Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Primary Question
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:- Ushirika katika Wilaya ya Siha umekumbwa na matukio ya ufisadi yakiwemo upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 840 katika Ushirika wa Siha Kiyeyu, upotevu wa shilingi milioni 337 ya SACCOS ya Sanya Juu pamoja na matumizi mabaya ya ardhi, licha ya uchunguzi mzuri uliofanywa na TAKUKURU Mkoa:- Je, ni kwa nini uchunguzi huo unaingiliwa na maslahi binafsi ya watu wachache na kusababisha matukio yanayodhalilisha Serikali?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kushukuru Wizara ya Kilimo, vilevile kumshukuru Rais. Nimemweleza hili, nimeona cheche kidogo. Niseme, kwa kuwa tumeshamkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Siha na amewekwa ndani kwa muda kwa ajilii ya tuhuma kama hizi za ufisadi, lakini sh. 1,600,000/= ambazo zimeshushwa siyo za kweli. Amesharudisha ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Charles Mlingwa na risiti tunazo. Tulimtafuta tukamkamate, lakini tukakuta amezungukwa na Jeshi la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kuwa Mkuu Mkoa wa Kilimanjaro Meck Sadiq amemtishia Meneja wa TAKUKURU wa Mkoa wa Kilimanjaro, kwamba hizi tuhuma anazozichunguza ni za uongo, swali langu la kwanza ni kwamba. Je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha watuhumiwa wote wa ufisadi ndani ya ushirika na KNCU Mkoa wa Kilimanjaro, wamefikishwa mbele ya sheria; na kutuhakikishia watamlindaje Mkuu wa TAKUKURU anayezuiliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kufanya kazi zake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali inatupa commitment gani kwamba Charles Mlingwa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, vilevile Meck Sadiq ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, bado wanastahili kupeperusha bendera ya Tanzania na vilevile kupigiwa saluti na majeshi yetu ya Tanzania kama Wakuu wa Mikoa na kumwakilisha Rais baada ya vitendo hivi?
Name
Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusiana na swali lake la kwanza, kwamba Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha kwamba watuhumiwa wanafikishwa Mahakamani au wanafunguliwa mashtaka? Nimhakikishie kwamba tunaendelea na chunguzi mbalimbali na pindi chunguzi hizo zitakapokamilika na itakapothibitika pasipo shaka kwamba wanayo hatia au wana hoja ya kujibu Mahakamani, basi kwa hakika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, kwa swali la pili kwamba Afisa wa TAKUKURU wa Mkoa anaingiliwa ama anazuiwa kufanya kazi zake na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, niseme kwamba siyo kweli. Ukiangalia kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, TAKUKURU kama chombo, kinao uhuru wa kufanya kazi zake bila kuingiliwa na imekuwa ikifanya hivyo. Hata katika jibu la msingi nilieleza, tayari kulikuwa kuna mkutano wa wanaushirika, tena Mheshimiwa Meck Sadiq huyo huyo aliitisha na waliweza kusomewa taarifa ya TAKUKURU pale na aliweza kuridhika na ndiyo maana mpaka leo kunakuwa na utulivu na uhimilivu katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, endapo ataona ana malalamiko dhidi ya Wakuu wa Mikoa hao, basi asisite kuwasilisha malalamiko stahiki na aweze kuchukuliwa hatua.
Name
Freeman Aikaeli Mbowe
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL aliuliza:- Ushirika katika Wilaya ya Siha umekumbwa na matukio ya ufisadi yakiwemo upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 840 katika Ushirika wa Siha Kiyeyu, upotevu wa shilingi milioni 337 ya SACCOS ya Sanya Juu pamoja na matumizi mabaya ya ardhi, licha ya uchunguzi mzuri uliofanywa na TAKUKURU Mkoa:- Je, ni kwa nini uchunguzi huo unaingiliwa na maslahi binafsi ya watu wachache na kusababisha matukio yanayodhalilisha Serikali?
Supplementary Question 2
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo ya vyama vya msingi vya ushirika katika Wilaya ya Siha, yanafanana sana na matatizo ya Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Wilaya ya Hai; na kwa sababu Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Mkoa wa Kilimanjaro vimehodhi maeneo makubwa sana ya ardhi, ambayo kimsingi kwa Mkoa wa Kilimanjaro ndiyo backbone ya economy ya Mkoa ule kwenye upande wa kilimo; na kwa kuwa kumekuwa na shutuma nyingi za muda mrefu ambazo pengine zimelindwa kwa kiwango kikubwa na sheria yenyewe ya ushirika, ambayo inatoa limited power kwa mtu mwingine yeyote kuingilia vitendo na kazi za ushirika:-
Je, Serikali haioni sasa kwa sababu ya matatizo haya ya muda mrefu yaliyokithiri, ni wakati muafaka wa ku-review Sheria ya Ushirika; na kabla ya kui-review Sheria ya Ushirika, kuangalia kwa kina matatizo ya Vyama vya Msingi vya Ushirika katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kuweza sasa kuweka mapendekezo sahihi ya kurekebisha sheria ile?
Name
Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kuhusiana na kufanya mapitio katika Sheria ya Ushirika, Wizara ya Kilimo bahati nzuri wapo. Niseme tu kama Serikali tumekuwa tukifanya hivyo kwa sheria mbalimbali siyo hii tu ya ushirika; na naamini Wizara husika itaweza kulichukua na nina uhakika watakuwa wameshaanza mapitio kwa sababu ni suala endelevu kila mara kungalia sheria inakidhi mahitaji ya wakati husika.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Serikali kuviangalia Vyama hivi vya Ushirika kama vina matatizo, napenda tu kusema kwamba katika Mkoa wa Kilimanjaro hata hivi sasa tunavyoongea tayari Vyama vya Ushirika vinne vimefanyiwa uchunguzi na tayari vyama vitatu uchunguzi umeshakamilika, kimebakia kimoja. Naamini matokeo ya uchunguzi hayo yataweza kutangazwa huko baadaye ili kuona ni hatua gani iweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, vile vile tumeshafanya uchunguzi katika Chama Kikuu cha Ushirika cha KNCU na tumefanya uchunguzi katika Chama cha Tanganyika Coffee Curing CompanyLimited na siyo kwa Vyama hivi vya Ushirika peke yake. Tumefanya pia uchunguzi katika SACCOS nne na tayari mbili zimeshafikishwa Mahakamani na mbili zinaendelea na uchunguzi.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbowe, kwa kutambua umuhimu wa Vyama hivi vya Ushirika kwa wakulima, tutakapoona kuna harufu au chochote kinachoashiria vitendo vya rushwa au vitendo vingine vya ubadhirifu wa mali za umma, tutahakikisha kwamba hatua stahiki zinachukuliwa.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved