Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Bwawa la Lukuledi ambalo huhudumia Kata za Lukuledi, Mpanyani na Chikinja ni muhimu sana kwa wananchi. Je, Serikali itafanya lini ukarabati wa bwawa hilo kwa sababu kiwango cha maji kinapungua kwa kujaa mchanga?
Supplementary Question 1
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza ningependa kutambua kazi inayofanyika kwenye Kata ya Mwena, Chikundi pamoja na Chigugu ya kusambaza miundombinu kwa ajili ya maji na Mheshimiwa Waziri wa Maji ametoa ushirikiano mkubwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa hili la Lukuledi tunalolitaja hapa sasa hivi kwa mara ya kwanza kabisa lilichimbwa mwaka 1955 lakini mpaka sasa hivi limekauka zaidi ya mara tano kwa sababu linategemea tu maji ya mvua kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuiongezea nguvu Mamlaka ya Maji Safi Masasi (MANAWASA) kwa kazi nzuri inayofanywa na Engineer David ili waweze kufikisha maji Kata ya Lukuledi na vijiji vyake vyote maji safi na salama badala ya kuendelea na huo mradi wa bwawa?
Swali la pili, pamoja na nia njema kabisa ya Serikali kutaka kuweka mabwawa kwenye maeneo waliyoyataja hapo ya Chingulungulu, Mihima pamoja na Mpanyani lakini tu niseme wanachokisema hapa sasa hivi, mwaka huu wametenga kazi ya usanifu.
Je, nini nia ya Serikali kuhakikisha wanawaondolea wananchi hawa taabu ya kupata maji kwa siku zijazo kwa sababu bajeti ya mwaka huu inaonesha tu ni kazi ya usanifu peke yake? (Makofi)
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza ya swali lake ni kweli kwamba bwawa hili limekuwa linapata matatizo makubwa ya kukauka kwa sababu mbalimbali, lakini miongoni mwa sababu hizo ni kujaa mchanga na matatizo mengine yanayosababishwa na kutotunza mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo lake kwamba tuwaambie MANAWASA wapeleke maji katika maeneo hayo badala ya kutegemea bwawa lile, naomba sana nimshauri tusubiri usanifu wa kina ukamilike, usanifu huo utatushauri kama chanzo hicho kitatosheleza mahitaji ya maeneo hayo na kama usanifu huo utashauri kwamba chanzo hicho hakitatosheleza basi tutaona njia nyingine ya kupata chanzo kingine ikiwemo hiyo ya kuchukua maji kutoka kwenye chanzo kilecha Mbwinji ambacho ndiyo kinategemewa na MANAWASA, kwa sasa hivi naomba sana tusimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutachukua maji kutoka Mbwinji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu kwenye sehemu hii ya swali la kwanza, ninamuomba sana usanifu utakapokamilika, kama utakaposhauri kwamba wananchi watunze mazingira na wengine watapisha katika eneo la mita 500 kutoka kwenye chanzo kwa ajili ya utunzaji wa mazingira ya bwawa basi naomba sana ashiriki kuwaelimisha wananchi wakubali hatua hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya swali ameonesha wasiwasi kwamba mwaka huu tuna bajeti ya kufanya usanifu peke yake, ndiyo tumetenga shilingi milioni 60 ili tufanye usanifu wa kina na ukamilike na DDCA wamepewa hiyo kazi wakamilishe usanifu mwaka huu wa 2017/2018. Watakapotupatia gharama sasa hapo ndiyo tutapanga lini utekelezaji utaanza kwa kushirikiana na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuondolea wasiwasi kwamba suala hili kwa sababu sasa limeletwa katika utaratibu wa vipaumbele, asiwe na wasiwasi awahakikishie wananchi kwamba tutatekeleza mradi huu ndani ya mwaka mmoja.(Makofi)
Name
Flatei Gregory Massay
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:- Bwawa la Lukuledi ambalo huhudumia Kata za Lukuledi, Mpanyani na Chikinja ni muhimu sana kwa wananchi. Je, Serikali itafanya lini ukarabati wa bwawa hilo kwa sababu kiwango cha maji kinapungua kwa kujaa mchanga?
Supplementary Question 2
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa swali hili la Ndanda la Bwawa la Lukuledi linafanana kabisa na bwawa lililopo Mbulu Vijijini, Bwawa la Mangisa ambalo linahudumia Kata ya Yaeda Ampa, Bashay na Gidihim na hali yake kwa kweli inaelekea kuisha kabisa kwa sababu linakauka.
Je, Serikali itatusaidiaje ili hili Bwawa la Mangisa liweze kupatiwa ufumbuzi ili vijiji nilivyovitaja viendelee kupata huduma ya maji?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufanya clarification vizuri katika maswali yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Mbulu kweli kuna changamoto kubwa ya hili bwawa ambalo Mheshimiwa Flatei analizungumzia, lakini naomba nikiri wazi kwamba miundombinu ya mabwawa katika maeneo mbalimbali imeendelea kuathirika siku hadi siku na kushindwa kuhakikisha uwezo wake unapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hiyo changamoto kubwa ni suala zima ambalo hata Naibu Waziri hapa amezungumza, uharibifu mkubwa wa mazingira katika vyanzo vya maji, watu wanapenda katika maeneo ya mabwawa kuweka mashamba, kinachotokea ni kwamba mvua inavyonyesha udongo unatiririka kutoka mashambani unaenda kujaza katika mabwawa na mabwawa haya yanakufa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Flatei tumeisikia hoja yako tutawatuma wataalam kwenda kufanya uhakiki kuangalia nini kinachotakiwa kufanyika pale. Hata hivyo, naomba niwasihi viongozi wote katika maeneo mbalimbali hasa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, wahakikishe kwamba katika suala la vyanzo vya maji hasa mabwawa kuzuia vitendo vya shughuli za kibinadamu hasa kilimo, kwa sababu jambo hilo linaharibu miundombinu ya mabwawa katika nchi yetu. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved