Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Salma Mohamed Mwassa
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SALMA M. MWASSA aliuliza:- Je, ni nini umuhimu wa kuwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya katika nchi hii?
Supplementary Question 1
MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Spika ahsante. Pamoja na majibu ya kuleta matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika Sheria hii ya Mabaraza ya Ardhi inasema kwamba; Baraza la Ardhi la Wilaya lisiongelee kesi inayozidi au kiwanja kinachozidi thamani ya shilingi milioni 50, na Baraza la Nyumba la Kata lisiongelee kiwanja au nyumba inayozidi shilingi milioni tatu.
Meshimiwa Spika, kwa mikoa kama Dar es Salaam, Mwanza, maeneo yoye ya mijini Nyumba nyingi zimezidi thamani ya shilingi milioni 50. Sasa kutokana na sheria hii kutokukidhi matakwa halisi ya mwenendo wa thamani ya ardhi iliyopo mijini kwa sasa, ni lini sheria hii itarekebishwa au iletwe hapa Bungeni irekebishwe au ifanyiwe amendment ili iendane na hali halisi ya sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, migogoro mingi ya ardhi ya ardhi nchini inasababishwa na ardhi kutopimwa na kumilikishwa kwa ufasaha, na hii inasababishwa na gharama kubwa na mlundikano wa kodi ya umilikaji wa ardhi kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano kodi ya premium katika umilikaji wa ardhi ambayo ni asilimia 7.5 ni kubwa mno kwa sasa, ni lini kodi hii itashushwa au itafutwa ili kuwaletea tija wananchi au kuwapunguzia mzigo wananchi katika kupata haki yao hii ya kumiliki ardhi kwa sasa? Ahsante.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anazungumzia sheria kutokidhi kwa mana ya kwamba viwango vilivyopo kwa sasa na hasa mijini ukiangalia kwa Mabaraza ya ardhi kiwango chake ni shilingi milioni 50 lakini nyumba nyingi zimezidi.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu haya masuala yanakwenda kisheria, na kama hitaji linaonekana kwamba sheria imepitwa na wakati nadhani ni wakati muafaka pengine wa kuweza kupitia upya na kuweza kuangalia kwasababu kadri siku zinavyokwenda ndivyo jinsi na majengo yana-appreciate value zake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ni wazi kweli anavyolisema limepitwa na wakati, lakini bado pale inapoonekana kwamba viwango, au kiwango cha kesi husika kinazidi Mamlaka ya Baraza husika kesi hiyo huwa inapelekwa kwenye mahakama ya juu. Kwa hiyo bado linaweza kufanyika wakati bado tunasubiri kubadilisha sheria hii.
Mheshimiwa Spika, suala la pili ni suala la viwango. Tukumbuke katika bajeti nadhani ya mwaka 2015/2016 kiwango cha premium kilishuka kutoka asilimia 15 kwenda kwenye asilimia 7.5. Sasa tuna miaka kama miwili tu toka hii imeanza kutumika na bado inaonekana ni kubwa. Lakini tukumbuke pia kwamba viwango vingi vya ardhi ambavyo vilikuwepo vilishushwa ikiwepo hata ile ya upimaji wa ardhi kwa kiwanja kutoka shilingi 800,000 kwenda shilingi 300,000. Kwa hiyo, haya yote ni mapitio yanayofanyika kulingana na muda jinsi ulivyo.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu hili nalo bado linaonekana ni tatizo siwezi kuahidi hapa ni lini tutaleta sheria hiyo kwa sababu ndiyo kwanza imeanza. Lakini tutazidi kufanya utafiti wa kina na kuweza kujua kama kweli ni kikwazo kikubwa tuweze kuona namna gani tutapitia tena viwango vyetu ili wananchi ambao tunategemea wanufaika wa ardhi hii ambayo sehemu kubwa haijapimwa waweze kunufaika na kupata ardhi zao na kuweza kupata hati ili waweze kufanya shughuli zingine za maendeleo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved