Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ng'wasi Damas Kamani

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELO aliuliza:- Je, sababu zipi zinasababisha Mikopo ya Wanawake kuchelewa kutolewa kwa waliokidhi vigezo vyote, hasa Wanawake wa Mkoa wa Mwanza?

Supplementary Question 1

MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Niendelee kuipongeza Serikali kwa kuendelea kurahisisha utaratibu huu wa kutoa mikopo hii ya vikundi maalum. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza; changamoto hii inayowakuta wanawake wa Mkoa wa Mwanza ya ucheleweshwaji wa kutolewa mikopo pindi wanapotimiza vigezo vyote, ndiyo hasa inawapata vijana kote nchini wanaoomba mikopo hii kupitia halmashauri zetu. Sasa, nini kauli ya Serikali kwa ajili ya kutatua changamoto hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; vijana wengi sana wamehamasika kujiajiri na wanatuma maombi mbalimbali kwenye Halmashauri kupata mikopo hii kwa ajili ya mitaji yao, lakini ni ukweli usiofichika kwamba, fedha hizi hazitoshi kuwahudumia vijana hawa. Sasa, ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha inaendelea kuongeza fedha katika mifuko hii ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Ng’wasi Kamani kwa swali lake lenye nia ya kuwasemea vijana wote nchini. Kuhusiana na swali lake la kwanza, naomba nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuendelea kuwasisitiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri wafuate Kanuni za Utoaji wa Mikopo hii ya 10% inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zinataka ndani ya siku 60 mchakato mzima uwe umekamilika na wale wote wanaokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo hii waweze kupatiwa mikopo hii. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuendelea kutoa msisitizo huo ili kuepusha ucheleweshaji wa utoaji wa mikopo, vijana wetu na wanawake waweze kupata mikopo, watu wenye ulemavu waweze kupata mikopo waende kwenye shughuli zao za uzalishaji mali waweze kujipatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Ng’wasi Kamani, naomba niendelee kuzisisitiza halmashauri zetu ziweze kuendelea kuwa bunifu kuanzisha vyanzo vya mapato kwa tafsiri ya kwamba, vyanzo vya mapato vikiongezeka, mapato ya halmashauri yakiongezeka, hata ile 10% inayotengwa kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu itaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtoe shaka Mheshimiwa Ng’wasi Kamani kwamba, ukiacha tu utaratibu wa kutoa mitaji kupitia Mfuko huu wa 10% ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri, kuna taratibu nyingine ambazo zinawawezesha kimitaji vijana pamoja na makundi mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna mifuko ambayo inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo kuna Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi; kuna Mfuko wa Maendeleo ya Vijana; na pia kuna mifuko ambayo inaratibiwa na Wizara za kisekta, kwa mfano, kwenye madini kuna Mradi unaitwa Mining for Better Tomorrow ambao unawawezesha vijana kupata mikopo kwa ajili ya uwekezaji katika uchimbaji mdogo. Pia, kwenye sekta ya kilimo. Wizara ya Kilimo kuna Mradi wa Building Better Tomorrow ambao unawawezesha vijana kuingia katika sekta ya kilimo na kuwawezesha kimtaji ili waweze kufanya shughuli hizi za uzalishaji mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali kwa ujumla itaendelea na taratibu hizi zote za kuwawezesha vijana kupata mitaji kwa ajili ya kujitengenezea ajira. Namshauri Mheshimiwa Ng’wasi Kamani aendelee kuwahamasisha na kuwaelimisha vijana kwamba, fursa ambazo zimewekwa na Serikali yao makini ya Awamu ya Sita zipo nyingi na waweze kuzitumia fursa hizi ili kuweza kupata mitaji, kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Name

Zaytun Seif Swai

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELO aliuliza:- Je, sababu zipi zinasababisha Mikopo ya Wanawake kuchelewa kutolewa kwa waliokidhi vigezo vyote, hasa Wanawake wa Mkoa wa Mwanza?

Supplementary Question 2

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Je, ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi, hasa wa ngazi za chini kabisa, kwenye kata na vijiji wanapatiwa elimu hii ya mikopo na taarifa ya utoaji wa mikopo ili wengi zaidi waweze kunufaika? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Zaytun Swai kwa swali lake ambalo linalenga kuendelea kuongeza uelewa au kuzungumzia umuhimu wa kuendelea kutoa uelewa zaidi kwa Watanzania kufahamu kuhusiana na fursa mbalimbali za kimitaji zilizopo, hasa katika upande huu wa halmashauri, kupitia 10% ya mapato ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kutumia nafasi hii kuwaomba hata ninyi Waheshimiwa Wabunge tendelee kuwaelimisha, kuwafahamisha na kuwahamasisha wananchi tunaowawakilisha ili wafahamu fursa nzuri ambazo zimewekwa na Serikali yao kwa ajili ya kuwawezesha kimitaji. Upande wa Serikali tunafanya hivyo, pia, tunatoa mafunzo mahususi. Katika kipindi kile cha kuvipitia hivi vikundi huwa kuna mafunzo mahususi kabisa ambayo yanaelezea taratibu na fursa zaidi ambazo wanavikundi wanaweza wakapata kutokea kwenye mikopo hii ya 10% ya mapato ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali tutaendelea kutoa hamasa na kuwajengea elimu na tunafanya hivyo. Tunapita katika vyombo vya habari kuelezea kuhusiana na fursa hizi za mikopo. Pia, nasi Waheshimiwa Wabunge naomba tuungane kwa pamoja kutoa elimu hiyo kwa jamii ili waweze kufahamu fursa mbalimbali ambazo zimewekwa na Serikali yao makini. (Makofi)

Name

Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELO aliuliza:- Je, sababu zipi zinasababisha Mikopo ya Wanawake kuchelewa kutolewa kwa waliokidhi vigezo vyote, hasa Wanawake wa Mkoa wa Mwanza?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, mikopo hii ina kanuni zake na sheria, vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wameshahamasika na kukidhi vigezo vingi, lakini kuna baadhi ya halmashauri hawatoi mikopo hiyo. Je, Serikali inachukua hatua gani kwa Wakurugenzi ambao hawatimizi matakwa ya kanuni hiyo? (Makofi)

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kumpongeza kwanza Mheshimiwa Christina Mnzava kwa swali lake linalolenga kuzungumzia fursa hii ya kimitaji, ambayo inatokana na 10% ya mapato ya ndani katika halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nimhakikishie kwamba hakuna halmashauri ambayo haitoi mikopo hii kwa taarifa tulizonazo kwa wakati huu. Halmashauri zote zina utaratibu kwa sababu, mikopo hii imewekwa kwa mujibu wa sheria. Halmashauri zote zina mapato ya ndani. Halmashauri zote kwenye mapato ya ndani zinatenga 10%, kwa ajili ya mikopo hii kutoa na kuwezesha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kutumia nafasi hii kuendelea kuwasisitiza Wakurugenzi wote katika Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa waendelee kutimiza masharti ya Kisheria na Kikanuni ya utengaji wa fedha hizi na mitaji hii kutoka kwenye mapato yao ya ndani, kwa ajili ya kuendelea kuviwezesha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kimitaji.