Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Primary Question

MHE. COSTANTINE J. KANYASU aliuliza:- Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kupitia mtandao wa Twitter alitangaza kuzuia timu yoyote katika kundi „Cā€Ÿ la Ligi Daraja la Kwanza kupanda daraja kabla ya mechi zao kukamilika na kabla ya vikao halali vya uchaguzi kufanyika:- Je, Serikali haioni kwamba, maamuzi yalifanywa kinadharia na uonevu mkubwa kwa Timu ya Geita Gold Sport?

Supplementary Question 1

MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nakubaliana na agizo la Serikali kwenye sentensi nne za jibu lake za mwisho, lakini sikubaliani kabisa na majibu aliyoyatoa na sababu za msingi ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Mpira kabla ya adhabu yoyote kutolewa Chama cha Mpira (TFF) kinasubiri taarifa ya Refa na taarifa ya Kamishna au Msimamizi wa Mechi. Taarifa hizo mpaka wakati Rais wa TFF ana-twit, dakika ya 80 mechi inaendelea, alikuwa hana mezani, ni wakati gani Waziri ananiambia Rais huyu alitumia Kanuni? (Makofi)
Swali langu la pili; baada ya adhabu hii baadhi ya wanamichezo wamefungiwa maisha kwa tuhuma kwamba, palikuwa na makosa ya rushwa ambayo ni makosa ya jinai. Tunavyo vyombo ambavyo vinachunguza rushwa na ni kosa la jinai, ni uchunguzi gani ambao vyombo vya jinai vilitoa kwa sababu vilipewa agizo la kuchunguza suala hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Kanyasu kwa jinsi ambavyo anajitahidi kutetea timu yake ya Geita Gold Sports.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alitaka kujua wakati ambao vikao hivi vilikaa, swali la kwanza hilo. Kama nilivyosema katika jibu la msingi vikao hivi vilikaa baada ya kupata malalamiko kutoka timu za Kundi ā€žCā€Ÿ na ndipo vikao vikakaa, lakini Rais wa TFF alichukua tahadhari, sio kwamba, alitoa maamuzi, alikuwa anatoa tahadhari. Vikao vilivyofanya maamuzi ni vile ambavyo vilikaa baada ya kupata malalamiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lake la pili ni kwamba, ni ruksa kwa mtu binafsi au taasisi au timu kukata rufaa kwa kutumia taratibu ambazo zipo. Ahsante.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Costantine John Kanyasu Mbunge wa Geita, naongezea katika majibu ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya kwanza, kama alivyosema Naibu Waziri, maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Mbunge na tuliwahi kuyatoa hapa Bungeni, tukasema wale ambao hawakuridhika na uamuzi uliofanywa na TFF, TFF uamuzi wao siyo wa mwisho, wafuate taratibu na watumie hayo ambayo wanaona ni upungufu katika uamuzi uliofanyika kukata rufaa. Sehemu ya kwanza hii, watumie nafasi hiyo wakate rufaa na Serikali tutasimamia haki yao ipatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, ni kweli katika mchakato huu kuna tuhuma nyingi za rushwa na niliwahi kusema hapa Bungeni, tuhuma zile waliotuhumiwa sio wadogo wa chini peke yake ni pamoja na wa katika mhimili wenyewe unaosimamia soka. Hivi tunavyoongea chombo ambacho kinahusika na suala la rushwa, TAKUKURU wanakamilisha kazi yao ya uchunguzi, wakikamilisha na kama kutakuwa na watu watabainika kuhusika na rushwa hatua za Kisheria zitachukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni kuthibitisha kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kufuta suala la rushwa kwenye michezo kwa sababu linatafuna na kuharibu michezo yetu.

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSTANTINE J. KANYASU aliuliza:- Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kupitia mtandao wa Twitter alitangaza kuzuia timu yoyote katika kundi „Cā€Ÿ la Ligi Daraja la Kwanza kupanda daraja kabla ya mechi zao kukamilika na kabla ya vikao halali vya uchaguzi kufanyika:- Je, Serikali haioni kwamba, maamuzi yalifanywa kinadharia na uonevu mkubwa kwa Timu ya Geita Gold Sport?

Supplementary Question 2

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Nami ni mdau mkubwa wa michezo na hasa mchezo wa soka. Mchezo wa soka ni mchezo unaopendwa nadhani kuliko mchezo wowote duniani na ni mchezo ambao unaweza kutumika kuwa kiunganishi muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kulikuwa na tuhuma za rushwa katika suala hili kwa kuwa, mchezo huu ni kipenzi cha watu wengi, je, Waziri anaweza kuliambia Bunge hili kwamba, ni lini sasa uchunguzi huu utafika mwisho na wahusika kuchukuliwa hatua ambazo zinatakiwa kuchukuliwa? Ahsante sana.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema TAKUKURU wanakamilisha utaratibu. Wakati mwingine uchunguzi wa makosa hasa ya rushwa ambayo kwa namna moja ama nyingine wahusika wa pande mbili wanakuwa wamekubaliana huwa yanaweza yakachukua muda mrefu na wakati mwingine kupata uhalisia wake inakuwa ngumu, lakini habari nilizonazo ni kwamba, TAKUKURU wako hatua za mwisho za kukamilisha uchunguzi huo na baada ya kukamilisha uchunguzi huo, hatua zinazostahiki zitachukuliwa.