Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Primary Question

MHE. ANDREW J. CHENGE aliuliza:- Katika miaka ya 1980 wanakijiji wa Kijiji cha Mwanchumu, Salaliya na Matongo walitoa maeneo yao kwa Serikali ili yatumike kwa shughuli za kilimo zilizokusudiwa na Gereza la Matongo lakini kwa sasa maeneo hayo hayatumiwi na Magereza kikamilifu. Je, Serikali ipo tayari kurejesha eneo hilo ambalo halitumiki kikamilifu kwa wananchi wa vijiji hivyo?

Supplementary Question 1

MHE. ANDREW J. CHENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Gereza la Matongo ni miongoni mwa Magereza yaliyoanzishwa na Serikali katikati ya miaka 1970 kwa lengo hilo hilo ambalo Waziri amesema katika jibu lake, lakini zaidi ya miaka 40 ukifika pale Matongo hakuna cha maana kinachoendelea. Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake anasema Gereza hili limo kwenye mpango wa kuboresha kilimo, ni lini mpango huu mahsusi kwa Gereza la Matongo utaanza kutekelezwa na Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ametambua mazao yanayolimwa katika eneo hilo likiwepo eneo lenyewe la Matongo. Je, yuko tayari na ikiwezekana kushirikiana na Mbunge wa eneo hilo kutafuta mwekezaji ili kuanzisha kiwanda ili kuongeza thamani ya mazao yatakayolimwa na Magereza lakini pia kusaidia soko kwa wananchi ambao wanazunguka eneo hilo? Ahsante. (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza nimeshamjibu katika majibu yangu ya msingi, naomba tu nichukue fursa hii kufafanua. Nimesema kwamba tuna mkakati wa kuhakikisha kwamba Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula. Kwa sasa hivi Jeshi la Magereza linajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 30, malengo yetu ni kuhakikisha kwamba tunafikia asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu utatekelezwa baada ya kuhakikisha kwamba tumepata fedha za kutosha kuwekeza. Katika bajeti ya maendeleo ya mwaka huu tunatarajia kupata takribani shilingi bilioni 3 ambazo zitatumika katika moja ya mikakati ya kuimarisha kilimo pamoja na kujitosheleza katika Magereza yetu. Pia tuna mpango vilevile kupitia jitihada za Mheshimiwa Waziri Mkuu kupata matrekta 50 kwa kuanzia ambayo tutayapeleka katika Magereza ikiwemo Gereza hili la Matongo ili kuweza kusaidia kuimarisha kilimo katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira lakini ni jambo ambalo tayari liko katika hatua nzuri za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba kama Serikali iko tayari kushirikiana na mwekezaji kuwekeza. Ndiyo mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba nchi yetu inafikia uchumi wa kati kupitia viwanda. Kwa hiyo, nina uhakika kabisa Mheshimiwa Mbunge akiweza kuwasiliana na mamlaka husika kwa maana ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji atapata mwongozo na msaada mzuri wa kuweza kusaidia jitihada za Serikali za kuimarisha viwanda katika nchi yetu. Sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pale ambapo tunaweza kutoa mchango wetu kwa namna yoyote ile tutakuwa tayari kushirikiana naye.