Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Primary Question

MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza maji Kata za Kaboha, Shabaka, Nyang’hwale, Nyaburanda, Mwingiro, Nyugwa ili kuondoa shida ya maji?

Supplementary Question 1

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali kwa baadhi ya kata ambazo amezitaja Kaboha, Shabaka, Nyang’hwale, Nyaburanda, Mwingiro na Nyugwa kwa kuendelea kusambaza maji kupitia visima virefu tisa na visima saba vya pampu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa tumepitisha Bajeti ya Wizara ya Maji na kutengewa fedha juzi kwa ajili ya kwenda kusambaza maji kupitia Mradi wa JWPP, je, Serikali iko tayari kupeleka wakandarasi kwenye kila kata baada ya fedha hizo kutoka ili waweze kuifanya kazi hiyo kwa haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nataka kujua, Mfuko wa Maji mgawanyo wake ukoje kati ya mjini na vijijini? Ahsante. (Makofi)

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natumia fursa hii kumpongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Hussein Nassor, Mbunge wa Nyang’hwale kwa kazi nzuri ya kuwatetea wananchi wa Nyang’hwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana naye kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto za huduma ya maji katika Jimbo la Nyang’hwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameshauri na tumeupokea ushauri wake. Sambamba na hilo, tutafanya tathmini ili kuona kama kutakuwa na uhitaji wa kupeleka wakandarasi wengi katika eneo hilo. Lengo ni kwamba, mradi uweze kukamilika kwa wakati. Tutafanya hivyo kwa kuzingatia mapana yote hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Maji ambao unafanya kazi chini ya Sheria ya Usambazaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya Mwaka 2019, mgawanyo wa fedha hizi upo kikanuni. Tuna kanuni ambazo Mheshimiwa Waziri wa Maji alishasaini ambapo inaonesha kabisa kwamba tutakuwa na 60% ambayo itaenda kwa ajili ya vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa na 29% ambayo itaenda kwa ajili ya mjini na tutakuwa na 10% kwa ajili ya kulinda vyanzo vyetu vya maji. Vilevile, tutakuwa na asilimia moja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata vifaa kwa ajili ya kupima ubora wa maji ili maji yatakayowafikia wananchi yawafikie katika ubora unaotakiwa. (Makofi)