Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Primary Question

MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:- • Je, Serikali kupitia REA III ina mpango gani wa kusambaza umeme katika kata zilizobaki Wilayani Nachingwea? • Je, nini mpango wa Serikali kutatua tatizo la kukatikakatika kwa umeme Wilayani Nachingwea?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, nilikuwa naomba kupata ufafanuzi katika maeneo mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, ni takribani miezi minne sasa imepita toka Mkataba wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu usainiwe pale Chinongwe, lakini mpaka leo nazungumza, pamoja na majibu aliyoyatoa, kazi kubwa iliyofanyika ni kuweka tu vijiti. Sasa nilikuwa nataka kujua Serikali imekwama wapi kutoa fedha mpaka sasa hivi kwa ajili ya kuanza kazi hii ya kusambaza umeme vijijini?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nilikuwa naomba nimuulize Naibu Waziri, pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme pale Mahumbika ambacho tuliamini kingekuwa ni tiba kwa tatizo la kukatika umeme kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Ni jitihada gani za makusudi au za dharura ambazo Serikali itakwenda kuchukua, ili kuwaondoa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara gizani, ukizingatia maagizo ya kufunga mashine yalishatolewa na Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Mkoani Mtwara na aliwapa siku kumi, mpaka leo bado hakuna kilichotekelezwa, naomba kufahamu nini kinaendelea?

Name

Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ni kweli wakandarasi wa REA walishaanza kazi kama anavyosema miezi minne iliyopita na ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge pamoja n Bunge lako Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) wameshalipa kiasi cha takribani bilioni 28 kwa wakandarasi wote kama advance. Nimeongea pia na Mkandarasi wa Mkoa wa Lindi ambaye ni State Grid, yupo anafanya kazi na alikuwa katika Wilaya ya Ruangwa na kati ya vijiji 34 alikuwa amevifikia vijiji 19 mpaka jana na akitoka Ruangwa ataelekea Wilaya ya Nachingwea. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kweli Serikali imedhamiria kabisa kwamba vijiji vyote vilivyosalia na kwa awamu hii ya kwanza ni vijiji 3,559 mpaka 2019 umeme vitakuwa vimepeta.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili aliuliza namna gani Serikali inachukua jitihada kumaliza tatizo la umeme Mikoa ya Mtwara na Lindi. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, mkandarasi anayefanya matengenezo ya mashine tisa za kuzalisha umeme Mkoa wa Mtwara ameanza hizo kazi. Vipuri vimewasili kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alielekeza na kazi inaendelea. Na mpaka jana mashine sita zenye uwezo wa kuzalisha megawati 12 zilikuwa zinafanya kazi, lakini pia Serikali imechukua hatua imeagiza mashine mbili mpya kwa ajili ya kuzalisha megawati nne kwa thamani ya bilioni nane ambazo zitafika mwakani mwezi wa tatu na zitakuwa zimefungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia Serikali kupitia TANESCO inafanya matengenezo ya mtambo wa kuzalisha umeme Somangafungu ambao unazalisha megawati 7.5. Tuna uhakika, naomba niwathibitishie wakazi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi itakapofika Disemba, 31 hali ya upatikanaji umeme Mtwara na Lindi itaboreka. Ahsante sana. (Makofi)