Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mussa Ramadhani Sima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Primary Question
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:- Tunatambua kuwa michezo duniani kote imekuwa chanzo cha mapato na kuinua uchumi wa Taifa husika, lakini nchini Tanzania michezo hususan soka imebaki kuwa burudani tu. (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuinua Soka la Tanzania? (b) Je, kuna mahusiano gani kati ya Serikali na TFF katika kuimarisha soka la Tanzania kuanzia ngazi ya Wilaya? (c) Je, Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) linapata fedha za ruzuku kiasi gani toka FIFA na Wadhamini kama TBL na Serengeti Breweries?
Supplementary Question 1
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na niipongeze Serikali kuwa wazi kwenye swali hili. Pia ni-declare interest, mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka, Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Na. 12 ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1971 na Kanuni za Usajili wa Vyama vya Michezo, Namba 442 ya mwaka 1999, kifungu cha 7(2)(c)(ii), inatambua mamlaka ya Waziri na Waziri ndiyo mwenye maamuzi ya mwisho ya vyama vya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini viko baadhi ya vyama katiba zao hazitambui mamlaka ya Waziri na vyenyewe ndiyo vyenye mamlaka ya mwisho ikiwemo TFF. Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana, ikikupendeza kama utakuwa tayari kulinda, kuheshimu na kusimamia sheria hii iliyotungwa na Bunge na kuhakikisha vyama hivi kwenye katiba zao zinatambua role ama wajibu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, Serikali imekiri wazi katika ruzuku ambayo inatolewa TFF ni zaidi ya bilioni 10 na ile dola milioni tatu tunazungumzia karibu bilioni saba, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, kama utakuwa tayari uiombe TFF ilete mpango kazi kwenye mikoa yetu ili tuweze kujua fedha hizi zinatumikaje. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Juliana Daniel Shonza
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Sima kwa sababu amekuwa ni mwanamichezo mahiri na vilevile ni mdau mkubwa sana wa michezo katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na kujibu swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kama kuna vyama vya mpira ambavyo havitambui mamlaka ya Waziri. Mimi niseme kwamba tunatambua kabisa kwamba TFF pamoja na viongozi wake wote wanapaswa, wanalazimika na hivyo wanatambua mamlaka ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Ukisoma Katiba ya TFF, Ibara ya 1(2) inasema kwamba TFF ni chombo cha mpira ambacho kimesajiliwa chini ya Sheria ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967 kama ambavyo umesema na marekebisho yake ya mwaka 1971. Kwa maana hiyo sasa, kimsingi kwa sababu Baraza la Michezo ambalo ndiyo ambalo linasajili TFF liko chini ya Wizara ya Habari, kwa maana lipo chini ya Waziri husika mwenye dhamana ya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu TFF iko chini ya Baraza la Michezo, kwa hiyo, kimsingi ni kwamba TFF inapaswa kutambua mamlaka ambayo Waziri kwa maana ya Serikali inayo. Naamini kabisa kwamba TFF inatambua mamlaka ya Waziri kwa sababu ni takwa la kikanuni na kikatiba na wanapaswa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikija kwenye swali lako la pili ambapo unataka kujua hizi fedha za FIFA Forward ambazo zimetolewa, unaiomba Serikali iweze kuishauri TFF iweze kutoa mchanganuo wa fedha hizo mapema. Mheshimiwa Sima natambua kabisa kwamba wewe ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu katika Mkoa wa Singida na kwa jinsi mimi ninavyotambua ni kwamba humu ndani tuna Wabunge wengi ambao ni viongozi wa vyama vya mipira. Kwa hiyo, najua kabisa kwamba ninyi kama Wenyeviti pamoja na Makatibu ndiyo mhimili mkubwa kabisa wa TFF lakini kimsingi ninyi ndio washauri wakubwa wa TFF. Kwa hiyo, kwa sababu TFF ina taratibu zake, ina mikutano yake ambayo huwa mnakaa na kila mwaka huwa mnakutana, mna mkutano wa robo mwaka, nusu mwaka pamoja na wa mwaka, naamini mtakapokutana ninyi mna nafasi kubwa kabisa ya kuweza kuishauri TFF ili kuweza kuandaa huo mchanganuo wa fedha.
Niseme kabisa sisi kama Serikali tumelipokea wazo lako na tunakubaliana kabisa na wazo lako kwa sababu tunajua kwa namna moja au nyingine litasaidia kuweka uwazi wa mapato na matumizi na kuondoa sintofahamu ambazo zilikuwepo siku za nyuma. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved