Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:- Kati ya mwaka 1954 na 1957 kulifanyika zoezi la upimaji wa maeneo ya Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba na Hifadhi katika Wilaya ya Sikonge ambapo kulikuwa na wakazi takribani 16,000 na ng’ombe wapatao 2500. Kwa sasa wakazi wameongezeka hadi kufikia takribani 300,000 na ng’ombe wapo takribani 200,000 lakini eneo la kuishi, kulima na malisho ya mifugo na shughuli nyingine za kiuchumi ni lile lile la asilimia 3.7 ya eneo lote la Wilaya huku eneo la Hifadhi likibaki asilimia 96.3 na hali hii inasababisha migogoro kati ya wakulima, wafugaji na warina asali dhidi ya Maafisa Maliasili. (a) Je, ni lini Serikali itawaongezea wakazi wa Wilaya ya Sikonge eneo la kuisha, kulima na kulishia mifugo kutoka asilimia 3.7 hadi angalau asilimia 25 ya eneo lote la Wilaya? (b) Je, Serikali haioni kuwa kuongeza eneo la Wilaya hiyo kwa asilimia 25 kutaepusha migogoro iliyopo sasa na hivyo wananchi watatekeleza shughuli zao kwa amani na utulivu huku wakilinda mazingira pamoja na hifadhi?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kunipa nafasi. Niseme wazi kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza kwamba wananchi wa Sikonge wemesikitishwa sana na majibu ya Serikali. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kutumia takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) za mwaka 2012 kama zilivyo ni sahihi, lakini je, Serikali haioni kuwa kutumia takwimu hizo bila kufanya projections kwa kutumia formular rasmi iliyo kwenye taarifa ya uchambuzi ya NBS inaweza kusababisha takwimu zisizo sahihi kwa mwaka 2017 na hivyo kusababisha Bunge hili pamoja na wananchi kuamini kuwa Serikali imelidanganya Bunge pamoja na wananchi? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa takwimu rasmi zilizoko kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Sikonge pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ambazo pia ndizo alizonazo Mkuu wa Idara ya Maliasili wa Halmashauri inaonyesha kwamba kati ya kilometa za mraba 27,873 za Wilaya ya Sikonge, kilometa za mraba 26,834 ambayo ni sawa sawa na asilimia 96.3 ni hifadhi za misitu, wanyamapori, mapori ya akiba na maeneo mengine ya hifadhi ambayo yote hayo yako chini ya udhibiti na dhamana ya Kisheria ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Je, wananchi tumebaki na kilometa za mraba elfu moja na thelathini na...
…hili la pili, Serikali itateua lini timu yake ije kufanya kazi na timu yetu Sikonge, ili kusudi tupate suluhisho la kudumu kuhusu takwimu hizo?

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, takwimu huwa zina chanzo, na mara nyingi unapokuwa unataka kunukuu takwimu ni lazima useme chanzo cha takwimu hizo yaani hizo takwimu ni kwa mujibu wa nani aliyezifanya. Takwimu zina mwenyewe na mwenye takwimu ni lazima awe ni mtu mwenye mamlaka na kwa Taifa hili takwimu ni mali ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, takwimu nilizozitumia kwa kuwa ni za Mtakwimu Mkuu wa Serikali sina shaka kwamba takwimu hizi ni sahihi na hizi ndizo takwimu zinazotakiwa kutumika
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kufanya projections kwamba ilitakiwa kuzitoa kutoka mwaka 2012 kuzileta leo, hiyo inaweza kuwa ni hoja, lakini ingekuwa ni hoja tu kama kweli hoja ya takwimu ingekuwa ni ya msingi kutokana na swali la msingi lililoulizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ifahamike kabisa kwamba nchi yetu ndio nchi inayoongoza duniani kwa kuwa na eneo kubwa lililotengwa kwa ajili ya uhifadhi kwa ajili ya wanyamapori, misitu na hifadhi nyingine. Sisi tumetenga asilimia 25 ya eneo zima la nchi yetu, hiyo inatosha kutuma ujumbe kwamba ni kweli tumehifadhi maeneo makubwa. Lakini hatukufanya hivyo kwa makosa, tulifanya hivyo kwa sababu za msingi ambazo ndio zimekuwa zikitupa faida nyingi sana zinazotokana na uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tunapozungumzia uhifadhi kwenye eneo la Sikonge ifahamike kabisa kwamba uhifadhi huo sio kwa ajili ya Sikonge. Kila eneo lililohifadhiwa hapa nchini limehifadhiwa kwa maslahi ya Taifa. Eneo hilo litaweza kupitiwa pale ambapo kama Taifa tutaona kwamba kweli kuna haja ya kufanya mapitio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimuombe Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kumpongeza kwamba yuko hodari wa kufuatilia masuala yanayohusu wananchi wake, na yeye atakumbuka vizuri kabisa kwamba mwanzoni mwa mwaka huu tulikuwa wote Sikonge, tumepita kwenye maeneo yake, nami napenda wananchi wa Sikonge wajue kabisa kwamba wanao jembe, Mbunge wao ni mfuatiliaji sana wa masuala yanayohusu wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huo huo nataka nimuombe kwamba atumie fursa hiyo ya kuwakilisha wananchi kwa kuwaambia ukweli kwamba akiba ni akiba na tunatakiwa kuyahifadhi maeneo yale kama akiba. Tutaweza kuyatumia pale tu itakapotokea kwamba kuna ulazima wa kuweza kufanya vinginevyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Serikali kuteua timu, nirudie tu kwamba tayari timu ipo na iko kazini na inaendelea na kazi hiyo, kinachosubiriwa sasa hivi ni wao na ile kazi yao kukamilika na kuweza kuleta mrejesho Serikalini kwa ajili ya kuweza kupiga hatua kutekeleza masuala haya yanayohusiana na upitiaji upya wa kile ambacho tunacho hivi sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho kabisa niseme kwamba kamwe Serikali haitaweza kufikia mahali ikaamua tu haraka haraka kuweza kuyaondoa maeneo yaliyohifadhiwa kwa matumizi mengine bila kufanya tathmini ya kuangalia kwamba maeneo yasiyohifadhiwa yametumika kwa tija. Kwa hiyo, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba maeneo ambayo hatujahifadhi yanatumika kwa tija kwanza ndipo tuanze kugusa maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa ajili ya akiba ya Taifa hili kwa ajili ya kizazi kijacho.