Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. AIDA J. KHENAN (k.n.y MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA) aliuliza (a) Je, kuna sheria yoyote ya nchi inayomruhusu askari polisi kumkatamata mtuhumiwa, kumpiga na kumtesa kabla hajajua kosa lake na kabla ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi? (b) Je, Serikali inachukua hatua zipi za kuhakikisha kuwa askari wanaofanya vitendo kama hivyo wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi? (c) Je, mpaka sasa ni askari wangapi wameshachukuliwa hatua za kisheria kutokana na makosa ya kujichukulia hatua mkononi?
Supplementary Question 1
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu, anasema ni askari 105 ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu. Katika matukio ambayo yametokea ambayo hayana shaka, ni matukio ya wazi, ni matukio ambayo yametokea kwa Mheshimiwa Nape Nnauye ya kutolea bastola hadharani lakini pia Mdude Nyangali ambaye amepigwa mpaka sasa hawezi kutembea vizuri, Husna Amri ni kiongozi wetu wa CHADEMA ambaye amefanyiwa hicho kitendo mpaka sasa hivi tuko hospitali. Je, katika hao askari ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu ni miongoni mwa hao 105?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna askari ambao umekiri kwamba wamechukuliwa hatua za kinidhamu na hawa watu wanaoteswa wengine hawawezi tena kuendelea na shughuli zozote, wanapata fidia gani kulingana na madhara ambayo wamekuwa wameyapata? (Makofi)
Name
Eng. Hamad Yussuf Masauni
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa naibu Spika, swali lake ameuliza kwa kutoa mifano michache ya baadhi ya watu ambao walipata majeraha mbalimbali, lakini naomba nichukue fursa hii kutoa ufafanuzi kidogo wa majibu ya swali hili, nadhani itasaidia kuweza kutoa uelewa mpana wa utaratibu wa jinsi ambavyo polisi wanafanya shughuli zao wanapokabiliana na changamoto ya uvunjifu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba ukamataji nchini unasimamiwa chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu namba 11 ambacho kinaeleza kwamba polisi anapaswa atumie njia ya kumshika muhusika (physical contact) pale tu ikiwa yule mtuhumiwa amegoma. Katika hali ya kawaida ni kwamba polisi wanapohitaji kumkamata mtuhumiwa inamueleza na watuhumiwa ambao wanafuata sheria bila shuruti huwa polisi hawana haja ya kuwashika au kuwakamata kwa kutumia mikono yao. Hii inadhihirishwa na hata Waheshimiwa Wabunge huwa ni mashahidi mara nyingi, wakiwemo viongozi ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa mambo mbalimbali wanapelekewa taarifa kwa njia ya simu au hata kwa barua waweze kujisalimisha wenyewe polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia ya pili ni ambayo sheria hii inaainisha ni kwamba endapo mtu huyo atakuwa amebisha, basi polisi wataweza kutumia njia yoyote ambayo ni stahiki kuweza kumkamata mtuhumiwa, kwa kiingereza wanasema; “may use all means necessary to effect the arrest.”
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hivi ndivyo ilivyoandikwa katika Sheria yenyewe ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Hata hivyo, hata hii nayo imefafanuliwa katika PGO namba 274 ambayo inaeleza utaratibu wenyewe hata wa kukamata ukoje na unazingatia mambo mengi. Kwa mfano, unaweza ukaangalia aina ya tishio kwamba je, madhumuni ya mtu huyu ni yapi na mazingira ambayo yanahusisha mtuhumiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengine mengi ambayo yanaangaliwa miongoni mwayo wanaangalia vilevile, kwa mfano; wanaangalia resistance ilivyo. Wakati mwingine inawezekana mtu akawa amesimama tu au ameshikilia kitu au wakati mwingine ameshikilia silaha, kwa hiyo vile vile maamuzi ya kumkamata yanategemea aina ya mtuhumiwa mwenyewe mazingira yake aliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia inetegemea aina ya silaha ambazo polisi anazo, inategemea vilevile utafiti ambao polisi wanafanya kabla, mbinu gani watumie. Wanaweza wakahitaji kupata taarifa za kiintelijensia kabla ya kumkamata muhusika. Niliona nitoe ufafanuzi huo ili nieleweke vizuri. Hata matumizi ya nguvu kwa wale ambao ni majambazi au wanaotumia silaha nao kuna utaratibu wake kwa mujibu wa PGO namba 7 na 8.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kujibu specifically suala la watu ambao wanawataja itategemea na mambo yote ambayo nimeeleza, kwamba je, mazingira ambayo mtuhumiwa alikuwepo yalikuwa ni yapi? Sasa kusema sasa hivi kwamba mtu fulani alikuwa amechukuliwa hatua gani kwa maelezo ya hapo moja kwa moja, nadhani cha msingi ni kwamba tunashughulika na kesi kwa kesi kulingana na aina ya mtuhumiwa jinsi ambavyo ametenda lile kosa. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved