Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Primary Question

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:- Idadi ya watu nchini inazidi kuongezeka, ongezeko hili linaenda sambamba na ongezeko la mahitaji ikiwemo ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji ili waendeshe shughuli zao katika maeneo madogo lakini kwa tija kubwa na kuwaondolea adha wanazozipata?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niipongeze sana Serikali kwa mkakati huu mzuri ambao umeiuweka na kwa sehemu imetekeleza lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile moja kati ya migogoro ambayo inatokana na tatizo hili ambalo limeelezwa ni migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Na kwa vile migogoro hii kwa sehemu kubwa inachangiwa na ukosefu wa mipango bora ya matumizi ya ardhi kwa baadhi ya maeneo, na kwa vile pamoja na jitihada nzuri za Serikali migogoro hii imechangiwa na Halmashauri za wilaya hasa watumishi ambao hawapo tayari kwenda kufanya kazi hii bila kulipwa posho, sasa je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba vijiji vyote ambavyo havina mpango bora wa ardhi vipatiwe mpango huo? Na pili ina mpango gani kuhakikisha kwamba watumishi ambao hawapo tayari kwenda kufanya kazi hizi bila kupata posho wanachukuliwa hatua?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama kwa kuijali sana hii sekta ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, hata viwanda vinategemea sana sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vijiji ambavyo hadi sasa havina mipango ya matumizi bora ya ardhi tunayo changamoto kubwa sana, moja, ili kijiji kipime, kiwe na mpango wa matumizi bora ya ardhi yake bajeti ambayo inahitajika angalau kuweza kuwezesha upimaji huo inaanzia kati ya shilingi milioni tano hadi milioni nane na baadhi ya vijiji ambavyo ni vikubwa hadi milioni kumi. Sasa kwa sababu Halmashauri nyingi bado hazijawa na uwezo wa kuwa na fedha hizo utekelezaji umekuwa ni wa pole pole sana, ikiwemo Halmashauri yake ya Madaba hadi sasa ni vijiji nane tu ndio vina mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa wito kwa vijiji ambavyo vina fedha, vipo vijiji ambavyo vina fedha, vigharamie mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa manufaa ya kiuchumi ya wananchi wa vijiji hivyo. Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini wafanye mapitio ya vijiji vyote na kuvishauri vile ambavyo vina uwezo wa kugharamia zoezi hilo viweze kugharamia, na vile ambavyo havina kabisa uwezo halmashauri ijipange kugharamia.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunawachukulia hatua gani watumishi ambao hawataki kwenda kufanya kazi vijijini hadi walipwe posho. Nataka nitoe angalizo kwao, kwamba walipoajiriwa walipewa maeneo ya kufanya kazi. Kama mtu amepewa eneo la kijiji halafu ndani ya kijiji hataki kufanya kazi mpaka alipwe posho huyu mtu tunatakiwa tupate taarifa zake mapema iwezekanavyo ili tuweze kumchukulia hatua na Wakurugenzi wa Halmashauri waanze kuchukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa maagizo wale watumishi ambao wana mazoea ya kukaa Makao Makuu ya Halmashauri bila kwenda kutembelea vijiji waanze kupangiwa kazi na Wakurugenzi wa Halmashauri bila kujali kama kuna posho au hakuna, ili mradi tu aweze kuwezeshwa vyombo vya usafiri vya kuweza kuwafikisha kwenye vijiji wanavyotakiwa kwenda kufanya kazi, basi. Kwa hiyo, hiyo ndio ushauri wangu na maelekezo yangu kupitia Bunge lako Tukufu.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru sana Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa majibu yake mazuri kulingana na swali lililoulizwa juu ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi. Wizara imejipanga vizuri katika mwaka wa fedha unaokuja kwa ajili ya kupima maeneo ambayo yana migogoro mingi, hasa yale maeneo yanayozunguka kwenye mbuga za wanyama. Tayari ile Tume ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi imeshaingia makubaliano pia na wenzetu wa TANAPA, kwa hiyo kuna vijiji vingi ambavyo vitapimwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo tukumbuke tu kwamba mpango wa kupanga matumizi bora ya ardhi au masuala ya mpango miji ni jukumu la Halmashauri zenyewe husika. Kama alivyosema Naibu Waziri bado pia vijiji na maeneo ambayo yanakuwa na pesa wanayo fursa hiyo. Kama Wizara tuna-facilitate uwezekano wa kuweza kuwapa elimu na namna bora ya kupima, lakini Wizara tumejipanga vizuri na tutakwenda kupunguza sana kero hii. Kwa hiyo, tunachowaomba sana wananchi tuwe tayari katika suala hilo.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba niongezee na niliarifu Bunge lako tukufu kwamba Wizara ya Kilimo tumeandaa mpango mkakati wa kilimo ASDP II ambao utahusisha zaidi ya Wizara sita. Hata hivyo kutokana na swali la msingi ni kwamba katika hizi green house tumepanga kila halmashauri iweze kuwa na green house ili wananchi waweze kujifunza, kwa sababu hizo green house ambazo tunazizungumzia zinachukua eneo dogo lakini uzalishaji wake unakuwa ni mkubwa zaidi na vile vile ni katika kuendeleza hii tasnia yetu ya horticulture.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni kwamba Wizara tunatoa mafunzo na maelekezo ambayo yanafanyika kwa kutumia udongo na teknolojia mbalimbali za kuhifadhi udongo huo ili kuzuia mmomonyoko na vile vile kuweza kuongeza tija kwa ajili ya kupunguza tatizo hili nililolisema, ahsante.