Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Salma Rashid Kikwete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Primary Question
MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza:- (a) Kwa kuwa elimu ni haki ya kila mtoto, je, Serikali inawasaidiaje watoto wenye usonji ili nao wapate elimu? (b) Je, Walimu wanaofundisha watoto hao wanatosheleza kwa mujibu wa ikama? (c) Kwa kuwa watoto hao wana mazingira tete, je, Walimu wao wana utaalam wa kutosha?
Supplementary Question 1
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Pia namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Sheria Namba Tisa ya Mwaka 2010 inamzungumzia mtoto mwenye ulemavu kupata haki ya elimu pamoja na kulindwa. Watoto hawa wenye usonji, kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi wana mazingira tete. Sasa je, nili lini, au je, upi ni mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata elimu toshelezi katika mazingira yao ya miundombinu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, watoto wenye usonji kwa kawaida wanatakiwa kila watoto watano wawe na Mwalimu mmoja. Sasa katika majibu ya msingi tunaambiwa watoto wapo 1,416 na Walimu wapo 157, maana yake watoto hawa wanatiwa wawe na Walimu wasiopungua 283. Sasa je, ni lini Walimu hawa watapewa elimu stahiki ili waweze kuwapa watoto wenye ulemavu, hasa usonji elimu inayostahiki? Ahsante. (Makofi)
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, yeye ni mdau mkubwa wa elimu na kwa kweli hasa katika elimu maalum ametoa mchango mkubwa sana wa mawazo kuhusu kuendeleza watoto hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wenye usonji mara nyingi huzaliwa kawaida na usonji huanza kuonekana baada ya mwaka mmoja na nusu hadi miaka miwili. Kwa hiyo, wazazi wengi wamekuwa wakipata shida ya kuwatambua vizuri kwamba huyu mtoto ana usonji, kwa hiyo, imekuwa vigumu hata kuwaratibu. Matokeo yake wengine wamekuwa labda wakiwapiga wanadhani ni watukutu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao mpango maalum wa kwanza kuwatambua watoto hao wote na kuwasajili ili hatimaye tuhakikishe kwamba wote wanapata elimu kama ilivyo haki ya kila mtoto Mtanzania kupata elimu. kwa hiyo, mkakati wetu tutaanza zoezi la kuwatambua na kuwasajili ili hatimaye wapate elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, nakubaliana naye kwamba katika kila watoto watano wanatakiwa kuwa na Mwalimu mmoja lakini standard ambayo ni nzuri sana ya Kimataifa inatakiwa anapomfundisha amfundishe akiwa peke yake (one to one), hiyo ndiyo standard ya kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, upungufu wa walimu waliopo sasa hivi wanaofundisha shuleni ni mkubwa kama alivyoainisha. Hata hivyo, kwa kuwa tunao Walimu wengine ambao wameshapata mafunzo hayo kule Patandi halafu bado hawajahamishiwa kwenye hizo shule ambazo zinafundisha watoto hawa kwa sasa, ndiyo maana nimetoa agizo kwamba ifikapo Desemba wawe wamehamishiwa kwenye hizi shule ili kusudi watoto hawa waweze kupata haki yao ya msingi kabisa ya elimu.
Name
Susan Anselm Jerome Lyimo
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza:- (a) Kwa kuwa elimu ni haki ya kila mtoto, je, Serikali inawasaidiaje watoto wenye usonji ili nao wapate elimu? (b) Je, Walimu wanaofundisha watoto hao wanatosheleza kwa mujibu wa ikama? (c) Kwa kuwa watoto hao wana mazingira tete, je, Walimu wao wana utaalam wa kutosha?
Supplementary Question 2
MHE. SUSAN A.LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba kuna tatizo kubwa la upungufu wa Walimu hawa, lakini nina taarifa kwamba tuna Walimu wengi sana waliosoma katika vyuo kwa mfano Chuo cha Tabora cha Viziwi, wamesomea kufundisha watoto hawa, lakini wapo mitaani na wana resources.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kwa nini Serikali isiwachukue Walimu hawa ambao wamesomea kwa miaka mitatu degree zao na kuendelea kuchukua Walimu ambao wamepata kozi za juu juu tu za mafunzo kazini wakati tunajua tuna tatizo kubwa sana la Walimu kwa ajili ya watoto hawa wenye ulemavu mbalimbali pamoja na viziwi na hawa wengine wa usonji? (Makofi)
Name
Joseph George Kakunda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sikonge
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Susan Lyimo kwa sababu kwanza amekuwa ananiletea maswali mengi hata kwenye karatasi, vi-note na nimekuwa nikimpa maelezo ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili namuahidi katika Walimu ambao tutawaajiri hivi karibuni, kipaumbele kitakuwa ni kwa hawa ambao wana taaluma ya elimu maalum ambao hawajaajiriwa ili waajiriwe haraka waweze kutusaidia katika shughuli zetu.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved