Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Daniel Edward Mtuka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Primary Question
MHE. DANIEL E. MTUKA aliuliza:- Taarifa ya Idara ya Upimaji wa Ramani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inalitaja eneo la Chisinjisa lililopo Wilaya ya Manyoni kuwa ndipo alama pekee ya katikati (center point) ya Tanzania inapatikana. • Je, ni lini Serikali italitambua rasmi eneo hili na kulitangaza katika Gazeti la Serikali? • Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendeleza na kulitangaza eneo hili ili kuvutia utalii wa ndani na nje kama chanzo cha mapato?
Supplementary Question 1
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Huu ni ubunifu mkubwa na wa kupongezwa kwa wananchi wa Manyoni Mashariki kwamba tuwe na eneo sasa litambuliwe la katikati ya nchi, na kwa sababu taarifa za awali zinaonyesha kwamba eneo hili liko kwenye Manyoni Mashariki. Nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa Serikali imeona umuhimu wa kulitambua, kulipima na kulitangaza eneo la katikati ya nchi kwa lengo la kukuza utalii; na kwa kuwa wananchi wa Manyoni wako tayari kushirikiana na Serikali katika kuliendeleza eneo hilo pamoja na kujenga mnara mrefu ambao utawekwa taa au bendera ya Taifa.
Je, Waziri anaweza kutoa maelekezo sasa hivi hapa ndani amuagize Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani aanze kazi hiyo mara moja ya kulitambua eneo hili? (Makofi)
(b) Kwa kuwa lengo kubwa hapa ni kukuza utalii na kuongeza vivutio vya watalii, tunayo hazina ya mali kale, kubwa eneo la Kilimatinde pale Manyoni.
Je, Waziri na Maliasili na Utalii atakuwa tayari kufuatana na Mbunge kwenda kuona eneo hilo ambalo ni hazina kubwa ya kumbukumbu za biashara ya utumwa pamoja na ngome za wakoloni? (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza amesema je, niko tayari pengine kutoa tamko hapa, ili Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani aende aanze kufanya kazi hiyo; nadhani katika jibu langu la msingi nimesema kwamba Wizara sasa tayari inaweka mikakati ya kuweza kufanya ufatiliaji wa karibu, kwa sababu tumeona kuwa na eneo ambalo linatambulika kama ndilo center (katikati) ya nchi si tu kwamba tutatambua eneo hilo na kuliacha kama lilivyo, lakini bado ni sehemu ambayo inaweza ikatumika pia kama utalii. Ndiyo maana nimesema uendelezaji wa eneo hilo, unaweza ukafanyika katika mustakabali wa kutaka patambulike.
Mheshimiwa Spika, na kwa sababu wananchi wa Manyoni Mashariki wanasema wako tayari kushirikiana mara zoezi hilo litakapoanza tutawashirikisha kwa pamoja ili tuweze kuona suala lile linafanyika katika umakini zaidi ili kuweza kupafanya pawe kivutio cha kweli.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili la kuweza kutambua vivutio vilivyoko katika maeneo ya Kilimatinde, nadhani hili ni la Wizara ya Utalii, lakini kwa sababu wote tunajenga taifa moja, tutashirikiana na wenzetu kuweze kuona maeneo hayo yanatambulika na yanaingia katika historia, lakini pia kuweka kama vivutio vya utalii ili paweze kufikika pia na patakuza soko la utalii kwa nchi yetu.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Manyoni.
Mheshimiwa Spika, Mbunge wa Manyoni tunamshukuru sana kwa kutupa taarifa ya malikale hizo ambazo ziko katika eneo hilo na ninataka nimhakikishie kwamba tuko tayari kutembelea eneo hilo na kufanyia kazi vivutio hivyo, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved