Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:- Bagamoyo ni mji mkongwe wenye vivutio vya kitalii kama ilivyo miji mingine nchini kama vile Zanzibar, Kilwa na Mapango ya Amboni, Tanga. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha vituo vya kitalii nchini ikiwemo Bagamoyo ili kupata wageni wengi zaidi na kukuza pato la Taifa?

Supplementary Question 1

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa hali ya utalii kwa sasa hivi imeshuka kutoka asilimia 12.9 na kufika asilimia 3.3 na Mji wa Bagamoyo wanategemea uvuvi na utalii na kuonekanika mahoteli mengi ya kitalii ya Bagamoyo kukosa wageni, je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inatangaza vituo vya utalii vya Bagamoyo na kuangalia ni tatizo gani lililofanya kushuka kwa asilimia hii ya utalii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa majengo ya kale ya mji mkongwe wa Bagamoyo yamekuwa yanabomolewa na ramani za majengo yale yanatoweka ambapo yalikuwa ni kivutio sana kwa utalii, lakini ramani zile za kale zinapotea na kujengwa katika miundombinu mingine tofauti, je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha majengo yale yanaboreshwa kurudi katika hali ile ya mji mkongwe?

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya utalii kwamba imeshuka kutoka asilimia 12 hadi asilimia tatu katika eneo la Bagamoyo, hii kwa kweli inahitaji labda nipitie takwimu vizuri. Kilichojitokeza zaidi ni kwamba katika hoteli nyingi za kitalii zile za Bagamoyo zilikuwa zinategemea sana uendeshwaji wake wa mikutano, yaani utalii ule wa mikutano ambao ulikuwa unaendeshwa sana Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivi sasa mikutano mingi imepungua kutokana na mabadiliko ya hali ya uchumi. Hata hivyo, kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuamua kuchukua mashirika yetu yaliyoko chini ya Wizara ili yaweze kukabidhiwa hii dhamana ya kutangaza maeneo yote yaliyoko Bagamoyo ikiwemo na ile Hifadhi nyingine ya Saadan kusudi iweze kuvutia watalii zaidi waendelee kuwepo na kuongezeka kule Bagamoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu majengo ambayo yamekuwa yakiharibiwa na kubomolewa ramani zao zile za awali, ni azma ya Serikali kuendelea kuwahamasisha wananchi wanayoyamiliki hayo majengo kuhakikisha kwamba wanafuata taratibu za kurudishia ujenzi uliokuwepo kabla. Kwa sababu katika eneo lile tunataka majengo yale yaendelee kuwa na ramani na sura iliyokuwa inaonekana toka awali ili iendelee kuwa kivutio kwa upande wa wageni.