Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ritta Enespher Kabati
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: - Je, lini Serikali itawalipa watumishi wastaafu waliopandishwa madaraja kisha hatua hizo kusitishwa?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili. Kwanza naipongeza Serikali kwa majibu ya Waziri. Kwa kuwa kuna baadhi ya watumishi waliokuwa wastaafu ambao tangu tamko hilo la Serikali lilipotolewa mpaka sasa hivi bado halijatekelezwa, je, Serikali sasa inachukua hatua gani kwa wale watekelezaji ambao walitakiwa wawatekelezee hawa wastaafu na hawajafanya hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wapo wastaafu ambao wamestaafu muda mrefu sana, lakini mpaka sasa hivi hawajalipwa nauli zao za kwenda kwao. Je, Serikali inachukua hatua gani?
Name
Deus Clement Sangu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati kwa namna anavyofuatilia masuala yanayowahusu wastaafu. Nataka tu kumhakikishia kwamba Serikali ina nia ya dhati, na ndiyo maana hadi mwaka huu wa fedha tayari wastaafu walioathirika 1,200 walishalipwa fedha zao, takribani shilingi bilioni 2.7.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kupitia Bunge lako, nitoe rai kwa waajiri wote kuhakikisha wanaleta taarifa za hawa wastaafu wanaodai Ofisi ya Rais, Utumishi ili tuweze ku-process madai yao na kupeleka Hazina kwa ajili ya malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wastaafu ambao wamestaafu na nauli zao hazikulipwa; mstaafu anapostaafu ana stahiki yake, na ni taratibu na sheria kwamba alipwe nauli mpaka mahali pale alipokuwa ameajiriwa, kwa maana ya domicile place. Sasa naomba nichukue nafasi hii pia kutoa rai kwa waajiri wote katika taasisi za umma, kwamba kama kuna wastaafu wa aina hii wahakikishe kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha wawe wamelipa wastaafu hao nauli zao kwa sababu ni haki yao. (Makofi)
Name
Esther Nicholus Matiko
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: - Je, lini Serikali itawalipa watumishi wastaafu waliopandishwa madaraja kisha hatua hizo kusitishwa?
Supplementary Question 2
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wastaafu waliokuwa wakifanya kazi Jeshi la Magereza, kuna wengine wamestaafu mwaka 2015, wengine 2019 na wengine 2021, wamekuwa wakidai madai mengi mengi kama vile nauli za safari za kikazi, nauli za uhamisho na zile za kustaafu, lakini mpaka leo hawajalipwa na wamekuwa wakifuatilia muda wote huu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba watu wanapostaafu wachukue interval kidogo tu waweze kulipwa? Maana wanakuwa na database, wanajua kwamba hawa watu wameajiriwa kwenye idara hizo.
Name
Deogratias Francis Ngalawa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ludewa
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza niendelee kumpongeza dada yangu, Mwalimu wangu, Mheshimiwa Matiko kwa namna anavyofuatilia mambo ya askari, hasa Magereza, na amekuwa champion mzuri hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tunalichukua kwa uzito wake. Kwenye mwaka huu wa fedha, tayari tumetenga shilingi bilioni 207 kwa ajili ya kulipa madai haya yote. Kwa hiyo, sisi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tutawasiliana na wenzetu wa mambo ya ndani, tuone namna ya ku-compile haya yote ili hawa wanaodai madai yao yote waweze kulipwa kwa wakati.
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: - Je, lini Serikali itawalipa watumishi wastaafu waliopandishwa madaraja kisha hatua hizo kusitishwa?
Supplementary Question 3
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mimi nipo Kamati ya LAAC, na moja ya changamoto tunazokutana nazo kwenye Kamati hii kwenye halmashauri, mbali ya madai ya wafanyakazi ni pamoja na madai ya wastaafu ambao wamestaafu, hawajalipwa malipo yao, pamoja na malipo mbalimbali ya mizigo. Je, ni lini Serikali itakapohakikisha wanaziagiza halmashauri ziwe zinalipa wastaafu kwa wakati?
Name
Deus Clement Sangu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, na pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Ester Bulaya, amekuwa akipigania jambo hili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyosema hapa kwamba tayari tarehe 30 mwezi wa Nne tulitoa Mwongozo na Waraka kuzitaka mamlaka zote za waajiri kuhakikisha madai ya wastaafu yanalipwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa jambo la kustaafu siyo dharura, ni jambo ambalo lipo kisheria. Kwa hiyo, niendelee tena kusisitiza kupitia Bunge hili, ule Waraka na Mwongozo tuliotoa kuwakumbusha waajiri wote waweze kuuzingatia.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved