

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini ukarabati na upanuzi wa Mradi wa Maji Makonde utakamilika?

Supplementary Question 1

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali. Kwanza, nitumie nafasi hii kumpongeza Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha nyingi na kuokoa Mradi wa Makonde ambao kwa miaka mingi ulikuwa haujatekelezwa, kwa hiyo ninaishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa Mkandarasi ambaye anaendelea na ujenzi wa mradi anafanya kazi kwa kusuasua kwa changamoto ambazo Serikali inazifahamu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitatua hizi changamoto ili Mkandarasi wetu aendelee na kazi yake? Ninakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwenye upande wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, kuna mradi mdogo umesanifiwa kwa ajili ya kutoa maji Kijiji cha Nyundo na kupeleka Kata ya Nima, Hinju na Njengwa. Je, mradi huo mdogo umefikia katika hatua gani ya utekelezaji? Ahsante sana.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kutumia fursa hii pia kumshukuru sana na kumpongeza sana Mheshimiwa Chikota kwa kupitisha Bajeti ya Wizara ya Maji, bajeti ambayo imevunja rekodi kwa kipindi cha kwanza kwa ongezeko la 31%. Hii inaonesha namna gani commitment ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi kupata huduma ya maji safi na salama. Waswahili wanasema mwenye haki akitawala nchi hujaa neema na kwa hakika kwa bajeti hii kwa kweli tunaenda kuona miradi mingi ikitekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chikota natambua Mradi huu ambao unaenda Newala- Tandahimba- Nanyamba kwa Mheshimiwa Maimuna, Mheshimiwa Mkuchika, Mheshimiwa Katani pamoja na wewe mwenyewe ni jicho la Serikali kuona wananchi wa maeneo haya Mradi huu wa Makonde unaenda kukamilishwa na waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mdogo ambao umesanifiwa Mheshimiwa Mbunge amesema, tunafahamu dhamira yake na anapenda sana kuona wananchi wake wakinufaika; huu Mradi unaitwa Nyundo – Lipwidi. Kutakuwa na tenki litakalojengwa pale Nyundo, lakini utaweza kuhudumia vijiji takribani 11. Vilevile unaenda kwenye Kata za Njengwa, Mnina pamoja Hinju zile kata zote tatu kwa umoja wake kutakuwa na vijiji 11.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mradi huu tayari umesanifiwa, bilioni 14 zinakadiriwa kuhitajika na tumeshaanza mchakato wa manunuzi tuko kwenye prequalification na baada ya hapo tunaomba kibali Wizara ya Fedha wakishatoa tutatangaza ili kumpata Mkandarasi ili mradi huu uweze kukamilika na bahati nzuri umeingizwa kwenye bajeti ya mwaka huu 2025/2026. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, mradi huu utaenda kutekelezwa vizuri na utakamilika kwa wakati. Ahsante sana.

Name

Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini ukarabati na upanuzi wa Mradi wa Maji Makonde utakamilika?

Supplementary Question 2

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Mimi nina swali tu la nyongeza kwamba, wakati tunasubiri mradi huu mkubwa wa Makonde kuendelea kukamilishwa au kuendelea kwenye ujenzi wake. Upi mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba, ile miradi midogo ya visima ambavyo vimechimbwa kule katika kila jimbo vitaanza kutoa huduma na wananchi wakawa wanatumia hayo maji kwa uhakika? Ahsante.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la mama yangu Maimuna, Mbunge wa Newala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana mama yangu kwa kuendelea kuwapigania wananchi na kuhakikisha kwamba, anaiishi kwa vitendo falsafa ya Daktari Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani kwa yeye kuendelea kuwa kisemeo kwa ajili ya wananchi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba, programu ya visima 900 ni programu ambayo Daktari Samia Suluhu Hassan alilitazama hilo na kuona kwamba kuna miradi mingi mikubwa inayoendelea lakini kuna miradi midogo midogo pia. Tukaona kwamba, miradi hii ya visima ndiyo mkombozi wakati miradi mikubwa ikiwa inaendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa muktadha huo nikuhakikishie kwamba mradi wa visima 900 tumeshajiwekea deadline mpaka tarehe 25 Juni visima vyote viwe vimeshaanza kutoa huduma kwa wananchi wote. Ninakushukuru sana.

Name

Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini ukarabati na upanuzi wa Mradi wa Maji Makonde utakamilika?

Supplementary Question 3

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mradi mkubwa wa maji wa Kiwira ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na wananchi wa Mbeya Jiji na wananchi wengi sana wa Mji wa Mbalizi. Mradi huo unasubiriwa kwa hamu hasa wanawake wa maeneo hayo wanapata shida sana kutafuta maji. Je, huo mradi mpaka sasa hivi umefikiwa asilimia ngapi? Wananchi wa Mkoa wa Mbeya wanataka kujua. Ahsante.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la dada yangu. Ni ndani ya mwezi mmoja ameliuliza hili swali mara ya pili leo nadhani hii ni dhamira yake ya moja kwa moja. Huu mradi unawasaidia Wanambeya, Mbeya Mjini pamoja na kwenye Jimbo la Mheshimiwa Spika. Tunatambua umuhimu wa namna gani maji ni msingi wa uchumi wa nchi yetu, tunatambua kwamba maji ni uhai na pia tunafahamu kwamba, maji yakishakuwepo basi kuna adha ambazo zitakuwa zimeondoshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mradi unaendelea kutekelezwa. Majibu ya wiki iliyopita hayawezi kuendana na leo kwa sababu tayari mradi unaendelea kwenye progress mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe hofu kwamba mradi huo unaenda vizuri sana kulingana na makubaliano yaliyopo kwenye mkataba na hata mpaka itakapofikia mwisho wa mkataba mradi huo utakuwa umekamilika na wananchi watapata. Kama akihitaji taarifa za takwimu halisi tukitoka hapa nitaweza kuwasiliana na waliopo site ili waweze kutupatia takwimu halisi kwa ajili ya wananchi wake. Ahsante sana.

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini ukarabati na upanuzi wa Mradi wa Maji Makonde utakamilika?

Supplementary Question 4

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari kufanya tathmini kwenye Wilaya ya Nyang’hwale ili kuweza kupunguza gharama ya bei ya maji kutoka 2000 na kuwa 1500?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Mbunge wa Nyang’hwale. Ni kweli Serikali iko tayari, lakini utayari wa Serikali pia unaendana na aina ya huduma inayotolewa. Kama maji ni maji mserereko gharama haiwezi kufanana tunapotumia nguvu ya solar na vilevile kama maji yanasukumwa kwa pampu ambazo zinatumia umeme wa TANESCO gharama yake pia haiwezi kufanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini itakapofanyika tutaweza kuangalia production cost na ndio inaenda kutoa majibu kwamba, maji yauzwe kwa kiasi gani. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa ushauri huo Serikali tumeupokea. Ahsante sana.

Name

Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini ukarabati na upanuzi wa Mradi wa Maji Makonde utakamilika?

Supplementary Question 5

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanatemeke tunashukuru sana kwa maji ambayo yanaendelea kuwekwa, lakini kuna namna ambayo ya kulipa jinsi ya kuvuta maji kuja kwenye nyumba zetu. Sisi kama Wanatemeke tunatamani kufanya mkataba kati ya wizara na mwananchi mmoja mmoja kwa bei ilivyo kubwa ili tuweze kulipa kidogo kidogo na watukate kwenye bili. Je, wako tayari kufanya mikataba hiyo na sisi Wanatemeke? Ahsante.

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge mahiri kabisa wa Temeke, mwanamama ambaye anaendelea kuwapambania wananchi wake wa Temeke na hakika naamini kabisa kwamba, Novemba atarudi hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo ambalo sisi Serikali daima tumekubali kushirikisha wadau mbalimbali kupokea ushauri na hili nalo ni jambo la msingi sana ambao ni ushauri mzuri ambao tunaupokea, lakini lazima tufanya tathmini tuangalie faida na hasara ya kufanya hivyo na tukiona kwamba, faida ni kubwa kwa maslahi ya wananchi wetu Serikali iko tayari kushirikiana nawe ili kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ambayo inaonekana ni tatizo katika eneo lao. Ahsante sana.

Name

Hamida Mohamedi Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini ukarabati na upanuzi wa Mradi wa Maji Makonde utakamilika?

Supplementary Question 6

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Lindi zawadi mliyotupa ya kutuchimbia visima vitano, vitano kila jimbo maana yake majimbo yote ya Mkoa wa Lindi visima vimechimbwa isipokuwa Jimbo la Lindi Mjini bado visima vitano havijachimbwa na tulielekeza kupeleka katika maeneo ambayo wana uhitaji mkubwa wa maji. Sasa ningependa kujua ni lini watakuja kukamilisha mchakato wa kuchimba visima vitano katika Jimbo la Lindi Mjini?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na unyenyekevu, kwa niaba ya Waziri wa Maji ninaomba nilipokee na tukaone ni nini kimesababisha mpaka sasa Lindi Mjini hawajapata maji, japo hapo awali tulikuwa tumepanga visima hivi vinapelekwa katika Majimbo ya Vijijini ambayo kimkakati ni kuhakikisha kwamba tunaondoa ile gap ya upatikanaji wa huduma ya maji kati ya mjini na vijijini kwa sababu tunaamini mjini kuna miradi mikubwa ambayo inaendelea kutekelezwa ambapo hawatohitaji visima. Kwa hiyo, nitaenda kulitazama kwa kina na nitamshirikisha Mheshimiwa Mbunge ili aweze kuelewa kwamba ni nini kinaendelea. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:- Je, lini ukarabati na upanuzi wa Mradi wa Maji Makonde utakamilika?

Supplementary Question 7

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Wanawake wa Mkoa wa Simiyu tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa shilingi bilioni 440 kwa ajili ya Mradi wa Ziwa Victoria. Wakati mradi huo ukiendelea sasa, Kata ya Budekwa na Kata ya Busilili Wilaya ya Maswa kuna shida sana ya maji. Je, ni lini Serikali itachimba visima virefu katika kata hizo? (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Esther Midimu, Mbunge mahiri wa Mkoa wa Simiyu. Kazi anayoifanya sisi Wanasimiyu tunaifahamu na hakika katika mradi huu ni baadhi ya kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Mbunge ameshiriki kuhakikisha kwamba mradi huu unapatikana na unaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa takribani shilingi bilioni 440 kwa awamu ya kwanza kutoka Nyashimo – Bariadi – Itilima inapita kuanzia kwa Mheshimiwa Simon Songe inaenda Bariadi, inaenda Itilima kwa Mheshimiwa Njalu Silanga. Awamu ya pili tumeishatangaza tender ambapo unaanza kutoka Maswa kwenda upande wa Meatu napo huko kote ni kwa ajili ya neema ambayo Mheshimiwa Rais ameendelea kuiweka kwa Wanasimiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mradi huu utakapopita kwa Sera yetu ya Maji, bomba kubwa likipita kilometa 13 kushoto, kilometa 13 kulia vijiji vyote na maeneo yote yanaweza kupata huduma hiyo ya maji safi na salama. Kwa hiyo nimtoe hofu dada yangu vijiji hivyo na kata hizo iwapo zitakuwa nje ya range hiyo ambayo tumeiweka basi Serikali iko tayari kwenda kuchimba visima ili waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana.