Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Omary Tebweta Mgumba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Primary Question

MHE. OMARY T. MGUMBA aliuliza:- REA I na II ilikuwa ni kupeleka miundombinu ya umeme vijijini na baadhi ya Makao Makuu ya vijiji tu na kuacha vitongoji vya vijiji husika. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwapatia umeme vitongoji vyote na vijiji vilivyorukwa katika REA I na II?

Supplementary Question 1

MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake anasema kwamba REA Awamu ya Tatu lengo lake kubwa ni kupeleka umeme katika vijiji ambavyo havina miundombinu ya umeme, lakini kosa lile lile lililofanyika katika REA I na II, kuruka Vitongoji na Vijiji tumeliona tena katika REA hii ambayo inatekelezwa. Kwa mfano, sasa hivi kimepewa Kijiji cha Bagilo ambapo vimerukwa Vijiji vya Hewe, Mgozo na Tegetero, lakini pia...
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kidunda kimepewa, vimerukwa vijiji vya Mkulazi na Chanyumbu; je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia vijiji hivyo ambavyo vimerukwa katika REA III ili tusirudie kosa lile la REA I na II?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mradi huu umeanza. Ni kweli umeanza, lakini mkandarasi huyu ana miezi sita sasa tangu alipokuja kufanya tathmini tu, hajarudi site mpaka leo. Baada ya kumfuatilia inaonekana kwamba hajapewa advance wala letter of credit ya kuanza kazi. Katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri anasema mradi huu unatakiwa ukamilike Julai, 2019, mpaka leo kazi haijaanza. Je, ni lini Serikali itaweza kutoa letter of credit kwa mkandarasi huyu ili aweze kuanza kupata vifaa na vitendea kazi ili aweze kuanza mradi na kutekeleza ndani ya wakati? (Makofi)

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza lazima nimpongeze Mheshimiwa Mgumba kwa kazi anayoifanya. Ndani ya kipindi kifupi amkeshauliza zaidi ya maswali manne ya Sekta ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza alijielekeza kwenye changamoto zilizojitokeza katika REA ya I na REA II ya urukwaji wa vijiji. Naomba nikiri kweli changamoto hiyo ilikuwepo, lakini pia naomba niseme kupitia mradi huu wa REA Awamu ya Tatu, baada ya kupokea maombi mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge, awali mpango ulikuwa ni vijiji 3,559 lakini baada ya kupokea malalamiko ya kurukwa kwa vijiji, vitongoji na taasisi za umma tumefanya tathmini nyingine na upembuzi yakinifu, tumepata vijiji kama 1,541 ambavyo vinatakiwa viongezeke awamu hii tunapoendelea kutekeleza mzunguko huu wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge vijiji alivyovitaja ni miongoni mwa vijiji 1,541 ambavyo vitaongezeka kwenye vijiji 3,559 na vitakuwa vijiji 5,100 kwa awamu ya kwanza ambavyo vitapelekewa miundombinu ya umeme. Pamoja na kwamba nakiri, lakini gharama zitaongezeka. Pia kwa kuwa kazi ya Bunge hili ni kuidhinisha bajeti kwa miradi hiyo na uhitaji unaonekana ni mkubwa, sina mashaka kwamba Bunge litatimiza wajibu wake na kwamba vijiji ambayo tumeviona lazima viongezeke ili kutimiza lengo ambalo limekusudiwa kwamba tusirudie makosa ya awamu nyingine, litatimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, amejielekeza kwamba ni kweli Mkandarasi wa Mkoa huu wa Morogoro, State Grid alifanya tathmini na kwamba hajalipwa advance. Nataka niseme wakati wa malipo ya advance kulikuwa na masharti na sharti mojawapo lilikuwa malipo lazima wa-submit performance bond. Bahati mbaya mkandarasi huyu haku-submit kwa wakati, lakini nakiri mpaka sasa hivi Wakandarasi wote wamesha-submit, utaratibu wa malipo unaendelea kwenye Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, utaratibu wa ufunguaji wa letter of credit, tunashukuru tumepokea barua wiki iliyopita kwamba sasa tunaweza tukaendelea na utaratibu huo. Kwa hiyo, tunajipanga pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini ili kuifanya kazi hiyo kwa haraka na miradi hii itekelezeke kwa haraka. Ahsante. (Makofi)