Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Je, ni lini Mahakama zote nchini zitaanza kuendesha kesi kwa lugha ya Kiswahili?

Supplementary Question 1

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake, naomba kuuliza maswali tu madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa jibu katika swali langu la msingi linakiri kuwa kumbukumbu na hukumu katika Mahakama za Wilaya hadi Mahakama ya Rufani ni kwa Kiingereza. Je, Serikali haioni kuwa kumbukumbu na hukumu katika lugha ya kigeni yaani Kiingereza ni kikwazo kikubwa kwa mwananchi anayetaka kukata rufaa kwa kupata haki yake?
Swali la pili, kwa kuwa kauli mbiu ya Serikali ni haki sawa kwa wote na kwa wakati, lakini tumekuwa tukishuhudia Mahakama zikijitahidi kumaliza kesi zake, lakini hukumu zinakuwa zinapatikana kwa kuchelewa sana, hali inayopelekea wengine kutokukata rufaa kwa wakati na walioko gerezani kuendelea kuteseka gerezani.
Je, Serikali inatoa kauli gani? (Makofi)

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kukubaliana na Mheshimiwa Ritta Kabati kwamba ana hoja ya msingi, lakini nikumbushe tu Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tuliamua mwaka 1964 kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa, vilevile Kiingereza kuwa lugha ambayo tunaitumia katika shughuli za Serikali. Ni kama Mheshimiwa Baba wa Taifa alivyosema kwamba Kiingereza ndiyo Kiswahili cha dunia.
Kutoka 1964 mpaka sasa tumeweza kufanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha kwamba tunakiingiza Kiswahili katika mfumo wa Mahakama bila kupotosha utoaji haki.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni suala la utumiaji wa Kiswahili kwa kumbukumbu, kwa hukumu, kwa uendeshaji katika Mahakama za Mwanzo ambao umefanikiwa sana. Hatujaona kabisa miscarriage of justice pale.
Mheshimiwa Spika, pili Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ambayo mwanzoni ilikuwa inaitwa TUKI (Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili) chini ya Profesa Mlacha, iliweza kushirikisha Baraza la Kiswahili la Tanzania pamoja na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa Sheria, nilikuwepo mimi pamoja na Marehemu Profesa Joan Mwaikyusa, Mungu aiweke roho yake pema, peponi, tukaweza kutoa Kamusi ya kwanza ya Kiswahili ya Kisheria, yote haya ni maandalizi.
Mheshimiwa Spika, tatu, kila Muswada wa Sheria leo hii ukiletwa hapa Bungeni na sheria zenyewe, lazima ije kwa Kiingereza na Kiswahili na hilo wewe mwenyewe umekuwa ukisisitiza sana.
Mwisho BAKITA imeshakusanya sasa hivi Istilahi zaidi ya 200 za kisheria ambazo zinasubiri tu kusanifishwa (standardize). Kwa msingi huo, Mahakama yetu ambayo ni chombo huru katika Katiba yetu ni Muhimili unaojitegemea, una msingi sawa wa kutosha tuweze kupanua wigo wa matumizi ya Kiswahili katika kumbukumbu na hata kutoa hukumu hata kwenda Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi kwa kuanzia.
Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Kabati kwamba tunachoepusha hapa ni kukurupuka tu kuingia na kutumia Kiswahili ilikuwa tu ni kuepusha utata katika nyaraka zetu, ambiguities na kuwa equivocal, kuwa na utata katika utafsiri nyaraka za Kimahakama, ndiyo maana tumekwenda polepole sana.
Mheshimiwa Spika, suala la pili, nakubaliana naye kwa kweli haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa, lakini ni kweli vilevile kuwa haki iliyowahishwa sana mara nyingi hukosa umakini. Kesi nyingi zinachelewa hasa za jinai kumalizika si kwa sababu ya Mahakama lakini kutokana na mchakato mzima wa utoaji haki. Kwa mfano, suala la upelelezi huchukua muda mrefu sana, na inachukua muda mrefu si kwa sababu vyombo vyetu vya dola havifanyi kazi, lakini kuna tatizo la kutopata ushirikiano mzuri kwa mashahidi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Iringa anakotoka Mheshimiwa Kabati, tuna kesi nyingi sana, sana za makosa ya kujamiiana na yanatokea ndani ya familia, kupata ushahidi mle ndani ni kazi kubwa kweli na ndiyo maana tunatoa wito kwa wananchi wote kushirikiana na vyombo vya dola pale inapotokea kosa, kusaidia katika ushahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kwamba, uthibitisho wa makosa mengine unahitaji Mkemia Mkuu achunguze na atoe jibu, inachukua muda mrefu, Mkemia Mkuu anaweza kuwa na mafaili 3000 ya uchunguzi na yote yanahitaji kwenda Mahakamani, kwa hiyo kazi ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na la mwisho ni uhitaji wa kisheria kwamba kila kosa lazima lithibitishwe beyond reasonable doubt yaani pasipo na wasiwasi wowote. Sasa hiyo hatuwezi kulikwepa ili kuweza kulinda haki za kila mtu.

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Je, ni lini Mahakama zote nchini zitaanza kuendesha kesi kwa lugha ya Kiswahili?

Supplementary Question 2

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwenye Kijiji cha Mnara, Kata ya Mnara, Tarafa ya Rondo Jimboni Mtama kwa kupindi cha miaka mitatu sasa imepita tumekamilisha jengo zuri la kisasa la Mahakama, lakini kwa kipindi chote hicho Serikali imekuwa kwa namna moja ama nyingine pengine inapiga chenga kufungua na kuruhusu jengo hili litumike.
Mheshimiwa Spika, Mbunge aliyepita alisaidia ujenzi, ameomba Serikali tulifungue, lakini mpaka leo Serikali haijafungua. Sasa ni lini Mheshimiwa Waziri Serikali itaruhusu jengo hili litumike ili haki itendeke kwa watu wangu hawa kupata huduma karibu na maeneo yao.

Name

Dr. Harrison George Mwakyembe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Answer

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana yeye pamoja na wananchi wa Jimbo lake kwa kupata jengo la Mahakama zuri, lakini mimi mwenyewe nasikitika kwamba mpaka sasa halijaweza kuzinduliwa.
Naomba nitoe ahadi kwamba tutakapotoka tu hapa, tena nataka niwe mbele yake, nitampigia Mtendaji Mkuu wa Mahakama, tuhakikishe kweli hili jengo linaanza kutumika. Kwa sababu huko ndiko kusogeza huduma za Mahakama kwa wananchi. (Makofi)